Wanasiasa hawa hawana shukurani vinywani mwao – Rais Kikwete.

 

 

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete.

 

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amewashangaa baadhi ya wanasiasa ambao amewaeleza kuwa hawana shukurani vinywani mwao na wala hawana macho ya kuona mafanikio ya dhahiri ya Serikali katika sekta mbali mbali ikiwemo ile ya barabara na ujenzi wake nchini.

 

Zaidi, Rais Kikwete amewashangaa baadhi ya wanasiasa wa Mikoa ya Kusini ambao wamekuwa wanalalamikia kutokumalizia kwa kipande kifupi cha barabara la Somanga-Nyamwage kuwa ni kushindwa kutimizwa kwa ahadi za Rais Kikwete.

 

Akizungumza juzi, Jumamosi, Aprili 13, 2013 katika Kijiji cha Kasera, Wilaya ya Mkinga, Mkoa wa Tanga wakati wa uzinduzi wa Barabara ya lami ya Tanga-Horohoro yenye kilomita 65.14, Rais Kikwete alisema:

 

“Hakuna mtu yoyote ambaye haoni kuwa barabara hii ni ukombozi mkubwa wa wananchi ambao huko nyuma hawakuwa na barabara ya lami, isipokuwa wale wenye macho lakini wanajifanya hawaoni. Hawa ni watu wenye hiana mioyoni mwao na hata Serikali ifanye nini wataendelea kuimba santuri yao ambayo sasa imewachosha watu.”

 

Aliongeza Rais Kikwete: “Wapo watu wanaoendelea kudai kuwa hakuna kilichofanyika. Hawa ni sawa na wale watu wawili ambao walikuwa wanapoteza muda wake kubishana mchana kweupe kuhusu kile walichokuwa wanakiona juu yao kama ni Jua ama Mwezi. Ni wapuuzi tu.”

 

Kuhusu malalamiko ya baadhi ya wabunge wa Mikoa ya Kusini juu ya Barabara ya Lindi-Kibiti na hasa sehemu ya Nyamwage-Somanga, Rais Kikwete alisema:

 

“Hawa ni watu ambao hawana hata shukurani vinywani mwao. Hapa ni mahali hapakuwa na barabara kabisa wala Daraja lile la Mkapa. Wakati Mzee Mkapa alipojenga Daraja la Mkapa wakamkejeli kuwa alichokuwa amefanya ni sawa na kumnunulia shati mzazi wake aliye uchi. Atatoka vipi nje na shati tupu?”

 

“Tulichofanya sisi ni kujenga barabara yote hii ya lami kutoka Lindi hadi Kibiti. Hii ilikuwa ni barabara iliyokuwa haipitiki wakati wa majira fulani fulani. Tumemaliza kuijenga yote isipokuwa kilomita 9.5 ambazo nazo wanamalizia. Sasa watu hawa, wanasiasa hawa wanataka tuwafanyie nini? Barabara haikuwepo kabisa na zimebakia kilomita 9.5 tu na bado wanalalamika na kusema Serikali gani hii? Wanataka tufanye nini?”

 

Wiki iliyopita Bungeni Dodoma Mbunge mmoja wa Viti Maalum wa Chama cha CUF alidai kuwa ahadi ya Mheshimiwa Rais Kikwete kujenga Barabara ya lami ya Lindi-Kibiti ilikuwa haitekelezwi kwa sababu ya kutokamilika kwa sehemu ya Somanga-Nyamwege. Mbunge huyo aliungwa mkono na wabunge kadhaa kutoka Mikoa ya Kusini.

 

Rais Kikwete pia amekumbushia kuwa katika miaka saba tu, Serikali yake imekomesha aibu ya watu wanaokwenda  sehemu moja ya nchi kulazimika kupitia nchi jirani ili wafike.

 

“Tumesahau kuwa miaka michache tu iliyopita watu wa kwenda Mwanza na Musoma walikuwa wanapitia Nairobi na Kisumu katika Kenya? Watu wa kwenda Bukoba walikuwa wanapitia Nairobi, Kampala, Masaka ndiyo wafike Mutukula kuingia Tanzania? Tumesahau haya katika muda mfupi tu wa miaka saba?”

 

Barabara ya Tanga-Horohoro ni moja ya miradi mingi ya miundombinu ambayo inajengwa chini ya ufadhili wa Mpango wa Millenium Challenge Account (Tanzania) wa Shirika la Millenium Challenge Corporation (MCC) wa Marekani.

 

Ujenzi wa barabara hiyo umegharimu Sh. Bilioni 75.715 ambazo zilikuwa ni pamoja na fidia kwa nyumba na mali nyingine za wananchi pamoja na ujenzi wa misikiti mipya kuchukua nafasi ya misikiti iliyovunjwa kupisha barabara.

 

 

 

Imetolewa na:

 

Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,

 

Ikulu.

 

Dar es Salaam.

 

15 Aprili, 2013

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s