KWA NINI KORTI YA KIMATAIFA (ICC) IMECHEMSHA KWENYE UCHAGUZI WA KENYA?

Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta (kulia) akiwa na Makamu wake, William Ruto (kushoto).

BY MOHAMED MATOPE

WAKENYA wengi walikuwa hawaijui International Criminal Court ( ICC), Korti ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai mpaka wakati Rais Uhuru Kenyatta na Makamu wake, William Ruto, waliposhitakiwa. Vilevile Waafrika  wengi wanaelewa  kwamba  watu wanaoshitakiwa kwenye korti ya kimataifa ni viongozi wa nchi wanaotawala kwa mabavu na wauaji wa raia wowote wanaowapinga kisiasa kama, Charles Taylor wa Liberia au viongozi wa vita vya misituni vya kuipinga serikali tawala (Warlords)  kama Joseph Kony wa Uganda.

ICC ni korti ya kimataifa iliyoundwa mwaka 2003,  ina mamlaka ya kuwahukumu watuhumiwa wa makosa ya mauaji ya kimbari (genocide), vitendo vya uhalifu dhidi ya binadamu katika nchi zote ambazo ni wanachama wa korti hiyo.

Cha kustaajabisha ni kwamba, Rais Kenyatta anashutumiwa na ICC kwa kosa la jinai dhidi ya binadamu  kwa kushiriki kwake kwenye mauaji ya Wakenya baada ya uchaguzi wa rais wa Kenya wa mwaka 2007. Mashitaka ya Kenyatta kwenye korti ya kimataifa ni sawa na mashitaka yanayomkabiri Joseph Kony wa Lord’s Resistance Army (LRA) ya Uganda  na  Bosco Ntaganda Kamanda wa Patriotic Force for the Liberation of the Congo (FPLC).

Wakenya wengi wanaomjua Kenyatta, hawajawahi kumuona amevaa nguo za jeshi, au ameshika bunduki, au yuko msituni akiwa amezungukwa na vijana wadogo wenye bunduki aina ya AK47. Wakenya wanamjua Kenyatta kama mtoto wa Baba wa Taifa, Jomo Kenyatta, mfanyabiashara, mwanasiasa, Mkikuyu na mtu anayeipenda nchi yake.

Mauaji ya Kenya ya mwaka 2007-2008, yalitokea baada ya uchaguzi wa rais wa mwaka 2007, mauaji hayo yalisababiswa na vita kati vya makabila ya Wajaluo na Wakikuyu, na Wakikuyu dhidi ya Wakalenjin. Vita hivi vilianza baada ya  mgombea urais, Raila Odinga (Mjaluo) alipokataa kukubaliana na matokeo yaliyotangazwa na Tume ya Uchaguzi ya Kenya, ambayo ilimtangaza  Rais Mwai Kibaki (Mkikuyu) kuwa mshindi wa kura za urais. 

Ukweli wa mambo ni hivi:  Kenyatta na Ruto hawakuwa wagombea wa urais kwenye uchaguzi wa mwaka 2007.  Swali linakuja, kama Kenyatta na Ruto hawakugombea urais,  kwa nini wameshitakiwa  kama waanzilishi wa vurugu zilizofuata baada ya uchaguzi huo?

Vilevile watu wanajiuliza, kwa nini kesi ya Kenyatta na Ruto ilipelelezwa kwa kasi kubwa, na mashitaka yakaletwa  mbele ya jaji wa mahakama ya kimataifa miezi saba kabla ya uchaguzi mkuu? Kama ICC inaweza kuendesha kesi kwa kasi hivyo, mbona haijamshitaki mtu yeyote kwa kuhusiana na vita vya Iraq  na Afganistani, ambapo maelfu ya raia wameuawa  na vita vimekuwa vinaendelea zaidi ya miaka kumi sasa? 

Vilevile watu wanajiuliza hivi sasa imeshapita miaka miwili tangu vita vya Syria vianze na ICC bado inapeleleza tuhuma za vitendo vya jinai katika vita hivyo nchini humo, kwa nini inachukua muda mrefu kuwaleta watuhumiwa kizimbani? ICC ipo wapi kwenye vita vya Israel dhidi ya Palestina au kwenye migogoro ya Ulaya ya Mashariki?

Pamoja na hayo vilevile  watu wengi  wanaituhumu  korti hiyo kuwa ni  fimbo ambayo mataifa ya magharibi wanaitumia kuwachapa viongozi wa Afrika. Kwa mfano toka ICC ianzishwe, miaka kumi ililiyopita imeshatangaza  watuhumiwa 32, ambao wote ni Waafrika, kwa maana hiyo viongozi wa Afrika ndiyo watu pekee wanaoua watu kwa kiwango kikubwa hapa duniani?

Kwa ufupi kesi ya Kenyatta haina miguu ya kusimama yenyewe, kwani kesi ililetwa mahakamani kutokana na mashahidi ambao wanasema walimsikia Rais Kenyatta akiongea kuhusu kuwaajiri Mungiki (kikundi cha ugaidi cha Kenya) ili wawavamie kabila la Wakalenjin.
Kati ya mashahidi hao shahidi mmoja tu (shahidi namba tano) ndiye aliyetoa ushahidi kwamba alikuwepo wakati Rais Kenyatta alipowaajiri Mungiki. Na shahidi huyo ametolewa katika kesi hiyo kwa sababu za rushwa na uongo.

Kwa kifupi ICC  imechemsha kwenye uchaguzi wa Kenya, kwanza kwa kuleta mashitaka ya Rais Kenyatta na makamu wake, William Ruto, katika kipindi ambacho siasa ilikuwa imechachamaa  nchini Kenya katika kipindi cha uchaguzi mkuu.  Watu wote tunaelewa jambo lolote linalokuja wakati wa uchaguzi lazima liwe na siasa ndani yake.

Pili , Kwa  kawaida kabla kesi haijafunguliwa, mwendesha mashitaka anapeleleza kesi kuona uzito wake na kukagua sehemu mauaji yalipotokea kabla hajaipeleka kesi mahakamani.
Kwenye kesi ya Rais Kenyatta ilikuwa ni kinyume. Luis Gabriel Moreno Ocampo, mwendesha mashitaka wa ICC aliifungua kesi ya Rais Kenyatta na washitakiwa wengine kutokana na ripoti  zilizowasilishwa kwake.
ICC haikutuma waendesha mashitaka wake nchini Kenya kuchunguza mauaji, kuongea na mashahidi, kuongea na waathirika wa pande zote kabla haijaifungua kesi, na hilo lilikuwa kosa  kubwa sana kwa upande wa ICC.

Lakini kwa kuwa korti hiyo ilishindwa kufuata hivi vipengele viwili, imejikuta ikiingizwa kwenye uchaguzi kama chombo cha kampeni na kupigwa kama mpira wa miguu na matokeo yake imepoteza heshima yake yote ndani ya Bara la Afrika.

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s