Dk. Slaa Aichambua CCM

 
 
 
 
 
ADAI WATEULE WAPYA WANA TASWIRA YA UFISADI
 
 
KATIBU Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Willibrod Slaa, ameichambua safu mpya ya uongozi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) iliyoundwa hivi karibuni mjini Dodoma, akisema wana taswira ya ufisadi.
 
Amesema kuwa hali hiyo inatokana na baadhi yao kuhusika kwenye matukio kadhaa ya kifisadi moja kwa moja.
 
 
Akizungumza na Tanzania Daima jana kuhusu mtazamo wake kwa safu hiyo mpya ya uongozi wa CCM iliyoundwa na Mwenyekiti wake, Rais Jakaya Kikwete, katika mkutano mkuu uliomalizika juzi, Dk. Slaa alisema haoni jambo jipya.
 
“Nadhani hakuna jambo jipya, kipya ni kwamba wameteuliwa jana, lakini wote ni wazoefu wachafu,” alisema.
 
 
Katika safu hiyo, Kikwete anasaidiwa na makamu wawili, Philip Mangula wa bara na Dk. Ali Mohamed Shein wa visiwani na pia alimteua kada mkongwe, Abdullahman Kinana kuwa Katibu Mkuu mpya wa CCM.
 
 
Wengine wanaounda Sekretarieti ni Zakhia Meghji, Mwigulu Nchemba, Asha-rose Migiro, Vuai Ali Vuai, Nape Nnauye na Mohamed Seif Khatib.
 
Akimchambua mmoja baada ya mwingine, Dk. Slaa alimtuhumu Mangula kuwa ni mmoja wa watu waliohusika na ufisadi wa fedha za Akaunti ya Malipo ya Nje (EPA) katika Benki Kuu ya Tanzania.
 
 
“Makamu Mwenyekiti Mangula anahusika na EPA, vimemo vingi vya kutaka fedha za EPA vimetokea kwake…sioni leo atajisafishaje kuleta tumaini jipya kwa Watanzania,” alisema.
 
Kuhusu Meghji, Dk. Slaa alisema huyo ndiye aliyeandika barua na kudanganya kuwa fedha hizo za EPA zimetoka kwa ajili ya Usalama wa Taifa.
 
 
“Sasa mtu kama huyo aliyedanganya, leo hii ukamweka kwenye fedha maana yake ni ku-‘recycle material’ ile ile,” alisema Dk. Slaa.
 
 
Akimchambua Katibu Mkuu, Kinana, alisema kigogo huyo ana mkono katika biashara chafu za makampuni ya meli na kwamba hajakanusha mpaka sasa.
 
 
Dk. Slaa alisema Kinana ambaye alikuwa meneja kampeni wa mgombea urais wa CCM mwaka 2010, katika chaguzi hizo CCM imeshutumiwa kwa kuiba kura, hivyo uteuzi wake ni kukubali kuzika demokrasia nchini.
 
 
Alisema timu hiyo imeundwa mahsusi kwa ajili ya kujiandaa kuiba kura mwaka 2015.
 
Dk. Slaa aliongeza kuwa baada ya uchaguzi, CCM walitumia fedha nyingi kwa ajili ya kwenda kufanya utafiti wa kukijenga upya chama chao, ambao uliozaa kauli mbiu ya ‘Kujivua Gamba’, kwamba pamoja na kazi ya kitaalamu wameshindwa kuvuana magamba.
 
Alifafanua kuwa hatua hiyo inatokana na ukweli kwamba walioitwa magamba sasa wamo kwenye safu mpya ya uongozi wa CCM.
 
 
Katika kile kinachoonekana kuwa ni kumjibu Rais Kikwete hasa kutokana na kauli yake kuwa wapinzani wanafanya kazi ya kueneza uongo na kuwataka makada wa CCM kujibu mapigo, Dk. Slaa alimtaka aache kuwadanganya Watanzania.
 
Dk. Slaa alisema kuwa Rais Kikwete huenda hasomi, anadanganywa au anapenda lugha rahisi za kusema wenzake waongo.
 
 
“Mawaziri wameutumia Mkutano Mkuu kwa mbwembwe kueleza uongo…katika ripoti ya Juni 2012, hali ya uchumi wa taifa, iliyoandikwa na Ofisi ya Rais, Ofisi ya Mipango, na kelele zote zilizopigwa kuhusu maendeleo yaliyopatikana kwenye barabara.
 
 
“Kwenye ripoti hiyo imeandikwa kuwa mwaka 2011 barabara zilizokuwa katika hali nzuri ni kilomita 5,976 sawa na asilimia 30.4 ya barabara zote za mikoa,” alisema.
 
 
Ukilinganisha na mwaka 2010, barabara zilizokuwa na hali nzuri ni kilomita 11,012, maana yake ni kuwa nusu ya barabara zilizokuwa nzuri mwaka 2010 leo mwaka mmoja baadaye ni mbaya.
 
 
Aliongeza kuwa wakizitumia takwimu hizo ambazo zimeandikwa na Ofisi ya Rais, bado wanaambiwa ni waongo.
 
 
Alisema itakumbukwa kwenye viwanja vya Mwembe Yanga wakati alipotoa orodha ya mafisadi, Rais Kikwete alimjibu kuwa kelele za mlango hazimzuii mwenye nyumba kulala lakini leo amekiri ufisadi upo CCM.
 
 
Mwanasiasa huyo machachari, alisema kuwa Rais Kikwete amesikika mara kadhaa akilalamika kuhusu ufisadi ndani ya chama chake na kuhoji kati yake yeye na Kikwete nani muongo?
 
 
“Aidha Rais sio makini; anapenda maneno rahisi…tunamwambia aweke hadharani takwimu asilete propaganda,” alisema.
 
 
Slaa alikumbusha pia jinsi ambavyo Rais Kikwete na CCM walivyowaita ni waongo wakati CHADEMA walipokuja na sera ya matumaini kwa Watanzania mwaka 2010, wakisema nyumba za tembe na nyasi sasa basi na kueleza mikakati yao ya kushusha bei ya saruji na vifaa vya ujenzi.
 
 
Katika hilo Dk. Slaa alisema kuwa alifurahi juzi kusikia CCM katika maazimio ya Mkutano Mkuu wao wakisema kuwa watashusha bei ya saruji na vifaa vya ujenzi.
 
“Sasa CCM na CHADEMA nani waongo? Mimi nasema hakuna kitu kinachotushangaza katika uongozi wa sasa, timu ni ile ile ya mafisadi,” alisema
Aliwataka Watanzania kuwa makini akidai kuwa waliowekwa kwenye safu ya uongozi CCM ni mafundi wa ufisadi na kutoa wito kuwa wajiandae kulinda kura.
 
 
Naye Katibu Mkuu wa NCCR-Mageuzi Samuel Ruhuza, alisema wao kama chama wanawapongeza CCM lakini kwa jicho la siasa hawaoni kipya na kwamba viongozi wapya ni wachovu wale wale.
 
 
“Hawana jambo jipya kwa sababu CCM imechoka sana haina watu wapya ni walewale, sasa hivi tulitegemea vijana wapya lakini hilo halijatokea,” alisema Ruhuza.
 
 
JK awasuta wabaya CCM
 
Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Taifa (CCM), Rais Jakaya Kikwete, amewashambulia wanachama wa chama hicho waliokuwa na ndoto za kuona mkutano mkuu wao ukimalizika kwa mpasuko, akisema kuwa wameshindwa.
 
 
Rais Kikwete alitoa kauli hiyo jana ikiwa ni siku moja baada ya kuiteua sekretarieti ya chama hicho, itakayoongozwa na Katibu Mkuu, Abdullahman Kinana.
 
 
Akiwatambulisha rasmi wateule hao, Rais Kikwete alisema anawashangaa baadhi ya wanachama ambao wanaifahamu vizuri CCM lakini walikuwa wakiombea mabaya ili mkutano umalizike vibaya waweze kujivunia kile walichokikusudia.
 
 
“Namshukuru sana Mungu tumemaliza salama; kuna watu walikuwa wakitambika usiku na mchana CCM imalize vibaya mkutano wake na walitamani itoke na vipande lakini wameshindwa na sijui watamdai nani gharama zao?” alihoji.
 
 
Alisema watu hao wamepoteza muda wao bure na CCM imara imeweza kumaliza mkutano wake vizuri na kupanga safu ya ushindi katika uchaguzi wa serikali za mitaa pamoja na kuingia Ikulu mwaka 2015.
 
 
“Nimesikia mambo mengi na kuna watu kabisa walikuwa wakinijia wakiniambia kuwa kuna jambo hili na hilo, lakini nilikuwa nawaambia kuwa watulie kwani kuna watu wana ndoto za mchana wanatumia nguvu nyingi, wanatumia muda wao bure na wanapoteza wakati wao,” alisema.
 
 
Rais Kikwete alitamba kuyatekeleza maazimio yote waliyoazimia moja baada ya lingine ili kuhakikisha wanayatimiza kwa wakati na kwa muda mfupi ili Watanzania kuendelea kujenga imani na chama hicho.
 
 
Alisema wajumbe wa NEC wanatakiwa kutumia muda wao mwingi kuifanya kazi ya chama ili kuweza kukijenga chama hicho kwa kiwango kikubwa.
 
 
 
                                           Chanzo: Tanzania Daima

 

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s