TATIZO KATIBA MPYA NI MUUNGANO; WAKATI UMEFIKA KUACHANA NAO!

 

Mwalimu Julius Nyerere (kushoto) akibadilishana nyaraka na Mzee Abeid Amani Karume.

Na Walusanga Ndaki
WAKATI mjadala wa rasimu ya katiba mpya unaendelea nchi nzima katika mabaraza husika, tatizo kubwa linaloonekana kuvuruga na kutatiza mchakato mzima ni muungano wa sasa uliotokana na nchi za Tanganyika na Zanzibar.
Nimewahi kuandika mara kadhaa katika mtandao huu kwamba suala la muungano ambalo lilianza mwaka 1964 na sasa linakaribia kutimiza miaka 50 mwakani,  limekuwa na sura mbili zinazokinzana, hivyo lazima litafutiwe ufumbuzi leo, si kesho!
Ufumbuzi wenyewe ni kuwauliza  kwa kura wananchi wa Zanzibar ikiwa wanautaka au hawautaki muungano huu.

Ufumbuzi ni huo tu!  Hakuna ufumbuzi mwingine!  Ujanja mwingine wa kujaribu kulitatua suala hilo mbali na kuwauliza Wazanzibari, hautasaidia.  Ni kupoteza muda na raslimali bure kwa suala ambalo mamilioni ya wananchi wa pande hizi mbili –hususani wale wa Bara – hawalijui na wala haliwapi shibe yoyote!
Suala la muungano huu lina sura mbili zifuatazo:
Kwanza, kuna watu wanaoupenda muungano huu.  Watu hao idadi yao haijulikani, yaani hakuna aliyewahi kuwahesabu!  Watu pekee ambao unaweza ukawahesabu au kuwataja kwa majina ni   viongozi walioko madarakani Tanzania Bara na Zanzibar.

Hao ndiyo husema hadharani kuupenda na kuutetea  muungano huu.  Ni dhahiri watu hao husema hivyo kwa sababu umewanufaisha na kuwafikisha katika nafasi walizo nazo.  Kama kuna kero au maumivu yoyote ya muungano, wao si rahisi kuyakiri angalau hata kuyahisi.
 Hivyo, ni jambo la ajabu iwapo kuna kiongozi yeyote katika utawala wa nchi hii anayeweza kusema muungano haupendi!
Pili, kuna kundi la watu ambao nao husema hadharani  kutoupenda  muungano huu.  Vilevile, idadi ya watu hao haijulikani, kwani hakuna mtu ambaye amewahi kuwahesabu!    Isitoshe, nao husema hivyo kwa maslahi na hisia zao.  
 Wengi wa watu hawa (wasioupenda muungano) ni watu walioko mitaani, yaani watu ambao hawako katika safu za uongozi wa Tanzania Bara au Zanzibar!  Hivyo, kama kuna kero au maumivu yoyote yanayosababishwa na muungano huu, basi vyote hivyo wanavijua wao.

Baada ya kujua hivyo, uongozi wa nchi hii – kama unataka kulimaliza suala hilo kiungwana —  ni lazima uwaulize Wazanzibar kwa kura iwapo wanautaka muungano au la!  Kama wataukataa, basi ni lazima muungano ufe mara moja, Tanganyika wachukue nchi yao, na Zanzibar wachukue visiwa vyao ili maisha yaendelee bila misuguano isiyokuwa na tija, kwani hakuna sheria yoyote duniani inayowalazimisha watu kuungana au kuunganisha nchi zao!
Muungano ni suala la hiari, si la lazima!  Ni kama vile ndoa, ambamo wahusika huingia kwa hiari na wakaondoka kwa hiari.  Hakuna kulazimishana.  Muungano wa kisiasa, kama ndoa zilivyo, hauwezi kulindwa “kwa nguvu zote” kama wanasiasa wa nchi hii walivyozoea kusema.

Ifahamike wazi kwamba kitu chochote kinacholindwa “kwa nguvu zote” si cha hiari tena!  Hata katika ndoa, upande mmoja uking’ang’aniza kuishi na upande mwingine, hiyo inakuwa si ndoa tena!  Inakuwa ni jela ya mapenzi!
Vilevile, kusema kwamba “muungano ni tunu kutoka kwa Mwenyezi Mungu”, kama wanavyodai wanasiasa au viongozi wa nchi hii, ni njama za kutaka kurahisisha mambo kwa kuwatishia wananchi kwa kutumia  jina la Mungu.  
Na si vyema, kuwatisha wananchi kwa kutumia majina ya Nyerere na Karume ambao ndiyo waliosaini makubaliano ya kuanzishwa kwa Tanzania.  Vilevile si vyema kuendeleza matatizo ya muungano kwa kutaka kuwafurahisha Nyerere na Karume popote waliko!

Kizazi cha sasa kina haki ya kuelewa ni jinsi gani muungano huo ulivyoanza na malengo yake yalikuwa yapi.  Hiyo ni haki ya kila mtu katika nchi hii inayoitwa Tanzania.
Inawezekana, na ni dhahiri huko nyuma, hususani wakati wa utawala wa Nyerere, watu wengi walikuwa waoga kuhoji muundo na uhalali wa muungano huo.  Lakini, woga wa wananchi haukufanya kasoro za muungano ziondoke.  Ziliendelea kuwepo na viongozi waliofuata (baada ya Nyerere) wakajkinufaisha na woga wa Watanzania wengi waliokuwa wamefumba midomo yao.
Lakini, ukweli huwa haufi au hauuawi!  Wenye kuuhoji uhalali wa muungano huu bado wapo na kama kuna kasoro zilizokuwepo, bado zipo!  Vilevile, wenye madaraka ya kuweza kuziondoa kasoro hizo bado wapo.  Na wenye madaraka wasiotaka kuziondoa kasoro hizo, bado wapo pia!

Kama nilivyosema, ukweli hauwezi kuuawa na nguvu yoyote duniani!  Si kwa mazingaombwe wala risasi! Kama kweli muungano huu una kasoro za kweli, basi zitaendelea kuwepo daima, na asiyetaka kuziondoa kiungwana leo, ajue zitakuja kuondolewa kihuni na waungwana lakini kwa madhumuni ya kiungwana!
Kukubali kosa au dosari ni ujasiri na huonyesha busara kwa mhusika kwani jamii hutambua kwamba mhusika ana uwezo wa kutambua jema na baya.  Lakini, kwa mwenye kutaka kulinda heshima yake tu, ajue hubomoa si jamii tu, bali na heshima yake!
Kama nilivyosema, kwa upande wa Bara, kura hiyo siyo ya lazima kwani hakuna sababu yoyote ya msingi ya kuwauliza watu wa Bara, kwani hawana hisia za kupoteza chochote kihistoria, kiuchumi hata kiutamaduni. 

Tatizo kubwa limekuwa ni kwa Wanzanzibari ambao daima wamekuwa na wasiwasi wa kumezwa kwa taifa lao na hivyo kupoteza historia na utamaduni wao ambao umekuwepo kwa karne nyingi.
Kwa watu wenye msimamo wa busara na wasiojihusisha na upande wowote katika suala la muungano, watagundua kabisa kwamba madai ya watu wa Visiwani yaliyosababisha hadi kupata bendera yao, wimbo wao wa taifa, rais wao, katiba yao, na kadhalika, ni hatua za mwanzo za kutaka kuwa na nchi yao kamili inayotambulika duniani na katika taasisi zote ambazo nchi kamili hushiriki chini ya kivuli chake na si chini ya kivuli cha nchi nyingine.

Vilevile, muungano huu ulioanzishwa miaka karibu 50 iliyopita, umekuwa ni hadithi ya raha na karaha kwa vijana  ambao asilimia zaidi ya 80 walikuwa hawajazaliwa wakati unaanzishwa.  Hivyo, iwapo kura zitaruhusu kuendelea kwa muungano huu, hilo litawapa viongozi wa nchi hii baraka ya kutetea kitu ambacho kinakubalika na wengi.  
Lakini kama kura nyingi za Wazanzibari zitaukataa, hilo pia litawapa baraka ya kuachana na kitu ambacho hakitakiwi na wengi!
Majadiliano ya kumaliza migogoro ya muungano,  yamekuwa ni hadithi ya mbio za kupeana vijiji tangu enzi za marais Nyerere hadi  Kikwete!  Bila ya kuwauliza wenye nchi, yaani wananchi, viongozi wataendelea kubabaika na kuwababaisha wananchi wenzao kwa jambo ambalo linaweza kumalizwa mara moja, watu wakalisahau na wakaendelea na mambo mengine yenye tija zaidi kuliko kuhangaikia muungano wa nchi moja (Tanganyika) yenye watu karibu milioni 45 na nyingine (Zanzibar) yenye watu wapatao milioni moja!

Hicho ni kichekesho cha wazi!
Kinachotakiwa kwa viongozi ni kukumbuka kwamba: Kiongozi anatakiwa kufanya kile kinachotakiwa na wengi, si  kufanya kile anachotaka au kutamani yeye!
Isitoshe, Julius Kambarage Nyerere na Abeid Amani Karume hawakuwa miungu au malaika kiasi kwamba walichokipitisha hakiwezi kutenguliwa na binadamu!  Watu hao walikuwa ni binadamu, na kama walichokifanya leo kinaonekana kuwa na dosari, ni lazima binadamu wenzao wakirekebishe!
Kwa kutumia busara zaidi, lazima ifahamike kwamba inawezekana kabisa kwamba Nyerere na Karume waliupitisha muungano huo harakaharaka kwa sababu fulani ya kweli iliyokuwepo wakati huo.  Na inawezekana tena kabisa kwamba sababu hiyo iliyolazimisha muungano huo, leo hii haipo tena, hivyo sababu ya muungano wa Tanganyika na Zanzibar pia haipo tena!

Hivyo, wanaoutaka muungano, lazima wasikilizwe!  Vilevile, wasioutaka muungano lazima wasikilizwe!
Nasisitiza tena kwamba: Hakuna mtu aliyewahi kuwahesabu watu wanaoupenda muungano, na hakuna mtu aliyewahi kuwahesabu watu wasioupenda muungano!  Pande zote hizi mbili huvutia upande wao kwa kuwasemea watu ambao idadi yao haziwajui!
Ufumbuzi ni kura ya maoni kuwauliza  Wazanzibari iwapo wanautaka au kutoutaka muungano!   

Advertisements

One Comment

  1. NI DHAHIRI KABISA ULIYOYASEMA NI YA WAZI KABISA KWAMBA WANAONG’ANG’ANIA MUUNGANO BILA KUUJUA MATAKWA YA WANANCHI NI VIONGOZI AMBAO WANAFAIDI MATUNDA YA MFUMO HUU WA UTAWALA. WANANCHI WALIOWENGI HAWAGUSWI NA CHOCHTE KWA KUWEPO NA KUTOKUWEPO KWA MUUNGANO. LA MSINGI VIONGOZI WASIKILIZE MAONI YA WANANCHI KUHUSU MUUNGANO BILA YA KUPANDIKIZA MAWAZO AMBAYO HAYATOKANI NA MATAKWA YAPO

    Like

    Reply

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s