Tume ya Rwanda kuchunguza makala ya BBC


Serikali ya Rwanda imetangaza tume itakayotoa tathimini kuhusu shutuma na madai dhidi ya makala ya BBC iliyorushwa kwa njia ya Televisheni mwezi Oktoba, kuhusu mauaji ya Kimbari ya mwaka 1994.

Tume ya Watu watano akiwemo mwendesha mashtaka wa zamani wa Rwanda Martin Ngoga, pia wahadhiri wawili wa masomo ya uandishi wa habari .Serikali ya nchi hiyo imewapa kazi ya kuchunguza na kutathimini Makala ya BBC iliyoitwa ‘untold Story’.

Katika Makala hayo, aliyekua mkuu wa majeshi alimshutumu Rais wa Rwanda Paul Kagame kutoa amri ya kuidungua ndege iliyokua imembeba Raisi wa nchi hiyo wakati huo Juvenal Habyarimana na mwenzake wa Burundi wakati huo,Cyprian Ntaryamira. Baadhi ya wadadisi wa mambo wanaona kuwa tukio hilo lilikua chanzo cha mauaji ya kimbari mwaka 1994.

Mamlaka nchini Rwanda iliamua kufungia matangazo ya BBC ya ukanda wa maziwa makuu kusikika nchini humo.

Tume hiyo imetoa kipindi cha miezi mitatu kutathimini makala hayo hata hivyo muda zaidi unaweza kuongezwa kabla ya Ripoti ya tume kufikia uma.

Halikadhalika vipindi vya BBC vimepigwa marufuku kurushwa kwenye Redio ya Rwanda FM na mtandao wa BBC pia umezuiliwa na Serikali.

BBC imekanusha vikali ikisema kuwa hakuna sehemu yoyote katika makala hayo inayoelezea kukataa mauaji ya kimbari dhidi ya watutsi.

Katika taarifa ya hivi karibuni BBC imesema inawajibu wa kuchunguza maswala magumu na yenye changamoto pia imesema inaamini makala hayo yametoa mchango mkubwa katika kuleta uelewa kuhusu historia ya Rwanda na ukanda mzima.pia shirika hilo limesema limekua likifanya jitihada mara kadhaa kuipata Serikali ya Rwanda lakini halikufanyikiwa.BBC (VICTOR SIMON)