JIDE, RUGE KUMEKUCHA

Na Joseph Shaluwa

SAKATA kati ya mwanamuziki nyota wa Bongo Fleva, Judith Wambura Mbibo a.k.a Lady Jaydee ‘Jide’ na Clouds Media Group juu ya kupigana vita kibiashara limechukua sura mpya baada ya mkurugenzi wa vipindi wa kampuni hiyo, Ruge Mutahaba kuvunja ukimya na kulitolea ufafanuzi.  

Judith Wambura Mbibo a.k.a Lady Jaydee ‘Jide’.

Ruge alilipuka juu ya ishu hiyo juzi asubuhi, Jumatatu Mei 6, 2013 katika Kipindi cha Power Breakfast kinachoendeshwa na watangazaji Gerald Hando, Babra Hassan na Paul James wa Clouds FM.

MSIKIE RUGE
Akimjibu Jide katika kipindi hicho, Ruge alisema, hoja za Jide hazina mashiko na kwamba ishu yake ni ya kibinafsi zaidi inayoweza kumalizwa kwa mazungumzo na si kuendesha malumbano kwenye mitandao ya kijamii kama alivyofanya.
“Mimi niseme tu kwamba, Clouds ni private insitution (kampuni binafsi) , ina policy (taratibu) zake zinazofuatwa na kuheshimiwa. Zikivunjwa kuna sheria ndogondogo tulizojiwekea ambazo tunazifuata.

Ruge Mutahaba.

“Jide alilalamika wimbo wake mpya wa Joto Hasira haupigwi kwenye redio yetu. Nikaamua kufuatilia, unajua kwa bahati nzuri, zama hizi za digital system (mfumo wa digitali) ni rahisi kufuatilia mambo na kujua. Siku hiyo nilipofuatilia, nikagundua kwamba tayari wimbo huo umeshapigwa mara 46. Nikashangaa!
“Baada ya hapo akaanza kuandika manenomaneno yake kwenye mitandao ya kijamii. Sisi kama binadamu tukachukia na hatukuona sababu ya kuendeleakupiga nyimbo zake wakati yeye anatusema vibaya, tukaamua kukatisha. Ni kawaida kabisa kwa sababu amevunja taratibu zetu,” alisema Ruge.

KUHUSU KUMBANIA MATANGAZO
Ruge alisema: “Jide aliwahi kunitumia meseji akisema; nimelipa shilingi 240,000 kwa ajili ya matangazo ya Nyumbani Lounge lakini hayapigwi halafu unawaruhusu watangazaji wako wanitukane. Mimi nikaamua kumpigia.
“Nikamwambia inawezekana kuna tatizo la kibinadamu limetokea, maana sisi tunafanya biashara ya matangazo, hatuwezi kukataa kazi yako. Ila pia nilimwambia, kwa sababu Gardner (G. Habash) huwa anakuja kwa ajili ya kufanya matangazo, kwa nini asipite hapo chini (ofisi ya matangazo) akakumbushia?”

Bendi ya Skylight ikiwa kazini.

KUHUSU SKYLIGHT BAND
Akizungumzia madai ya Jide kunyang’anywa wanamuziki wake na kupelekwa Skylight, Ruge alikanusha vikali akisema yeye binafsi wala Clouds si wamiliki isipokuwa ni ya Sebastian Ndege.
“…lakini wanamchukulia wasanii, yeye anatafuta wengine anawatengeneza, wananyanyuka na bendi inaendelea kuwepo. Ndiyo maana anaitwa Iron Lady, ni sawa kabisa. Jaydee anatakiwa kukubali ushindani wa kibiashara.”

ATUPA KOMBORA
Katika mahojiano hayo, Ruge alikwenda mbali zaidi akisema kwamba, Jide yupo katika vita ya ushindani wa muziki lakini kwa bahati mbaya ameelekeza nguvu zake sehemu isiyostahili.
“Jaydee yupo kwenye anguko la muziki na kusema kweli, anasumbuliwa na Skylight Band sasa yeye anapigana the wrong way (isivyo), namshauri aelekeze nguvu zake Skylight. Apambane na washindani wake ili aendelee kuwa juu. Akubaliane na changamoto za kibiashara. Apigane kimuziki aendelee kusimama,” alisema.

SI SUALA LA KITAIFA
Alisema haoni kama ni sahihi suala la Jide kukuzwa kwa kiwango hicho kuwa kama la kitaifa kwa sababu ni jambo binafsi la kibiashara ambalo linaweza kumalizwa kwa mazungumzo.
Alitoa mfano kwamba, mgahawa wake wa Nyumbani Lounge umempiga marufuku Sam Machozi kufika pale kwa sababu amekwenda kinyume na taratibu za mgahawa huo.
“Mbona hilo halikuwa la kitaifa? Kuna wakati fulani nyimbo za Ray C (Rehema Chalamila) zilipigwa marufuku EATV, ilibidi mimi niongozane na Ray C hadi kwa mzee Mengi (Reginald) kumuombea msamaha ndipo nyimbo zake zikaachiwa. Mbona hilo halikuwa la kitaifa? Haya ni mambo binafsi na yanaweza kumalizika bila kukuzwa,” alisema.

AKUBALI KUKUTANISHWA
Katika kuonesha kwamba yupo tayari kukutana au kukutanishwa na Jide na kuyamaliza, Ruge alimtaka msanii huyo kutumia njia iliyo sahihi kumaliza tatizo lililopo kati yake na wao (Clouds) au yeye binafsi.
Alisema: “Sisi hatupigi nyimbo zake kwa sababu ametukosea lakini kama anahisi sisi ndiyo wakosaji kama anavyosema, zipo njia za kufanya ili kutafuta utatuzi. Jide anajua cha kufanya. Sisi hatuna matatizo naye. Kama anataka kuendelea kufanya kazi na sisi hata kesho au keshokutwa anaweza kuja tukazungumza.
“Si lazima aje yeye, anaweza kutuma hata watu anaowaheshimu, tukakodi mahali pazuri tukakaa na kuzungumza. Haya malumbano hayasaidii muziki wetu. Jaydee aje na hoja kamili zilizoainishwa tuzungumze. Nasisitiza haya ni mambo binafsi na si ya kitaifa.”

ASITISHA BONGO FLEVA
Katika kuonesha kuwa kila taasisi huwa na miongozo yake, Ruge aliagiza mara baada ya kumalizika kwa mahojiano hayo, redio isipige kabisa nyimbo za Bongo Fleva kwa siku nzima kama mfano wa uamuzi wa mamlaka ya taasisi yao.
“Ni utaratibu tu, ndiyo maana kuna siku huwa tunaamua kupiga nyimbo za wanawake tu. Sasa leo nasema kuanzia muda huu, msipige Bongo Fleva hadi atakapotoka Dj Nelly alfajiri. Hili ni agizo,” alisisitiza.

JIDE BADO YUPO NGANGARI
Katika kuonesha kuwa maneno ya Ruge hayakumwingia Jide, muda mfupi baada ya kauli hiyo kuisha aliandika katika akaunti yake ya Facebook kwamba mpambano bado unaendelea na ameahidi ataeleza mengine mazito zaidi hapo baadaye.
Jide aliandika: “Kama mtakumbuka niliahidi kutoa awamu ya pili tar 15 au 17 Mei na ahadi ni deni… japo naona mbali ila nitafanya hivyo. Bado nina mengi sana ya kuzungumza kuhusu Ruge na wenzake… Ile ilikuwa ni trailer tu, movie ndiyo inaanza sasa…”

MEZANI KWA MHARIRI
Ni vyema Jide akafikiria vizuri suala hili; maadam upande mmoja upo tayari kukutana naye akubali kufanya hivyo ili kumaliza tofauti hizi na kuendelea na ujenzi wa taifa.chanzo:www.globalpublishers.info

 

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s