Lema Kufuru

 
•  Apokewa kifalme, amkamia Pinda bungeni

na Grace Macha, Arusha
 
MAPOKEZI ya Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema (CHADEMA) yametingisha Jiji la Arusha.
Umati mkubwa wa watu ulijitokeza kwenye mapokezi ya mbunge huyo jana kuanzia njia panda ya kutokea Uwanja Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) ambapo msururu mrefu wa magari, bodaboda na baiskeli ulipamba mapokezi hayo.
Lema aliyekuwa akitokea jijini Dar es Salaam ambapo Mahakama ya Rufaa ilimrejeshea ubunge wake juzi, alikuwa kwenye gari la wazi huku akipungia wananchi.
Kwenye baadhi ya miji ya Wilaya ya Arumeru, alilazimishwa kusimama kutokana na wananchi kumzuia wakitaka awasalimu.
Hali hiyo ilisababisha safari kutoka KIA hadi jijini Arusha ambapo kwa kawaida hutumia saa moja, kuchukua zaidi ya saa sita, kuanzia saa tatu asubuhi mpaka saa tisa alasiri kufika jijini Arusha.
Baada ya kufika Arusha, msafara huo ulipita kwenye barabara mbalimbali za jiji hilo, ikiwemo ile ya Afrika ya Mashariki, Goliondoi, Sokoine kisha kuingia kwenye Uwanja wa Kilombero walikofanyia mkutano, ambapo kote walipokuwa wakipita wananchi walikuwa wamejaa barabarani wakimpungia huku wengine wakiwa wamebeba majani kuashiria amani.
Hata hivyo, wananchi wengine waliamua kufuata msafara huo kwa miguu na magari hali iliyofanya baadhi ya shughuli kusimama kwa muda kwenye maeneo ambayo ulipita, huku barabara zikiwa hazipitiki mpaka msafara huo ulipopita.
Aidha, wananchi mbalimbali walitoa maoni yao wakionesha kuridhishwa na uamuzi wa Mahakama ya Rufaa wa kumrejeshea Lema ubunge ambao alivuliwa na Mahakama Kuu kwa madai kuwa, haki inaweza kucheleshwa, lakini haipotei, hivyo wakautaka mhimili wa mahakama kujizatiti kuhakikisha unatenda haki ili uendelee kuheshimiwa.
Katibu Mwenenzi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Kata ya Nduruma, Iddi Ramadhani maarufu kama Iddi Nduruma akizungumza kwenye eneo la mkutano, alisema kuwa anaamini Mahakama ya Rufaa haitendi kosa kwani ina majaji makini, hivyo hana kinyongo na uamuzi huo, na kuongeza kuwa shauri hilo limemkuza zaidi Lema kisiasa kwani hajawahi kushuhudia mapokezi makubwa kama yake.
“Imefika wakati vyama vya siasa viache chuki binafsi ambazo zinaleta hasara kwa taifa, huku wakiwanyima wananchi kuhudumiwa na wawakilishi wao kama ilivyokuwa katika shauri hili ambalo limesababisha wananchi wa Arusha wakose uwakilishi kwa zaidi ya miezi nane, huku miaka miwili akiimalizia mahakamani kwenye kesi,” alisema mmoja wa watu waliofika katika mapokezi hayo.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Taifa wa Baraza la Vijana wa CHADEMA (BAVICHA), John Heche akizungumza kwenye mkutano huo alisema kuwa Mwenyekiti wa Taifa wa chama hicho, Freeman Mbowe amekwenda Nairobi nchini Kenya kwenye kampeni za chama cha ODM, kinachoongozwa na Raila Odinga, ambacho ni chama rafiki, vinginevyo naye angejumuika kwenye mkutano huo.
Aidha, aliwatahadharisha vijana aliodai kuwa hawana nidhamu ndani ya baraza hilo ambao wanatumiwa na watu ndani ya CHADEMA na CCM wakipewa fedha kwa lengo la kukivuruga.
Alisema hakutakuwa na msamaha kwa wote watakaobainika kwani watachukuliwa hatua kali kwa mujibu wa taratibu na kanuni walizojiwekea.
“Bora tubaki wachache ndani ya BAVICHA kulikoni kuendelea kukaa na watu wengi ambao ni mamluki, hatutakubali hawa wahuni wachache ambao kwa tamaa zao za kutaka utajiri wa haraka haraka watuvuruge pamoja na chama chetu, tutawashughulikia kwenye vikao vyetu,” alisema Heche.
Alisema CHADEMA inapigania kuhakikisha rasilimali zilizopo nchini ikiwemo nishati ya gesi, maji, ardhi, madini na nyingine nyingi zinawanufaisha Watanzania wote, hivyo hawako tayari kuwavumilia mamluki wachache wanaotumiwa kwa kupewa fedha ili kukwamisha jitihada hizo, ni lazima wawachukulie hatua.
“Rais Jakaya Kikwete alikuja Arusha akasema kuwa kuna amani, amani ipi? Amani siyo ujinga wala kuvumilia njaa, bali ni kuwa na maisha bora, uhakika wa huduma za afya. Hapa nchini hakuna amani bali kuna utulivu kwani watu wana shida nyingi zinazowakosesha amani, hata wakienda polisi wanaishia kubambikiziwa kesi,” alisema.
Akizungumza katika mkutano huo, Lema alitoboa siri kuwa kilichosababisha arudishiwe ubunge ni baada ya kubaini kuwa hata wakimvua na uchaguzi ukirudiwa, ataibuka mshindi tena na walifanya majaribio kwa uchaguzi mdogo wa udiwani wa Kata ya Daraja Mbili ambapo CHADEMA iliibuka mshindi.
Alisema kuwa hatakuwa tayari kuona machinga wakiendelea kunyanyasika ndani ya Jimbo la Arusha ambapo alidai kuwa wanahitaji kuheshimiwa kwa kuhakikisha wanatafutiwa maeneo kabla ya kuondolewa kwenye maeneo waliyopo kwa kile alichodai kuwa kuwaondoa bila kuwapa maeneo si sawa kwani hawawezi kwenda porini.
Lema alisema sasa anarudi bungeni, hivyo hoja yake aliyoiwasilisha akidai kuwa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda alilidanganya Bunge kuhusiana na mgogoro wa uchaguzi wa Meya wa Arusha, ataifufua upya.
Aidha, mkutano huo ulihudhuriwa na madiwani wa CHADEMA kutoka halmashauri za Jiji la Arusha, Hai, Moshi, Karatu, pamoja Mbunge wa Karatu, Israel Natse, Mbunge wa viti maalum Mkoa wa Arusha, Cecilia Paresso na Katibu wa CHADEMA Kanda maalum ya Kinondoni, Henry Kilewo.
http://www.freemedia.co.tz/daima/habari.php?id=43840
Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s