Na Khatimu Naheka
SAKATA la usajili wa kiungo wa Simba, Amri Kiemba, limechukua sura mpya. Sasa kiungo huyo ameweka wazi kuwa anataka alipwe ada ya usajili ya Sh milioni 30 na mshahara wa dola 1,500 (Sh milioni 2.4) ili amwage wino Msimbazi.
Simba bado ipo kwenye mazungumzo na kiungo huyo aliyeifungia mabao saba msimu uliopita, yakiwa ni mengi zaidi kuliko wachezaji wote wa Simba msimu huo. Awali, Kiemba alikataa ofa ya Sh milioni 20. Anadai kiwango chake hakilingani na mkwanja anaopewa.
Akizungumza na Championi Jumatatu, meneja wa kiungo huyo, Ulimwengu Hamim, alisema kama Simba wakichelewa kutoa kiasi hicho, wataangalia ofa zinazotoka katika klabu nyingine. Yanga bado inaripotiwa kumwania.
Alisema Kiemba angependa kubaki Simba, lakini kamwe si kwa dau la Sh milioni 20 asaini mkataba wa miaka miwili.
“Kila mtu anajua uwezo wa Kiemba, huu siyo wakati wa kuanza kupuuza viwango vya wachezaji wetu wa ndani na kuanza kuwatukuza wale wa nje, Kiemba yupo juu kwa sasa na huu ndiyo wakati wake wa kuona faida ya kazi yake.
“Hatutaki mshahara wake uwekwe katika kiwango cha fedha za hapa kwetu, tunataka Kiemba alipwe kama nyota wengine wa nje ambao wanalipwa kwa dola,” alisema Hamim.
Hamim alisema zipo klabu nyingi ambazo zinamwania Kiemba na Yanga wanasubiri kuona nyota huyo anashindwa kumalizana na Simba ili wao wachangamkie saini ya nyota huyo ambaye kwa sasa yupo na Taifa Stars ziarani nchini Ethiopia na Morocco.Chanzo:www.globalpublishers.info