Edward Lowassa,Familia Yake Wachangia Ujenzi Wa Dayosisi Mpya ya Shinyanga na Simiyu Millioni 21


 

Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa
KANISA la Kiinjili na Kilutheli Tanzania (KKKT), linalotarajia kuanzisha Dayosisi mpya ya Shinyanga na Simiyu limefanikiwa kukusanya Sh milioni 116 taslimu ambapo kati ya hizo, Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa na familia yake walichangia Sh milioni 21.

Katika harambee hiyo, Mchungaji wa KKKT, Philbert Celestine alimshukuru Lowassa na familia yake pamoja na wageni waalikwa kwa kufanikisha mchango huo ambao ulivuka lengo.

Awali, harambee hiyo ilikuwa na lengo la kupata Sh milioni 114 ili kukamilisha ujenzi wa kanisa hilo lakini walifanikiwa kuvuka lengo na kupata Sh milioni 204, kati ya hizo fedha
tasilimu zikiwa ni Sh milioni 116.

Kwa upande wake, Lowassa akizungumza waumini hao, alisema kuwa suala la ujenzi wa makanisa nchini ni zuri na ni vema kwa sasa kutokuwategemea wafadhili kama ilivyokuwa awali na badala yake tubadilike kwa kujenga sisi wenyewe.

“Zamani tulikuwa tumezoea kujenga makanisa kwa kuwategemea wafadhili mbalimbali kutoka nje ya nchi hasa wazungu, lakini kwa sasa tubadilike tujenge wenyewe kwani uwezo tunao wa kuchangishana,” alisema Lowassa.

Lowassa alisisitiza kuwa yeye yupo tayari kurudi akiitwa katika harakati zozote za kuchangia ujenzi wa nyumba za ibada. Askofu wa Dayosisi ya Mashariki ya Ziwa Victoria, Andrea Gule akitoa shukrani zake katika harambee hiyo, aliwataka wananchi na waumini kwa ujumla kuwa na moyo wa kuthubutu katika kuchangia ujenzi hasa wa nyumba za ibada ili kuwakomboa
watu kiroho.*Habari Hii na Raymond Mihayo, Shinyanga

Nahodha: Sitta lete ushahidi wa Mwakyembe


Fidelis Butahe
WAZIRI wa Mambo ya Ndani, Shamsi Vuai Nahodha amemtaka Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samwel Sitta kuwasilisha ushahidi wa madai aliyoyatoa juzi kuwa Naibu Waziri wa Ujenzi, Dk Harrison Mwakyembe alilishwa sumu.

Juzi akiwa na kundi la makada wenzake wa CCM wanaojipambanua kuwa wapambanaji wa ufisadi, katika uzinduzi wa Programu ya Neno la Hekima kutoka kwa Kiongozi iliyoanzishwa na Kanisa la Ufufuo na Uzima, Sitta alirejea kauli yake ya awali kuwa Dk Mwakyembe ambaye pia Mbunge wa Kyela, alilishwa sumu.

“Nasema Dk Mwakyembe kapewa sumu. Kama vyombo vya uchunguzi vinasema siyo, basi watueleze ukweli, tena haraka,” alisema Sitta na kushangiliwa na maelfu ya waumini wa kanisa hilo na kuongeza:

“Vipi uone binadamu ambaye ukimshika katika ngozi unga unamwagika chini, mhudumu anakuja kuufagia lakini baada ya saa moja unarudi tena, kitu hicho siyo cha kawaida. Wamejaribu, wameshindwa kwa kuwa Dk Mwakyembe analindwa kwa jina la Yesu ambalo ni kubwa kuliko yote.

Kwa hiyo nuksi, kurogwa kuwekewa sumu ni kama maji katika mgongo wa bata, yanatiririka tu na kwenda zake.” Alisema mafisadi wapo kwa ajili ya kuangamiza taifa na kuwaangamiza viongozi wanaotetea maslahi ya wananchi akidai kwamba sasa siku zao zina hesabika. Akizungumza jana, Vuai alisema ushahidi ukija suala hilo linaweza kuchunguzwa huku akihoji:

“Ulimwuliza Sitta kama ana uhakika.” Hata hivyo, Vuai alisema masuala yote yanayohusu uchunguzi hayawezi kuzungumzwa katika vyombo vya habari na kwamba ni mambo ambayo hufanyika kwa umakini mkubwa… “Labda nikueleze kitu… hilo suala unalolisema mimi sijalisikia ila kama amezungumza hivyo basi alete ushahidi.”

“Kwanza hilo jambo la Sitta kusema Mwakyembe kalishwa sumu unaniuliza mimi? Kwa nini usimtafute huyo Sitta ili akueleze vizuri ili ujiridhishe?” Alisema suala kama hilo linapotokea na mhusika akawa na ushahidi anatakiwa kuuwasilisha sehemu husika na kwamba kuzungumza kitu bila kuwa na ushahidi haisaidii huku akisisitiza kuwa mpaka sasa hakuna mtu yoyote aliyejitokeza kutoa madai hayo.

Dk Mwakyembe aliondoka nchini Desemba 9, mwaka jana kwenda katika Hospitali ya Appolo, India kwa matibabu baada ya kuugua maradhi yaliyosababisha ngozi yake kuharibika na tangu arejee nchini juzi ndiyo ilikuwa mara yake ya kwanza kuonekana katika hadhara ya watu.

Wengine waliohudhuria uzinduzi huo ni Mbunge wa Same Mashariki, Anne Kilango Malecela, Mbunge wa Kahama, James Lembeli, Mbunge wa Viti Maalumu Mbeya, Hilda Ngoye, aliyekuwa Mbunge wa Vunjo, Aloyce Kimaro na Mjumbe wa Umoja wa Vijana (UVCCM), Mkoa wa Kilimanjaro , Paul Makonda. Mbali ya kuapa kuendeleza mapambano dhidi ya mafisadi, Dk Mwakyembe pia alisema:

“Nilifika hospitalini Oktoba 10 (mwaka jana), na tangu wakati huo sikuweza kuvaa viatu lakini leo hii naweza kuvaa viatu, kwa hiyo shetani ameshindwa.” Alisema atatumia siku za Jumapili kuzunguka katika makanisa mbalimbali kwa lengo kumkemea shetani

Vodacom tanzania yatangaza promosheni ya punguzo la gharama


Vodacom tanzania yatangaza promosheni ya punguzo la gharama
Wateja kupiga simu kwa robo shilingi. Kutuma SMS kwa 25/-

Kampuni ya mawasiliano ya Vodacom Tanzania imetangaza promosheni ya aina yake ya punguzo la gharama za simu kupiga na kutuma ujumbe mfupi wa maneno- SMS itakayowahusisha wateja wa kampuni hiyo ambao sasa watapiga simu kwa gharama ya ROBO SHILINGI kwa sekunde.

Promosheni hiyo ya siku saba kuanzia Jumatatu Januari 30, 2012 inahusu kupiga simu za ndani ya mtandao wa Vodacom yaani kupiga Vodacom kwenda Vodacom kati ya Saa nne usiku na saa moja asubuhi kila siku kwa wateja wote wa malipo ya kabla. Aidha sanjari na ofa hiyo kamambe Vodacom imetoa pia punguzo la gharama ya kutuma ujumbe mfupi wa maneno hadi shilingi 25/- kwa ujumbe wakati wote wa siku kwenda mtandao wowote wa simu ya mkononi nchini kwa kipindi cha siku saba nayo pia kuanzia leo Jumatau Januari 30, 2012.

Akitangaza promosheni hizo mbili Mkurugenzi Mtendaji wa Vodacom Bw. Rene Meza amesema ni imani yake kwamba katika kipindi chote cha siku saba cha promosheni hiyo wateja watafurahia kwa kufanikishiwa mawasiliano ya biashara, familia, kazi na mengineyo kwa gharama nafuu zaidi. “Wateja wa Vodacom wakati wote wanafurahia huduma bora, nzuri na zenye kukidhi mahitaji halisi, ni wazi kipindi hiki cha siku saba cha promosheni hii ya punguzo la gharama za upigaji wa simu na utumaji SMS kitawapatia wakati mwengine bora wa kufurahia kuwa wateja wa kampuni inayoongoza soko”Alisema Bw. Rene.
Promosoheni hii inakwenda sawa na azma ya Vodacom ya kutoa fursa ya watanzania kuunganishwa kimawasiliano na kubadili maisha.

Ili mteja wa Vodacom aweze kufurahia promoheni hii ya punguzo la gharama za mawasiliano anapaswa kwanza kujiunga kwa kupiga *100# na kuanzia hapo atakuwa na uwezo wa kufurahia mawasiliano nafuu zaidi nchini miongoni mwa mitandao ya simu za mkononi.

“Ni fursa nzuri kwa wateja wetu, tunawaomba waitumie ikiwa ya kiwango cha chini zaidi kuwahi kutokea katika soko la mawasiliano ya simu za mkononi nchini na Vodacom itaendeleza utamaduni wa kuwa kinara wa kubuni na kuleta sokoni promosheni pamoja na huduma zenye thamani na mantiki halisi ya wateja wetu na jamii nzima nchini.” Aliongeza Bw. Rene

Rene aliongeza kwa kusema “Tunapoangalia katika utaratibu wetu wa kawaida wa mfumo wa maisha tanagundua kuwa muda wa kati ya saa nne usiku na saa moja asubuhi ndio wanafamilia hukaa pamoja na kufanya mawasiliano yenye lengo la kupashana habari za familia na hata kazi na biashara baada ya majukumu ya kutwa nzima au kabla ya kuanza siku mpya, hivyo ni imani yetu tumewapa wateja kitu chenye thamani na kinachoweza kutumika vema na kumnufaisha kila mteja.”Aliongeza

Vodacom ikiwa na wateja zadi ya milioni kumi nchini ni wazi promosheni ya aina hii itatoa faida kubwa kwa jamii kwa kuwawezesha kutumia sehemu ya punguzo la gharama ambazo wangengia kupiga na kutuma ujumbe mfupi wa maneno kuelekeza sasa fungu hilo katika matumizi ya mahitaji mengine .

Ndugulile Atembelea Hospitali Ya Taifa Ya Muhimbili na Kusema “Ni Dhahiri Kuwa Mgomo wa Madaktari na Sasa Manesi Upo,Ni Dhahiri KuwaMGOMO WA MADAKTARI NCHINI:Mbunge Wa Kigamboni(CCM) Dk Faustine Mgomo Huu una Madhara kwa Wagonjwa Wasio na Hatia.”


Mbunge wa Kigamboni(CCM)Dk Faustine Ndugulile

UTANGULIZI
Leo mchana nimepata nafasi ya kutembelea hospitali ya Muhimbili hali niliyokuta ni tofauti na taarifa zinazotolewa kwenye vyombo vya habari.Kwa kifupi hali ni mbaya sana. Nilipofika maeneo ya mapokezi nilikutana na gari la Halmashauri ya Bagamoyo lililokuwa limezongwa na waandishi wa habari. Nilipoulizia nikaambiwa kuwa mgonjwa aliyekuwa mahututi katika gari hilo hakupokelewa na hospitali hiyo na hivyo kuamuriwa kurejeshwa Bagamoyo. Nilichukua hatua za haraka za kuwasiliana na uongozi wa idara ya dharura (Emergency Department). Namshukuru Prof.Victor Mwafongo kwa kuwasili katika eneo husika na kuchukua maamuzi ya kumpokea mgonjwa yule.

Nilipata nafasi ya kutembelea maeneo mbalimbali ya hospitali. Baadhi ya wodi hazikuwa na madaktari wala manesi. Nilitaarifiwa kuwa manesi nao walikuwa kwenye vikao vyao vya majadiliano. Wagonjwa walikuwa wanahudumiwa na wahudumu wa afya ambao kitaaluma hawapaswi kuhusika na matibabu ya mgonjwa.

Kliniki za wagonjwa wa nje vilikuwa hazina watu kabisa kinyume na hali ya kawaida. Madaktari waandamizi walinitaarifu kuwa operesheni zote zisizo za dharura (elective operations) zimesimama isipokuwa operesheni chache za dharura.

Ni dhahiri kuwa mgomo wa madaktari na sasa manesi upo. Ni dhahiri kuwa mgomo huu una madhara kwa wagonjwa wasio na hatia. Tusichokijua ni idadi ya wagonjwa waliopoteza maisha na kukosa tiba muhimu katika kipindi cha mgomo.

KIINI CHA MGOGORO
Mgogoro huu unatokana na kucheleweshwa kulipwa kwa posho za kila mwezi za madaktari walio kwenye mazoezi ya vitendo (Interns). Suala hili lilipelekea madaktari kugoma. Pamoja na kulipwa fedha walizokuwa wanadai madaktari hao, Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii haikutumia busara kuwahamisha madaktari waliokuwa wanadai haki zao. Vilevile kauli za kejeli na ubabe za viongozi wa Wizara zilizidi kuwachochea madaktari hawa, hali iliyopelekea kubadili sura ya mgomo kutoka ule wa interns hadi kuwa mgomo wa nchi nzima wenye madai lukuki kuhusu hali ya huduma za afya, maslahi na madeni ya madaktari n.k. Cha kutisha zaidi ni kwamba kada yingine kama manesi, mafundi sanifu maabara, mionzi na wafamasia nao wameanza kugoma pia.
Vilevile Wizara haikujipanga vizuri na wala kushirikisha wadau wengine muhimu katika kutafuta suluhu ya sakata hili.

NINI KIFANYIKE

Hekima na busara zitumike katika kushughulikia suala hili. Nguvu na vitisho vitazidi kuchochea mgomo huu.

Serikali ichukue hatua za haraka za kukutana na madaktari walio kwenye mgomo na kuwasikiliza madai yao. Iundwe timu ya Serikali na madaktari kupitia madai yote , kuyachuja na kuyapa vipaumbele. Madai yatakayokubalika na pande zote mbili yawe na muda maalum wa utekelezaji (Timeframe).

Niwaombe madaktari wenzangu waweke utaratibu wa kutoa huduma za dharura kwa wananchi wakati huu ambao wako kwenye majadiliano na Serikali ili kupunguza usumbufu usio wa lazima kwa wananchi. Hatua hii itawajengea heshima kwenye jamii.
Serikali iangalie upya maslahi ya watumishi wa umma ikiwa ni pamoja wale walio kwenye sekta nyeti. Hili liendane sambamba na kuboresha mazingira ya kazi na upatikanaji wa vitendea kazi.

Serikali ichunguze kiini cha mgogoro huu na kuchukua hatua za nidhamu kwa watendaji waliosababisha sakata hili.