Je, Ushirikina Unafanikisha Biashara….?(1)

 
 
 
 
Na: Albert SangaIringa
 
Mapema mwaka huu nilikuwa mmoja ya maelfu ya wakazi wa mjini Iringa tuliokwenda mtaa wa Frelimo kushuhudia sakata la misukule; iliyodaiwa kuwemo katika nyumba ya mama mmoja mfanyabiashara maarufu mjini hapa. Licha ya kufika mapema sana eneo hilo lakini sikubahatika kuona misukule.
 
Wengi wetu, hata wale waliorusha mawe na kumpiga sana mama yule, hakuna aliyeiona misukule kwa macho zaidi ya kusikia tu! Sakata lenyewe lilivyoanza hadi kufika hapo ni habari ndefu na sitaiandika hapa kwa sababu wengi wenu mlisoma katika magazeti na mitandao mbalimbali. Kutokana na tukio lile nimeona ipo sababu tujadili hii “issue” ya ushirikina katika biashara.
 
Kwa miaka mingi nchini Tanzania (na duniani) kumekuwepo na imani, hisia, visa na matukio yanayohusisha ushirikina na mafanikio ya mtu kibiashara. Katika uzoefu wangu wa kusoma na kusikiliza sijakutana na utafiti ama maandishi yeyote  rasmi yanayodhihirisha kiusawa (fair verification) nafasi ya ushirikina katika mafanikio ya mtu kibiashara. Katika makala hii sitachambua kabisa habari za “Freemason” badala yake nitajikita kwenye ushirikina wa kijadi unaoaminika kuwepo Tanzania kwetu tangu zamani.
 
Wataalamu wa masuala ya biashara, taasisi za maendeleo, wanadini na watu wa kada ya kawaida mara zote wasimamapo katika hadhara husisitiza watu kutoamini mchango wa ushirikina katika mafanikio ya mtu katika biashara; lakini ni nini watu mbalimbali wanakiamini katika mioyo yao kuhusu jambo hili?
 
Ukweli ni kwamba watu wengi wanaamini uwepo wa imani hizi za kishirikina katika biashara mbalimbali. Ni wachache wanaokiri peupe ikiwa wanatumia ushirikina lakini siku kwa siku idadi ya wanaofika kwa waganga wa kienyeji kutaka ndumba za kuwatajirisha inaongezeka. Na tena upo uhalisia fulani (ambao haujathibitishwa kiutafiti) ya kuwa ndumba hizi huwafanikisha watu.
 
Ni mara nyingi sana tunasikia matangazo na habari za wataalamu wa jadi ambao wanajinadi kuwa wanao uwezo wa kuwafanikisha watu kibiashara. Vipo visa vya watu kutoa kafara za damu za binadamu kwa kuua watu (hasa ndugu zao) na kupewa dawa. Hivi karibuni kumevuma habari za uwepo wa waganga wa jadi nchi za jirani(Zambia, Malawi na DRC) ambao wanatoa “utajiri” kwa staili ya aina yake.
 
Inasemekana kuwa, huko kuna kuku wa uganga ambapo “mteja” huchota punje za mahindi na kuzirusha chini; kisha kuku wa uganga huanza kuyadonoa. Idadi ya punje atakazodonoa ndio miaka utakuwa hai ukiwa na utajiri wa kupindukia. Cha ajabu ni kuwa kuku huyo hawezi kuzidisha punje kumi. Kwa hiyo anaweza kudonoa punje moja, mbili ama kumi zote kutegemea na bahati ya muhusika. Mamia ya watanzania wanamiminika huko kila kukicha!
 
 
 
Katikati ya mwaka 2005 nilikuwa katika ibada ya kawaida kanisani kwetu, katika siku hiyo kulikuwepo na mtu aliyeamua kumgeukia Mungu na kuachana na utumwa wa dunia hii. Kwa bahati nzuri ninamfahamu mtu yule, alikuwa ni mmoja ya matajiri wakubwa na maarufu katika eneo letu.
 
 
 
Kuokoka kwake kuliambatana na uchomaji wa ndumba. Katika ushuhuda wake, alieleza kuwa kwa miaka karibu 16 amekuwa akifanya biashara kwa kutumia ushirikina. Alidai kuwa, mganga alimpa masharti ya kutoa kafara ya binadamu kila baada ya miaka miwili na kulala makaburini kila siku ya ijumaa na jumapili. Hadi kufika wakati huo alikuwa ameshawaua ndugu zake 8 kwa ushirikina wakiwemo baba, mama na mwanae wa kwanza!
 
Mtu huyu alitueleza alikuwa na chumba maalumu ambako alikuwa akitunza misukule ya wanaokufa kiuchawi na kila asubuhi alikuwa akifungua chumba kile na kukuta kimejaa mamilioni ya fedha za noti! Zilikuwa zikitoka wapi fedha hizo? Hata yeye hakuwa akijua, lakini mtindo huu wa mtu kuletewa fedha kishirikina ni maarufu sana, ukiitwa “chuma ulete”
 
 
 
Haitakuwa busara kwa wataalamu na wadau wa biashara kukaa kimya, ama kutoa majibu mepesi kwa maswali magumu. Lazima tutafiti na kujiridhisha kuhusu suala hili. Je, kwa ukweli kiasi gani kuwa ushirikina unaweza kumfanikisha mtu kibiashara? Kama ushirikina hauna nafasi katika biashara mbona kuna watu wanaoutumia na wanakiri kuwa wanafanikiwa?
 
Wakati fulani nilikutana na mganga mmoja wa kienyeji wilayani Njombe na nikabahatika kuongea nae mambo kadha wa kadha kuhusu, ndumba katika biashara. Mganga huyu alikiri kuwa zipo dawa na utundu wa kijadi ambao humuwezesha mtu kufanikiwa kibiashara. Ingawa mganga huyu alisema kuwa wanatumia zaidi kanuni za kisaikolojia kuliko, “dawa”. (Itaendelea)
 
 
 
Wajasiriamali tunastahili ushindi
stepwiseexpert@gmail.com.Chanzo:mjengwablog
Advertisements

One Comment

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s