Waziri wa Mambo ya Ndani, Dkt Emmanuel Nchimbi akizungumza wakati wa kufunga mkutano wa siku mbili wa viongozi wa dini na wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Dar es Salaam, juzi usiku.
WAZIRI wa Mambo ya Ndani, Dkt. Emmanuel Nchimbi amepiga marufuku mikutano ya hadhara isiyokuwa na vibali maalumu vya vyombo vya dola.
Kauli hiyo imekuja siku moja baada ya viongozi wa dini, kutaka mikutano ya hadhara isifanyike bila kufuata taratibu za kisheria.
Waziri Nchimbi pia amewaagiza makamanda wa polisi kote nchini, kuwafuatilia kwa karibu watu watakaokiuka agizo hilo na kuwachukulia hatua za kisheria.
Dkt. Nchimbi alitoa agizo hilo juzi usiku jijini Dar es Salaam, alipokuwa akizungumza katika mkutano wa viongozi wa dini.
Alisema kamanda yeyote wa polisi atakayeshindwa kudhibiti tatizo hilo, atakuwa wa kwanza kuwajibika katika eneo lake la kazi.
Akizungumzia kusambaa kwa maneno ya uchochezi kupitia mitandao ya kijamii alisema: “Ninaomba wazazi tuwaonye watoto wetu na vijana wetu wanaotumia mitandao hiyo vibaya kwani kama itaendelea kuachwa itumike ovyo, itaharibu amani tuliyokuwa nayo kwa zaidi ya miaka 50,” alionya Nchimbi
Katika hatua nyingine, alibainisha kwamba kwa sasa Serikali na vyombo vya usalama vinafuatilia mawasiliano ya simu yanayofanyika hasa yanayolenga kueneza masuala ya udini.
Maazimio hayo ni kutokuruhusu amani kuchezewa, viongozi wa dini wajihadhari na matamko yanayoweza kuleta mfarakano miongoni mwa jamii na waheshimu imani za wengine. Chanzo: http://www.mwananchi.co.tz