CHADEMA YAMNASA WAZIRI MULUGO KWA RUSHWA KATA MBALAMAZIWA WILAYA MUFINDI IRINGA.

 

 

 

 
 
 
Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Phillip Mulugo.


CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimemfikisha Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Phillip Mulugo, mbele ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kwa tuhuma za kutoa rushwa ya ahadi ya mifuko ya saruji na fedha taslimu 40,000 kwenye mkutano wa kampeni za uchaguzi.
Chama hicho pia kimemfungulia faili la tuhuma za ubakaji mgombea udiwani wa Chama cha Mapinduzi katika uchaguzi mdogo wa kata ya Mbalamaziwa, Zuberi Nyomolela, kwa kosa kuishi kinyumba na binti mwanafunzi.
Hayo yamesemwa jana katika kijiji cha Mbalamaziwa na mwanasheria wa CHADEMA Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Sinkara Lucas, kwenye mkut ano wa kampeni za uchaguzi mdogo wa udiwani kata ya Mbalamaziwa, uliohudhuriwa na mwenyekiti wa chama hicho taifa, Freeman Mbowe.
“Ndugu zangu wakati wa kampeni hasa za nyumba kwa nyumba tulikuwa tunakutana na maneno maneno hivi yanazungumzwa kuhusu mgombea wa CCM, maneno mazito sana, sasa kama kawaida ya CHADEMA kama mnavyojua huwa hatukurupuki, tunafanyia kwanza vitu utafiti kabla hatujatoka hadharani kutuhumu; tunakuwa na ushahidi wa kutosha.
“Wananchi wa Mbalamaziwa ninyi ni mashahidi; majuzi alipita hapa Phillip Mulugo akatoa rushwa ya ahadi ya mifuko 20 ya saruji na fedha taslimu 40,000 eti kwa vijana wakanunue mipira lakini wamchague Zuberi…amefanya yote hayo hadharani hapa jukwaani, kinyume cha sheria za uchaguzi na sheria za nchi. Sasa tunao ushahidi na tumeupeleka TAKUKURU na hivi sasa wanalifanyia kazi faili hilo. Wakati wowote atakamatwa.
“Atakamatwa na faili linashughulikiwa. Wananchi wenzangu hiyo ndiyo CCM inayolea rushwa na ufisadi na huyo Zuberi naye itakula kwake…hajapata udiwani anafanya hivyo sasa akipata itakuwaje…?” alisema Lucas.
Akihutubia mkutano huo wa kampeni kumnadi mgombea wa udiwani kwa tiketi ya CHADEMA, Ezekia Ambangile Mlyuka, Mwenyekiti wa Taifa, Mbowe alisema vitendo vyovyote vya makosa ya jinai havistahili kuvumiliwa hivyo chama chake hakitakubali kuona vinafanyika, ikiwemo rushwa kwenye uchaguzi.
Mkutano huo uliohudhuriwa pia na wabunge Peter Msigwa, David Silinde, Mbowe mbali ya kuwapa pole kwa kufiwa na diwani aliyekuwepo, aliwaambia wananchi kuwa wasirudie makosa kwa kuichagua CCM, akisema kuwa imekuwa sababu na chanzo cha umaskini wa Watanzania.
Akitolea mifano namna kata hiyo ilivyo nyuma katika maendeleo kwa kukosa huduma za msingi za kijamii kama kukosa kituo cha afya, na zahanati kwa zaidi ya miaka 50 ya uhuru. Mbowe alisema ni wakati mwafaka wa kuanza kubadilisha uongozi.
Akijibu tuhuma hizo, Mulogo alikiri kutoa rushwa hiyo ya ahadi kwa sababu hakujua kama mkutano wa kampeni ulishafunguliwa.
“Mimi nilikuwa napita kwenda Mbeya, sikujua kama mkutano wa kampeni ulishafunguliwa ila niliwakuta watu wakiwa wamekusanyika na nikakumbuka kwamba niko katika kata ya mheshimiwa Menrad ambaye alishawahi kuniomba msaada wa mifuko ya saruji kwa ajili ya shule moja hivi katika kata yake. 
Niliahidi hivyo na nikasema nitatoa mifuko hiyo,” alisema Mulugo. Alipobanwa kwamba haoni kufanya hivyo ni kuvunja sheria, Mulugo alisisitiza kwamba hakujua kama mkutano wa kampeni ulishaanza.
Kwa mujibu wa sheria ya uchaguzi, viongozi wa serikali hawaruhusiwi kutoa msaada wala ahadi wakati wa mikutano ya kampeni kwani kufanya hivyo ni rushwa. CHANZO TANZANIA DAIMA.

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s