YANGA: AL AHLY MKIINGIA TUNAWACHINJA

WIKIENDI hii zinachezwa mechi 16 za raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika. Lakini macho ya Afrika nzima yapo Dar es Salaam ambapo mabingwa watetezi wa mashindano hayo, Al Ahly, itacheza na Yanga kwenye Uwanja wa Taifa.

Afrika inafuatilia kwa karibu mechi hiyo kutokana na kupepesuka kwa Ahly kwenye ligi yao ya ndani katika siku za hivi karibuni huku Yanga ikionekana kupania kuangusha mbuyu uliowashinda Waafrika wengi.

Yanga imesisitiza kwamba itapambana kwa namna yoyote ile kuhakikisha inaidhalilisha Al Ahly jijini Dar es Salaam na kurahisisha kazi ya mchezo ujao ambao utakuwa ugenini Cairo.

Si wachezaji tu, hata kocha Hans Pluijm amepania kuweka historia ya aina yake akiwa na Yanga kwani ana uzoefu mkubwa na mashindano hayo. Mechi hiyo itakayoanza saa 10:00 jioni, itashuhudia ushindani wa aina yake huku Yanga ikipania kushambulia kwa nguvu na kubana sehemu ya kiungo na beki.

Yanga kabla ya kufika katika mchezo huo utakaochezeshwa na mwamuzi kutoka Ethiopia, Bazezew Belete, iliiondoa Komorozine ya Comoro kwa mabao 12-2. Yanga imekuwa ikijinoa kwenye Uwanja wa Boko Beach Veteran ulioko Tegeta, nje kidogo ya jiji huku ikipiga kambi kwenye hoteli ya Bahari Beach.

Mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu Bara wamekuwa wakipiga tizi asubuhi na jioni huku kocha akisisitiza zaidi umakini na kutumia nafasi pamoja na kuwajenga kisaikolojia wachezaji wake.

Kwa mujibu wa mazoezi yake, Yanga huenda ikaanzisha kikosi hiki; Deo Munishi ‘Dida’/Juma Kaseja, Mbuyu Twite, Oscar Joshua, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Kelvin Yondani, Frank Domayo, Simon Msuva, Haruna Niyonzima, Mrisho Ngassa, Emmanuel Okwi na Hamis Kiiza. Katika nafasi ya kipa, Dida, ameonekana kuwa chaguo la kocha, lakini Juma Kaseja pia ana nafasi ya kuanza.

Okwi atashuka uwanjani kuichezea Yanga kimataifa kwa mara ya kwanza baada ya Shirikisho la Kimataifa la Soka (Fifa) kubariki usajili wake Jangwani.

Yanga huenda ikatumia mifumo miwili ya 4-3-3 na 4-3-2-1 ambayo hutumiwa pia na Ahly ambayo huenda ikajilinda zaidi.

Pluijm aliishusha Yanga mazoezini kwenye Uwanja wa Taifa jana Ijumaa jioni na baadaye wakafanya wapinzani wao.

“Hatuwezi kuwaogopa kabisa Ahly, nafurahi kuona kila kitu kipo sawa morali kwa wachezaji iko juu kwa kiwango cha kutosha, tutawashangaza wote wanaotubeza wakifikiri Yanga ni timu ndogo. Lakini tunawaheshimu Ahly kupitia rekodi yao katika mashindano haya,” alisema kocha huyo.

Wachezaji wa Yanga wameshatangaziwa zaidi ya Sh100 milioni na matajiri wa timu hiyo wakiongozwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano ya Kimataifa, Seif Ahmed ‘Seif Magari’ na Makamu wake, Mussa Katabaro na Abdallah Bin Kleb, ambao wamepania kuweka historia katika uongozi wao chini ya Yusuf Manji.

Ahly tayari imepatwa na wasiwasi kwani juzi Alhamisi iliwatimua madereva wa magari waliyoyakodi wasishuhudie mazoezi yao kwa hofu ya kufanyiwa mizengwe. Pia katika hoteli ya Hyat Kempinski walipofikia, Waarabu hao wanafanya mambo kwa machale.

Yanga inatakiwa kuwa makini na washambuliaji wa Ahly, Mohamed Nagy ‘Gedo’ anayevaa jezi namba 15 na Amri Gamal wa jezi namba 17, ambao hawana masihara katika eneo la hatari kwa umahiri wao katika umaliziaji wa pasi za mwisho, hivyo ni wazi Cannavaro na Yondani wanatakiwa kuhakikisha wanawanyima nafasi ya kusogea karibu na eneo la 18. Lakini pia kuhakikisha hawaruki peke yao kutokana na shabaha ya vichwa vyao.

Ahly ni hatari kwa mashambulizi ya kutoka katikati ya uwanja, lakini pia hata mawinga wake hasa wa kulia huzalisha mabao yao.

Wakati akitua Jumatano kocha wa Ahly, Mohamed Youssef, alisema: “Tunawaheshimu Yanga, ni moja ya timu bora Tanzania kama ilivyo Simba. Lakini tumejiandaa vizuri kabla ya mechi hii, tunataka kuwaondoa ili tuendelee na mashindano haya, tunataka kupata ushindi hakuna shida katika hilo.”

Minziro aonya mabeki

Kocha Msaidizi wa zamani wa Yanga ambaye sasa anainoa JKT Ruvu, Fred Minziro, ameonya kuwa mabeki wanapaswa kuacha uzembe na kufanya kazi ya ziada.

Minziro aliyekuwa akiifundisha Yanga kwenye mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu Bara, alisema: “Yanga wana washambuliaji wakali, tatizo lipo kwa mabeki ambao mara nyingi huwa wanaigharimu timu kwa makosa ya kizembe.

“Kama watatumika akina Cannavaro, Kevin Yondani, Mbuyu (Twite) na Oscar (Joshua) basi wapangiwe majukumu maalumu wasiingiliane. Beki ya Yanga inahitaji kuwa na mawasiliano mazuri na kipa, wasimpoteze kipa na kumfanya abebeshwe lawama.”

Kibadeni atoa ufundi

Kocha mkongwe wa Ashanti United, Abdallah Kibadeni, amemwambia Mholanzi, Hans Pluijm na wachezaji wake kuwa kama wanataka kusonga mbele kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika basi wasiruhusu bao nyumbani.

“Ninawashauri Yanga kushambulia goli la wapinzani wao dakika zote 90 na siyo kulinda goli lao, kikubwa wanachotakiwa ni kujiamini na kutoihofia Al Ahly. Kweli wapinzani wao ni timu bora, lakini ninaamini Yanga nao wapo vizuri wana washambuliaji wenye uwezo mkubwa,” alisema Kibadeni.

Logarusic aipa mbinu

Kocha wa Simba, Zdravko Logarusic, amewataka Watanzania wote wakiwamo wa timu yake, kuishangilia Yanga dhidi ya Al Ahly bila kujali itikadi zao za kisoka, lakini akaipa onyo klabu hiyo ya Jangwani kwamba isiidharau mechi hiyo.

“Yanga ina nafasi kubwa ya kushinda kwani imetoka kupata matokeo mazuri katika ligi yetu, timu za Kiarabu sasa zinaweza kuwa sawa na za Afrika Mashariki kwani uwekezaji wa soka umekua mkubwa kama Afrika Kaskazini na Magharibi,” alisema.

“Yanga wacheze kwa kujiamini na kutodharau hata nafasi moja wanayopata, ni vyema wakashinda kama bao 1-0 au 2-0, wasiruhusu bao kwani faida ya bao la ugenini kwa Ahly inaweza kuwaweka mahali pabaya, wawachunge mawinga wa jamaa, maana ni hatari na wanajua wanachofanya.”

Chanzo:Mwanaspoti

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s