Majina ya Wanafunzi Waliochaguliwa kujiunga na Mafunzo ya Ualimu Mwaka wa Masomo 2013/2014 Haya Hapa


 

 

Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi,Dr Shukuru kawambwa. 
Serikali imetangaza majina ya wanafunzi 18,754 waliochaguliwa kujiunga na vyuo vya ualimu vilivyo chini yake ikiwa ni ongezeko la wanafunzi 1,659 ikilinganishwa na 17,095 waliochaguliwa mwaka jana.
 
Kati ya wanafunzi hao, 11,806 wamechaguliwa kusomea ngazi ya cheti (Grade A) na 6,948 watasoma katika ngazi ya stashahada.Wanafunzi 363 wamechaguliwa kusoma elimu maalumu kwa ngazi ya cheti huku 57 wakisoma elimu hiyo kwa ngazi ya stashahada.
 
MAELEKEZO MUHIMU:

Wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na Mafunzo ya Ualimu mwaka wa masomo 2013/2014 wanatakiwa kuripoti katika Vyuo walivyopangiwa tarehe 15/08/2013.

Fomu ya maelekezo (joining instruction) itatumwa kwa mhusika kupitia anuani yake. Aidha, fomu hizi zinapatikana pia kwenyetovuti hii  kwa kubofya katika link ya Chuo husika.
Wanafunzi wanatakiwa kufika Vyuoni wakiwa na mahitaji yafuatayo:

  1. Vyeti halisi vya Baraza la Mitihani la Tanzania kidato cha NNE na SITA kulingana na kozi husika;
  2. Ada ya muhula wa kwanza sh.100,000/= au ya mwaka sh. 200,000/=;
  3. Sare ya Chuo kulingana na maelekezo ya Chuo husika; na
  4. Fedha za tahadhari chuoni na matumizi binafsi.

Mkuu wa Chuo anatakiwa kuhakikisha wanafunzi wanaosajiliwa Chuoni ni wale waliopo kwenye orodha hii tu na SI vinginevyo.

Usajili wa waliochaguliwa kujiunga na Vyuo utafungwa tarehe 25/08/2013 saa 12.00 jioni.

*Bofya namba 1 au 2 hapa chini ili kupakua nakala yenye orodha ya majina

 

  1.  WALIOCHAGULIWA KUJIUNGA NA MAFUNZO YA UALIMU NGAZI YA CHETI 2013/2014 (1.64 MB)
  2.  WALIOCHAGULIWA KUJIUNGA NA MAFUNZO YA UALIMU NGAZI YA STASHAHADA 2013/2014 (997.5 kB)

TATIZO KATIBA MPYA NI MUUNGANO; WAKATI UMEFIKA KUACHANA NAO!


 

Mwalimu Julius Nyerere (kushoto) akibadilishana nyaraka na Mzee Abeid Amani Karume.

Na Walusanga Ndaki
WAKATI mjadala wa rasimu ya katiba mpya unaendelea nchi nzima katika mabaraza husika, tatizo kubwa linaloonekana kuvuruga na kutatiza mchakato mzima ni muungano wa sasa uliotokana na nchi za Tanganyika na Zanzibar.
Nimewahi kuandika mara kadhaa katika mtandao huu kwamba suala la muungano ambalo lilianza mwaka 1964 na sasa linakaribia kutimiza miaka 50 mwakani,  limekuwa na sura mbili zinazokinzana, hivyo lazima litafutiwe ufumbuzi leo, si kesho!
Ufumbuzi wenyewe ni kuwauliza  kwa kura wananchi wa Zanzibar ikiwa wanautaka au hawautaki muungano huu.

Ufumbuzi ni huo tu!  Hakuna ufumbuzi mwingine!  Ujanja mwingine wa kujaribu kulitatua suala hilo mbali na kuwauliza Wazanzibari, hautasaidia.  Ni kupoteza muda na raslimali bure kwa suala ambalo mamilioni ya wananchi wa pande hizi mbili –hususani wale wa Bara – hawalijui na wala haliwapi shibe yoyote!
Suala la muungano huu lina sura mbili zifuatazo:
Kwanza, kuna watu wanaoupenda muungano huu.  Watu hao idadi yao haijulikani, yaani hakuna aliyewahi kuwahesabu!  Watu pekee ambao unaweza ukawahesabu au kuwataja kwa majina ni   viongozi walioko madarakani Tanzania Bara na Zanzibar.

Hao ndiyo husema hadharani kuupenda na kuutetea  muungano huu.  Ni dhahiri watu hao husema hivyo kwa sababu umewanufaisha na kuwafikisha katika nafasi walizo nazo.  Kama kuna kero au maumivu yoyote ya muungano, wao si rahisi kuyakiri angalau hata kuyahisi.
 Hivyo, ni jambo la ajabu iwapo kuna kiongozi yeyote katika utawala wa nchi hii anayeweza kusema muungano haupendi!
Pili, kuna kundi la watu ambao nao husema hadharani  kutoupenda  muungano huu.  Vilevile, idadi ya watu hao haijulikani, kwani hakuna mtu ambaye amewahi kuwahesabu!    Isitoshe, nao husema hivyo kwa maslahi na hisia zao.  
 Wengi wa watu hawa (wasioupenda muungano) ni watu walioko mitaani, yaani watu ambao hawako katika safu za uongozi wa Tanzania Bara au Zanzibar!  Hivyo, kama kuna kero au maumivu yoyote yanayosababishwa na muungano huu, basi vyote hivyo wanavijua wao.

Baada ya kujua hivyo, uongozi wa nchi hii – kama unataka kulimaliza suala hilo kiungwana —  ni lazima uwaulize Wazanzibar kwa kura iwapo wanautaka muungano au la!  Kama wataukataa, basi ni lazima muungano ufe mara moja, Tanganyika wachukue nchi yao, na Zanzibar wachukue visiwa vyao ili maisha yaendelee bila misuguano isiyokuwa na tija, kwani hakuna sheria yoyote duniani inayowalazimisha watu kuungana au kuunganisha nchi zao!
Muungano ni suala la hiari, si la lazima!  Ni kama vile ndoa, ambamo wahusika huingia kwa hiari na wakaondoka kwa hiari.  Hakuna kulazimishana.  Muungano wa kisiasa, kama ndoa zilivyo, hauwezi kulindwa “kwa nguvu zote” kama wanasiasa wa nchi hii walivyozoea kusema.

Ifahamike wazi kwamba kitu chochote kinacholindwa “kwa nguvu zote” si cha hiari tena!  Hata katika ndoa, upande mmoja uking’ang’aniza kuishi na upande mwingine, hiyo inakuwa si ndoa tena!  Inakuwa ni jela ya mapenzi!
Vilevile, kusema kwamba “muungano ni tunu kutoka kwa Mwenyezi Mungu”, kama wanavyodai wanasiasa au viongozi wa nchi hii, ni njama za kutaka kurahisisha mambo kwa kuwatishia wananchi kwa kutumia  jina la Mungu.  
Na si vyema, kuwatisha wananchi kwa kutumia majina ya Nyerere na Karume ambao ndiyo waliosaini makubaliano ya kuanzishwa kwa Tanzania.  Vilevile si vyema kuendeleza matatizo ya muungano kwa kutaka kuwafurahisha Nyerere na Karume popote waliko!

Kizazi cha sasa kina haki ya kuelewa ni jinsi gani muungano huo ulivyoanza na malengo yake yalikuwa yapi.  Hiyo ni haki ya kila mtu katika nchi hii inayoitwa Tanzania.
Inawezekana, na ni dhahiri huko nyuma, hususani wakati wa utawala wa Nyerere, watu wengi walikuwa waoga kuhoji muundo na uhalali wa muungano huo.  Lakini, woga wa wananchi haukufanya kasoro za muungano ziondoke.  Ziliendelea kuwepo na viongozi waliofuata (baada ya Nyerere) wakajkinufaisha na woga wa Watanzania wengi waliokuwa wamefumba midomo yao.
Lakini, ukweli huwa haufi au hauuawi!  Wenye kuuhoji uhalali wa muungano huu bado wapo na kama kuna kasoro zilizokuwepo, bado zipo!  Vilevile, wenye madaraka ya kuweza kuziondoa kasoro hizo bado wapo.  Na wenye madaraka wasiotaka kuziondoa kasoro hizo, bado wapo pia!

Kama nilivyosema, ukweli hauwezi kuuawa na nguvu yoyote duniani!  Si kwa mazingaombwe wala risasi! Kama kweli muungano huu una kasoro za kweli, basi zitaendelea kuwepo daima, na asiyetaka kuziondoa kiungwana leo, ajue zitakuja kuondolewa kihuni na waungwana lakini kwa madhumuni ya kiungwana!
Kukubali kosa au dosari ni ujasiri na huonyesha busara kwa mhusika kwani jamii hutambua kwamba mhusika ana uwezo wa kutambua jema na baya.  Lakini, kwa mwenye kutaka kulinda heshima yake tu, ajue hubomoa si jamii tu, bali na heshima yake!
Kama nilivyosema, kwa upande wa Bara, kura hiyo siyo ya lazima kwani hakuna sababu yoyote ya msingi ya kuwauliza watu wa Bara, kwani hawana hisia za kupoteza chochote kihistoria, kiuchumi hata kiutamaduni. 

Tatizo kubwa limekuwa ni kwa Wanzanzibari ambao daima wamekuwa na wasiwasi wa kumezwa kwa taifa lao na hivyo kupoteza historia na utamaduni wao ambao umekuwepo kwa karne nyingi.
Kwa watu wenye msimamo wa busara na wasiojihusisha na upande wowote katika suala la muungano, watagundua kabisa kwamba madai ya watu wa Visiwani yaliyosababisha hadi kupata bendera yao, wimbo wao wa taifa, rais wao, katiba yao, na kadhalika, ni hatua za mwanzo za kutaka kuwa na nchi yao kamili inayotambulika duniani na katika taasisi zote ambazo nchi kamili hushiriki chini ya kivuli chake na si chini ya kivuli cha nchi nyingine.

Vilevile, muungano huu ulioanzishwa miaka karibu 50 iliyopita, umekuwa ni hadithi ya raha na karaha kwa vijana  ambao asilimia zaidi ya 80 walikuwa hawajazaliwa wakati unaanzishwa.  Hivyo, iwapo kura zitaruhusu kuendelea kwa muungano huu, hilo litawapa viongozi wa nchi hii baraka ya kutetea kitu ambacho kinakubalika na wengi.  
Lakini kama kura nyingi za Wazanzibari zitaukataa, hilo pia litawapa baraka ya kuachana na kitu ambacho hakitakiwi na wengi!
Majadiliano ya kumaliza migogoro ya muungano,  yamekuwa ni hadithi ya mbio za kupeana vijiji tangu enzi za marais Nyerere hadi  Kikwete!  Bila ya kuwauliza wenye nchi, yaani wananchi, viongozi wataendelea kubabaika na kuwababaisha wananchi wenzao kwa jambo ambalo linaweza kumalizwa mara moja, watu wakalisahau na wakaendelea na mambo mengine yenye tija zaidi kuliko kuhangaikia muungano wa nchi moja (Tanganyika) yenye watu karibu milioni 45 na nyingine (Zanzibar) yenye watu wapatao milioni moja!

Hicho ni kichekesho cha wazi!
Kinachotakiwa kwa viongozi ni kukumbuka kwamba: Kiongozi anatakiwa kufanya kile kinachotakiwa na wengi, si  kufanya kile anachotaka au kutamani yeye!
Isitoshe, Julius Kambarage Nyerere na Abeid Amani Karume hawakuwa miungu au malaika kiasi kwamba walichokipitisha hakiwezi kutenguliwa na binadamu!  Watu hao walikuwa ni binadamu, na kama walichokifanya leo kinaonekana kuwa na dosari, ni lazima binadamu wenzao wakirekebishe!
Kwa kutumia busara zaidi, lazima ifahamike kwamba inawezekana kabisa kwamba Nyerere na Karume waliupitisha muungano huo harakaharaka kwa sababu fulani ya kweli iliyokuwepo wakati huo.  Na inawezekana tena kabisa kwamba sababu hiyo iliyolazimisha muungano huo, leo hii haipo tena, hivyo sababu ya muungano wa Tanganyika na Zanzibar pia haipo tena!

Hivyo, wanaoutaka muungano, lazima wasikilizwe!  Vilevile, wasioutaka muungano lazima wasikilizwe!
Nasisitiza tena kwamba: Hakuna mtu aliyewahi kuwahesabu watu wanaoupenda muungano, na hakuna mtu aliyewahi kuwahesabu watu wasioupenda muungano!  Pande zote hizi mbili huvutia upande wao kwa kuwasemea watu ambao idadi yao haziwajui!
Ufumbuzi ni kura ya maoni kuwauliza  Wazanzibari iwapo wanautaka au kutoutaka muungano!   

Dk. Slaa awavaa CCM


KATIBU Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Willibrod Slaa, amesema kama utawala wa kimabavu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) ukiachwa uendelee, itafika mahali viongozi wake watataka kuabudiwa kama miungu.
 
Dk. Slaa alitoa kauli hiyo jana jijini Dar es Salaam wakati akifungua kongamano la kimataifa la vijana kutoka vyama vya kidemokrasia duniani (IYDU).
 
Alisema kuwa Tanzania ina upungufu mkubwa wa demokrasia na pengine upungufu mkubwa zaidi wa utashi wa chama tawala kuruhusu demokrasia ya vyama vingi.
 
“Ikiwa mfumo huu wa utawala wa kimabavu utaendelea, viongozi wetu wataanza kujiita kwa vyeo vya kikoloni kufuatia majina yao kama vile, Mheshimiwa A.N. jingine ; K.C.M.G; Mheshimiwa B.N. jingine G.C.M.G,” alisema.
 
“K.C.M.G linamaanisha Keep Calling Me God, yaani endelea kuniita Mungu na G.C.M.G linamaanisha God Calls Me God, yaani Mungu huniita Mungu,” alifafanua.
 
Dk. Slaa alibainisha kuwa hulka ya chama tawala nchini kutegemea mabavu kuongoza nchi inatokana na chama hicho kudumu madarakani kwa zaidi ya miaka 27 peke yake bila kuwepo vyama vya upinzani.
 
Alisema kipindi hicho kirefu ambacho CCM ilitawala bila kuwepo upinzani iliwafanya viongozi wake waamini kuwa wanayo haki ya kuitawala Tanzania peke yao.
 

 

JK awapa siku kumi na nne majambazi na wahamiaji haramu katika mikoa mitatu kujisalimisha.


 

 

 

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete ameamuru majambazi na wahamiaji haramu wote katika mikoa mitatu nchini kujisalimisha katika muda wa siku 14 kuanzia, Ijumaa, Julai 26, 2013 kabla ya kuanza kwa operesheni kubwa kuliko zote katika historia ya Tanzania nyenye lengo la kukomesha ujambazi katika mikoa hiyo na kukamata wahamiaji haramu.
 
Tanzania's President Kikwete address a news conference after meeting his Sudan counterpart al-Bashir in Khartoum
Rais Kikwete ambaye pia ni Amiri Jeshi Mkuu amesema kuwa leo ametoa amri kwa vyombo vyote vya ulinzi na usalama nchini kuanza maandalizii ya operesheni hiyo na hatimaye kuiendesha katika Mikoa ya Kagera, Kigoma na Geita.
 
“Majambazi wanateka magari, wanaua watu wetu, wanapora mali zao. Watanzania hawawezi kuendelea kuishi kwa hofu, woga na taabu katika nchi yao wenyewe. Tutawasaka majambazi misituni, tutawasaka majumbani, tutachimbua ardhini kutafuta hata silaha zilizofukiwa chini,” amesema Rais Kikwete.
 
Rais Kikwete ametoa amri hiyo mchana wa leo, Ijumaa, Julai 26, 2013 wakati alipohutubia wananchi wa mjini Biharamulo, Mkoani Kagera, kabla ya kuweka jiwe la msingi kwenye ujenzi wa barabara ya lami kutoka Kagoma, Wilaya ya Muleba kwenda Lusahuga, Biharamulo.
 
Rais Kikwete ametoa amri hiyo kufuatia matukio ya mara kwa mara na yasiyokuwa na mwisho ya majambazi kuteka mabasi, kuua watu na kupora mali zadi katika mikoa hiyo, hali ambayo imesababisha malalamiko ya wakazi wa mikoa hiyo.
 
Rais Kikwete ameaambia wananchi: “Tumeamua kukomesha upuuzi huu katika mikoa ya Kagera, Kigoma Geita. Leo nimetoa maagizo kwa vyombo vyetu vya ulinzi na usalama – Jeshi la Wananchi, Jeshi la Polisi, Uhamiaji na Usalama wa Taifa kuandaa operesheni maalum, operesheni kubwa kuliko zote tokea tupate uhuru. Upuuzi huu hauwezi kuendelea.”
 

 

DR. NCHIMBI AFUNGA MAFUNZO YA AWALI YA ASKARI POLISI NA UHAMIAJI


IWaziri wa mambo ya ndani ya nchi mh, Dr. Emmanuel Nchimbi akikaribishwa na mkuu wa jeshi la polisi nchini katika viwanja vya gwaride katika chuo cha polisi moshi (ccp) jana mkoani kilimanjaro alipokwenda kufunga mafunzo ya awali ya askari polisi na uhamiaji. takribani askari polisi elfu tatu na tisini na mbili walihitimu mafunzo, wakiwemo askari wa uhamiaji 51

 

AWaziri wa mambo ya ndani ya nchi Mh, Dr. Emmanuel Nchimbi akikagua gwaride la wahitimu wa mafunzo ya awali ya askari polisi wakati wa sherehe za kufunga mafunzo hayo jana katika chuo cha polisi moshi (CCP). takribani askari polisi elfu tatu na tisini na mbili walihitimu mafunzo, wakiwemo askari wa uhamiaji hamsini na moja. picha na hassan mndeme-jeshi la polisi.

 

BAskari polisi waliohitimu mafunzo, wakionyesha pikipiki inavyoweza kusaidia katika kukabiliana na wahalifu kwa waziri wa mambo ya ndani ya nchi mh, dr. emmanuel nchimbi aliyekua mgeni rasmi katika sherehe za kufunga mafunzo ya awali kwa askari polisi na uhamiaji jana mjini moshi. takribani askari polisi elfu tatu na tisini na mbili walihitimu mafunzo, wakiwemo askari wa uhamiaji hamsini na moja. picha na hassan mndeme-jeshi la polisi.

 

CWasanii wa kikundi cha ngoma cha chuo cha polisi Moshi wakitoa burudani jana mjini moshi wakati wa sherehe za kufunga mafunzo ya awali kwa askari polisi na uhamiaji. takribani askari polisi elfu tatu na tisini na mbili walihitimu mafunzo, wakiwemo askari wa uhamiaji hamsini na moja. picha na hassan mndeme-jeshi la polisi.

 

HWahitimu wa mafunzo ya awali ya askari polisi wakifanya onyesho la kareti  jana mjini moshi  wakati wa sherehe za kufunga mafunzo yaliyojumuisha askari polisi na uhamiaji. takribani askari polisi elfu tatu na tisini na mbili walihitimu mafunzo, wakiwemo askari wa uhamiaji hamsini na moja katika chuo cha polisi moshi (ccp). Picha na Hassan Mndeme-jeshi la polisi

 

JWaziri wa mambo ya ndani ya nchi mh, Dr. Emmanuel Nchimbi akimzawadia kirungu cha heshima mmoja kati ya wahitimu wa mafunzo ya awali ya askari polisi aliyefanya vizuri zaidi. Dr, Nchimbi alikua mgeni rasmi wakati wa kufunga mafunzo ya awali ya askari polisi na uhamiaji. takribani askari polisi elfu tatu na tisini na mbili walihitimu mafunzo, wakiwemo askari wa uhamiaji 51. picha na hassan mndeme-jeshi la polisi.

SOMA HOTUBA YA MHE. JAKAYA MRISHO KIKWETE, RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, WAKATI WA KUAGA WANAJESHI SABA WA KULINDA AMANI WALIOPOTEZA MAISHA DARFUR, SUDAN


 

Rais Jakaya Mrisho Kikwete akizungumza wakati wa zoezi hilo.Picha an Ofisi ya Makamu wa Rais

 

 

HOTUBA YA MHE. JAKAYA MRISHO KIKWETE, RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, WAKATI WA KUAGA WANAJESHI SABA WA KULINDA AMANI WALIOPOTEZA MAISHA DARFUR, SUDAN 

TAREHE 22 JULAI 2013

Mhe. Mohammed Gharib Bilal, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano;
Mhe. Balozi Seif Iddi, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar;
Mhe Shamsi Vuai Nahodha, Waziri wa Ulinzi na Jeshi laKujenga Taifa;
Waheshimiwa Mawaziri; Jenerali Davis Mwamunyange, Mkuu wa Majeshi yaUlinzi;
Wakuu wa Majeshi ya Ulinzi Wastaafu;Chief of Staff na Chief of Staff Wastaafu;Majenerali;
Maafisa Wakuu;
Maafisa Wadogo; Askari, Wafanyakazi raia wa Wizara ya Ulinzi na Jeshi laKujenga Taifa;
Waombolezaji wenzangu;
Familia za Wafiwa;
Mabibi na Mabwana.

Leo ni siku ngumu sana kutakiwa kuzungumza. Ugumuwenyewe unatokana na ule ukweli kwamba siyo siku ya furaha bali ya majonzi na huzuni kubwa kwangu, kwa taifaletu na familia za wanajeshi wetu saba marehemu ambaotumekusanyika hapa kuwaaga. Baada ya sherehe zakutunuku Kamisheni kwa Maofisa wapya katika Chuo chaMafunzo ya Kijeshi, Monduli Jumamosi tarehe 13 Julai, 2013 Mkuu wa Majeshi Jenerali Davis Mwamunyange aliniarifukutokea shambulio la kuvizia kwa baadhi ya wanajeshi wetuwalioko Darfur. Kwa kuwa wakati ule mapigano yalikuwayanaendelea, aliniambia kuwa atatoa taarifa zaidi baadae kadri taarifa zitakavyokuwa zinapatikana.

Baadae akanipa taarifa kuwa vijana wetu wamefarikina wengine wamejeruhiwa. Lazima nikiri kuwa taarifahiyo ilinihuzunisha, kunisikitisha na kunikasirisha. Kwa niniwatu wa Darfur wawaue wanajeshi wetu ambaowamekwenda kule kuwasaidia wapate utulivu, ili kunusurumaisha yao, kuwaondolea wasiwasi na kuwawezeshawafanye shughuli zenye tija kuendesha maisha yao. Mojakwa moja sikusita kuamini kuwa waliofanya hivyo ni watuwahalifu.

Tangu uhuru ni sera ya nchi yetu kutetea wanyongedhidi ya ukoloni, ubaguzi, uonevu, dhuluma na 

 

 

 

watu wotewalioko katika mazingira hatarishi Afrika na duniani. Njia za Kidiplomasia zilitumika na wakati mwingine JWTZlilishirikishwa. Ndio maana tumeshiriki kwenye vita vyaukombozi katika nchi kadhaa zilizopo Kusini mwa Afrika.Vilevile tumeshiriki katika shughuli za kulinda amani katikanchi mbalimbali zikiwemo Liberia, Sierra Leone na Eritrea.Hivi sasa Jeshi letu linaendelea na jukumu hilo nchiniLebanon, Cote d’Ivoire, Darfur (Sudan), Sudan Kusini na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Katika nchi zote hizo,askari wetu wanasifiwa sana kwa bidii ya kazi, uvumilivu,uhodari na nidhamu ya hali ya juu.

Wakati wote tulipoombwa na kukubali kupelekawanajeshi wetu kutekeleza majukumu hayo, uwezekano wawao kujeruhiwa au kufariki yanafikiriwa kutokea.Wanakwenda kwenye maeneo yenye mapigano hivyohatari hizo kutokea ni jambo linalowezekana. Tahadharizote husika huchukuliwa kuepusha hatari hizo. Ndiyomaana hupewa mafunzo ya kutosha na silaha za kutosha.Hata hivyo hutokea nyakati kukatokea yasiyotarajiwa kamayaliyotokea Darfur. Pia yaliwahi kutokea Liberia.

Kufuatia tukio hilo, nilizungumza na Katibu Mkuu waUmoja wa Mataifa ambaye alinielezea masikitiko yakemakubwa kwa yaliyotokea na kutoa pole zake nyingi. Pia alinieleza kuwa alizungumza na Rais Bashir wa Sudanakitaka wahalifu hao wasakwe, wakamatwe na kuadhibiwaipasavyo. Aidha, nilifanya mazungumzo na Rais Omar AlBashir wa Sudan, ambaye naye alinielezea masikitiko yakena kutoa pole nyingi. Katika mazungumzo yangu naye nilimsisitizia umuhimu wa Serikali yake kufanya uchunguziwa kina wa shambulizi hilo na kuwawajibisha waliohusika. Rais Bashir alikubaliana nami na kuahidi kufanya kilalinalowezekana ili ukweli ufahamike na hatua stahikizichukuliwe.

Sisi kwa upande wetu, Jeshi la Wananchi wa Tanzanialimeunda Bodi ya Uchunguzi inayotarajiwa kuelekea Sudankwa ajili ya kufanya uchunguzi wa kina kubaini chanzo chashambulizi hilo.

Kwa huko Darfur, tangu shughuli za ulinzi wa amani waUNAMID zianze mwaka 2007 walinzi wa amani 41 kutokamataifa mbalimbali wameuawa na zaidi ya walinzi wa amani 55 wamejeruhiwa. Kwa kweli idadi hii ni kubwa mnoinayohitaji kutafakariwa vizuri na wadau wote. Penginewakati umefika wa kuutazama upya mfumo wa kulindaamani Darfur hasa kuhusu uwezo wa kujilinda na wanajeshiwanaolinda amani. Hapana budi uwezo wao uongezwe ili kupunguza vifo na majeruhi. Narudia kuahidi kuwa rai hiitutaifikisha kwa mamlaka husika katika Umoja wa Mataifana Umoja wa Afrika.

Napenda kuchukua nafasi hii kuishukuru serikali yaSudan, Umoja wa Afrika na Umoja wa Mataifa kwaushirikiano mkubwa waliotupatia tangu kutokea kwa tukiola kushambuliwa kwa askari wetu. Pia nawashukuru nakutoa pongezi kwa Waziri Shamsi Vuai Nahodha, JeneraliDavis Mwamunyange na makamanda na askari wote wa JWTZ, kwa jinsi walivyoshughulikia msiba huu tanguilipopokelewa taarifa ya vifo vya mashujaa wetu hawampaka sasa. Mmewapa heshima kubwa wanaoistahili.Asanteni sana.

Kwa namna ya pekee, narudia kutoa pole nyingi kwafamilia za wafiwa. Nawashukuru kwa dhati kwa moyo waowa uvumilivu na subira. Naomba mfahamu kuwa, mimi naWatanzania wote tupo pamoja nanyi katika kuombolezavifo vya mashujaa wetu. Msiba huu ni wa taifa letu lote nawatu wote wenye kupenda amani duniani.

Daima tutawakumbuka mashujaa wetu na tutaendeleakuenzi na kujivunia kazi zao na mchango wao mkubwa kwanchi yetu na dunia kwa ujumla. Nawaomba sote tuendelee kumuomba Mwenyezi Mungu aziweke roho za mashujaawetu mahala pema peponi. Amen.

Kwa Jeshi na wanajeshi wetu wote, napenda kumaliziakwa kuwaasa kuwa yaliyotokea Darfur yasiwakatishe tamaakatika kutimiza wajibu wetu Darfur na kwingineko. Yaliyopita si ndwele, tugange yajayo.

Yaliyotokeayanatukumbusha kuchukua tahadhari zaidi na kuongezauwezo wa kujihami wa wanajeshi wetu kila wanapotumwakutekeleza jukumu lao.

Asanteni

TAARIFA MAALUM YA CHADEMA KWA UMMA KUHUSU KAULI YA CCM JUU YA KODI YA KUMILIKI KADI YA SIMU YA MKONONI/KIGANJANI


 
 

 
Mkurugenzi wa Habari na Uenezi  na mbunge wa jimbo la ubungo chadema John Mnyika
  Taarifa iliyotolewa na CCM na kunukuliwa na vyombo mbalimbali vya habari tarehe 18 Julai 2013 ya kuitaka Serikali inayoongozwa na CCM kuangalia njia nyingine mbadala ya kukusanya kodi na kuachana na hatua yake ya kukusanya kodi ya umiliki wa kadi ya sh. 1000 kila mwezi imethibitisha maneno ya Mwalimu Nyerere kwamba ‘chama lege lege huzaa serikali legelege’.

Aidha, taarifa hiyo ni mkakati legelege wa kujinasua katika malalamiko, kukusanywa kwa saini, kuandaliwa kwa miswada ya sheria, migomo ya kuzima simu kwa muda maalum na maandamano dhidi ya Serikali ya CCM kutokana na chama hicho kushindwa kuwa na sera sahihi na mikakati makini.

Taarifa hiyo haiwezi kurudisha nyuma hatua ya wananchi kukikataa chama hicho na kuunga mkono mabadiliko ya kweli kupitia CHADEMA kwa kuzingatia kuwa CCM imeshindwa kuhakikisha kwamba Ilani zake za uchaguzi ya mwaka 2005 na 2010 zinatekelezwa. Ikumbukwe kwamba kupitia ilani hizo CCM iliahidi maisha bora kwa kila mtanzania na badala yake maisha ya wananchi yamezidi kuwa magumu kutokana na ongezeko la bei na gharama za maisha.

Ili taarifa hiyo isiwe maneno matupu, Rais Jakaya Kikwete ambaye pia ni mwenyekiti wa CCM ajitokeze na 

 
 kuagiza utozaji wa kodi hiyo usitishwe kuanzia sasa. Izingatiwe kwamba Muswada huo ambao Rais aliusaini mwanzoni mwa mwezi Julai ulianzisha pia ushuru mwingine na tozo zingine mbalimbali zenye kuongezea mzigo wa gharama za maisha wananchi hususan wa kipato cha chini badala ya kuweka mkazo katika kupanua wigo wa vyanzo mbadala nchini.

Kadhalika, kwa kuwa chanzo cha hali hiyo ni maamuzi yaliyofanywa katika Mkutano wa kumi na moja wa Bunge uliopitisha Muswada wa Sheria ya Fedha wa mwaka 2013; ufumbuzi lazima uhusishe marekebisho ya sheria kufuta makosa yaliyofanywa na Serikali ya CCM na kupigiwa kura ya ndio na Bunge lililohodhiwa na CCM.

Hivyo, Rais Kikwete awasilishe katika mkutano wa Bunge kwa hati ya dharura muswada wa sheria wa kufuta vifungu vilivyoingizwa kwa marekebisho ya Sheria ya Ushuru wa Bidhaa, Sura 147 na kuondoa ushuru wa bidhaa kwa kadi za simu (sim card) kwa wamiliki wa simu za kiganjani/mkononi.

Taarifa hiyo isipoambatana na hatua za Rais Kikwete kuagiza Mamlaka ya Mapato (TRA) kuacha kutoza ushuru huo na Rais kuwasilisha muswada bungeni kupitia Waziri wa Fedha itakuwa ‘kiini macho’ kama ilivyokuwa taarifa nyingine kama hiyo iliyotolewa na msemaji huyu huyu wa CCM mwaka 2011.

Taarifa ya Nape Nnauye inapaswa kupuuzwa kwa kuwa alitoa taarifa nyingine kwamba CCM kupitia kikao cha kamati kuu yake Agosti 2011 ‘imeagiza’ Serikali ‘kutafuta njia ya kushusha bei ya mafuta ya taa’ iliyopanda baada ya kuongeza kodi ya mafuta ya taa.

Badala ya agizo hilo kutekelezwa mafuta ya taa yaliendelea kupanda bei na kinyume na agizo hilo katika mkutano wa 11 wa Bunge mwaka 2013 Serikali hiyo hiyo ya CCM ikawasilisha bungeni muswada wa sheria ya fedha na majedwali ya marekebisho ya kuongeza kodi ya mafuta ya taa kinyume cha agizo hilo.

Taarifa hiyo haiwezi kuinasua CCM dhidi ya kuendelea kukataliwa kwa kuwa imehusika katika maaandalizi ya bajeti ya Serikali na muswada wa sheria ya fedha kabla na wakati wa mkutano wa Bunge uliofanya maamuzi ya kuwaongezea gharama za maisha wananchi. Chama hicho kimeshiriki moja kwa moja kupitia vikao vyake vya kikatiba ikiwemo kamati kuu, sekretariati na kamati ya wabunge wa chama hicho.

Taarifa hiyo imethibitisha madhara ya Serikali ya CCM na wabunge wanaotokana na chama hicho wanavyoshindwa kusimamia maslahi ya umma kwa kuwa iwapo dhamira hiyo ingekuwepo katika hatua za awali wasingewasilisha bungeni mapendekezo hayo. Hata baada ya kuyawasilisha wangeyaondoa katika hatua zote kufuatia kodi hiyo kupingwa na kambi rasmi ya upinzani inayoongozwa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).

CCM itambue kwamba wananchi wanakumbuka kuwa kodi hiyo ya simu iliingizwa kwa mara ya kwanza ndani ya ukumbi wa Bunge na Rais kupitia kwa Waziri wa Fedha aliposoma bajeti ya Serikali ya CCM. Ilikuwepo kwenye Hotuba ya maandishi ya Waziri huyo ambaye pia ni mbunge wa CCM lakini wakati wa kusoma akaruka sehemu hiyo na kutangaza kwamba imefutwa. 

CCM ieleze katika hatua hiyo, wazo hilo lilitoka kwa nani mpaka likaingia katika kitabu cha hotuba ya Waziri na nini maamuzi ya Baraza la Mawaziri ambalo Mwenyekiti ni Rais (ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM) kwenye kikao kilichofanyika siku moja kabla ya yeye kusoma hotuba yake kilichojadili hatua za kikodi (tax measures).

Kifungu hiki kilirejeshwa kwa mara nyingine tena kwenye Muswada wa Sheria ya Fedha kupitia jedwali la Marekebisho lililowasilishwa na Waziri wa Fedha mwenyewe kwa niaba ya Serikali ya CCM na Bunge lenye kuhodhiwa na CCM likakipitisha. CCM iwapo ilikuwa na msimamo wa kuona kwamba kodi hiyo ni mzigo kwa wananchi kwanini haikuwasiliana na wabunge wake ambao ndio wengi katika Bunge kuhakisha kwamba wanaikataa.

Iwapo CCM haitajitokeza kutoa majibu na Rais hataagiza kwamba kodi hiyo isitishwe na muswada kuwasilishwa bungeni kuifuta, natoa mwito kwa wananchi kujitokeza katika mkutano wa hadhara nitakaoshiriki tarehe 21 Julai 2013 katika Uwanja wa Sahara kata ya Mabibo kuanzia saa 8 Mchana mpaka saa 11 Jioni.

Mkutano huo uliandaliwa kwa lengo la kutoa mrejesho kuhusu yaliyojiri bungeni katika mkutano uliopita na kupokea masuala ya kuyawasilisha katika mkutano ujao. Aidha, uchambuzi utafanyika kuhusu rasimu ya katiba sanjari na juu ya mchakato wa katiba mpya.

Hivyo, kupitia mkutano huo saini zitaendelea kukusanywa kwa ajili ya kutaka kodi hiyo ya kumiliki kadi za simu isitishwe na muswada kupelekwa bungeni kuifuta kodi hiyo yenye kuongeza gharama za maisha kwa wananchi na kuathiri haki ya kupata na kutoa taarifa pamoja na uhuru wa mawasiliano.

Taarifa hiyo imedhihirisha namna ambavyo tumefika hapa tulipo kutokana na udhaifu wa Serikali ya CCM, uzembe wa Bunge (ambalo limehodhiwa na CCM) na ulegelege wa CCM.

Hivyo, umma uipuuze na kuendelea kuchukua hatua za kuiunga mkono CHADEMA katika dhamira na dhima yake ya kuleta uongozi bora, sera sahihi, mikakati makini na oganizesheni thabiti kwa maendeleo endelevu ya Tanzania.
Imetolewa tarehe 18 Julai 2013 na:
John Mnyika (Mb)
Mkurugenzi wa Habari na Uenezi