TUZO ZA WANAMICHEZO BORA 2013/2014


 

index
MIFUKO ya hifadhi ya Jamii ya NSSF na PSPF imejitokeza kudhamini tuzo za Wanamichezo Bora wa Tanzania ambazo zitafanyika Desemba 12 mwaka huu ukumbi wa Diamond Jubilee (VIP), Dar es Salaam, zikiandaliwa na Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA).
 
Udhamini wa PSPF katika tuzo hizo ni Sh. Milioni tano, wakati NSSF imetoa Sh. Milioni mbili, hivyo kufanya fedha taslimu ambazo hadi sasa TASWA imepata kufikia Sh. Milioni 37.
 
Wadhamini wengine ni Kampuni ya Said Salim Bakhresa (SSB) Group Limited iliyotoa Sh. Milioni 10 na Kampuni ya Kufua Umeme ya IPTL iliyotoa Sh milioni 20.
 
Uongozi wa TASWA unaendelea na mazungumzo na kampuni mbalimbali kwa ajili ya kudhamini tuzo hizo, ambapo licha ya walioahidi kutoa fedha taslimu, lakini wapo wengine tunaendelea kuzungumza nao kwa ajili ya kudhamini kwa njia ya huduma zinazoambatana na tuzo hizo.
 
Ni imani ya TASWA kwamba hadi kufikia Novemba 20 mwaka huu kampuni na wadau mbalimbali walioahidi kutusaidia watakuwa wametekeleza ahadi zao kulingana na mazungumzo tuliyofanya nao, hivyo kuwatangaza rasmi.
 
Wanamichezo zaidi ya 100 wanatarajiwa kuwania tuzo kwa michezo mbalimbali, ambapo Kamati ya Tuzo za Wanamichezo Bora wa TASWA, inatarajiwa kukutana wiki ijayo kujiridhisha kwa mara ya mwisho orodha ya mapendekezo ya wanamichezo kutoka vyama mbalimbali vya michezo kwa ajili ya kuwania tuzo hizo.
 
B; MEDIA DAY BONAZA
TASWA kila mwaka inaandaa bonanza la vyombo vya habari linalojulikana kama Media Day Bonanza, ambalo hushirikisha wadau mbalimbali kutoka vyombo vya habari.
 
Lengo la bonanza hilo ni kuwaweka pamoja waandishi wote wa habari bila kujali ni wa siasa, michezo, uchumi, afya na mambo mengine pamoja na wafanyakazi wa vyombo mbalimbali vya habari, ili kubadilishana mawazo na kufurahi pamoja.
 
Lakini  mwaka huu bonanza hilo limechelewa kutokana na na suala la wadhamini ambao awali TASWA ilikubaliana nao, lakini baadaye walisema wamepata matatizo ya kifedha.
 
Hata hivyo kutokana na umuhimu wa bonanza hilo, uongozi wa TASWA umezungumza na wadau wengine na mazungumzo hayo yanaendelea ili Media Day Bonanza ifanyike mwezi ujao likiwa ni maalum kwa ajili ya kufunga mwaka 2014.
 
Tunajua maswali kuhusu Media Day yamekuwa mengi pengine kuliko majibu, pia wasiwasi kwa baadhi yenu ni mkubwa kuliko uhakika, lakini tunawahakikishia mambo yanaenda vizuri na ni imani yetu yanakaribia kuiva.
 
Kwa hili la Media Day, tuliona ni bora tukawie kuliko kuvurunda. Tusikimbie kwa kasi bila kutazama tuendako. Tutambae, lakini macho njiani na mbele tunakoelekea na hiyo ndiyo dhamira yetu.Chanzo:www.globalpublishers.info