Na Jackline Masinde, Mwananchi
Geita. Viongozi na jamii nchini wametakiwa kuwa makini na vyama vya siasa na makundi yanayoibuka ndani ya Bunge la Katiba kwa lengo la kupindisha maoni yaliyotolewa.

Badala yake wametakiwa kusimama kwenye mstari na kuwatetea wananchi, kwani wao ndiyo wawakilishi wao kwenye Bunge hilo.
Hayo yalisemwa jana na Askofu wa Jimbo Katoliki la Geita, Damian Dallu wakati wa iliyofanyika katika Kanisa Katoliki la Bikira Maria wa Fatima. Hivi sasa Bunge la Katiba linakabiliwa na wakati mgumu kutokana na msuguamo miongoni mwa wajumbe juu ya mfumo sahihi wa upigaji kura.
“Hakika kuna watu wanaibuka, wanapinga baadhi ya maoni yalitolewa na wananchi na wengine wanaleta maoni mapya,” alisema.
Dallu alisema inasikitisha kuona kuna baadhi ya wajumbe wako bungeni kwa ajili ya masilahi binafsi na siyo kwa niaba ya wananchi.
Alisema vitendo hivyo ni hatari kwa taifa na jamii, hivyo haipo sababu ya viongozi kufumba macho dhidi ya watu wachache wenye tabia za kutaka masilahi binafsi.
“Amani inalindwa na katiba ya nchi, kama tukiharibu katiba basi tufahamu kwamba tumeharibu amani ya taifa.
Viongozi wote wa dini tuliombee Bunge hili ili Mungu aliepushe na watu wenye maoni binafsi kwa masilahi yao,” alisema zaidi Dallu.
Advertisements