Salamu Za Kuukabirisha Mwaka Mpya Wa 2013 Kutoka Kwa Dk. Shein


 

 
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi. Dk Ali Mohamed Shein,akitoa salamu za kuukaribisha Mwaka mpya wa 2013,kwa wananchi wa Zanzibar na Watanzania wote kwa ujumla,pia aliwasihi wananchi kuendela kushirikiana   na Serikali yao katika kuendeleza mipando mbali mbali ya maendeleo,na kuwataka kuwa walinzi wa rasilimali pia kuzingatia   taratibu za kisheria, kwa kuwa na elimu bora ya rasilimali hizo. 
 
 [Picha na Ramadhan Othman,Ikulu.]

Lissu asema Profesa Shivji amepotoka kuponda kesi ya Lema


 

Fredy Azzah

HATUA ya mwanazuoni wa siku nyingi nchini, Profesa Issa Shivji kupinga hukumu ya Mahakama ya Rufani Tanzania iliyomrejeshea ubunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema imemtia matatani na baadhi ya watu wanasema gwiji huyo wa sheria “huenda amenukuliwa vibaya au hajasoma hukumu husika.”

 

Jana Wakili wa Lema, Tundu Lissu, alimkosoa Profesa Shivji pamoja na Rais wa Chama cha Wanasheria wa Tanganyika, Francis Stolla akisema wanasheria hao wamepotoka katika matamshi yao ya kupinga hukumu ya Mahakama ya Rufani.

 

 

TAMKO RASMI LA BAVICHA MKOA WA TANGA KUHUSU KATIBU WA BAVICHA MKOANI WA TANGA BW DEOGRATIAS KISANDU


 
NAPENDA kutoa taarifa kwa umma kutokana na habari zinazoandikwa kwenye  baadhi ya vyombo vya habari, huku chanzo cha habari hizo kikiwa ni Katibu  wa BAVICHA Mkoa wa Tanga, Bwana Deogratias Kisandu, ambazo zimekuwa  zikionesha kuwa vijana wa Mkoa wa Tanga tuna walakini katika chama chetu  cha CHADEMA. 
 
Leo katika baadhi ya vyombo vya habari, Bwana Kisandu amenukuliwa akitoa  taarifa kuwa yeye pamoja na makatibu wenzake nchi nzima, wamepanga kufanya  maandamano ya kuupinga uongozi wa juu wa kitaifa wa BAVICHA. 
 
Kwa kutambua na kuheshimu kuwa moja ya misingi muhimu ya uendeshaji wa  Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) pamoja na mabaraza yake ni  vikao, ambavyo vipo kwa mujibu wa Katiba, miongozo, taratibu, kanuni na  itifaki za chama, vijana wa CHADEMA Mkoa wa Tanga, ambao mimi ndiye msemaji  wao kikatiba, tunaamini Bwana Kisandu anazidi kupotoka. 
 
 
Kwa hiyo basi, kama ambavyo nimeshapokea malalamiko kutoka kwa vijana wa  Tanga baada ya hatua yake ya awali ya Bwana Kisandu kutoa taarifa kwa  vyombo vya habari, bila kuzingatia katiba, maadili na itifaki ya chama,  akibeba propaganda nyepesi za Sekretarieti ya CCM, juu ya suala la kadi  mbili kwa Katibu Mkuu wetu Dkt. Willibrod Slaa, kuna haja ya kufanya vikao  kuangalia na kujadili mwenendo wa kiongozi mwenzetu huyo. 
 
Kwa sababu kama vijana makini wa CHADEMA, chama ambacho kinaamini katika  kutoa utumishi bora, mikakati madhubuti, sera imara kwa ajili ya maendeleo  endelevu ya Watanzania wote, ambao wamekosa uongozi bora na siasa safi  kutokana na ufisadi na ubadhirifu wa CCM, lazima tuwe makini na kila  mwenzetu yeyote yule ambaye anaonekana kufanya kazi ya CCM kwa kutumia jina  la CHADEMA. 
 
Tunapenda kumkumbusha Bwana Kisandu kuwa atumie muda wake pia kuisoma vyema
katiba ya CHADEMA hasa katika Sura ya 10 inayozungumzia Maadili ya  Viongozi, Sifa mahususi za viongozi na maadili ya wanachama, kifungu
10.1(1-13), toleo la mwaka 2006. 
 
Kuhusu masuala ya ushiriki wa vijana kwenye shughuli mbalimbali za chama  ikiwemo mikutano ya M4C, Bwana Kisandu anapaswa kuelewa kuwa vijana  kutokana maeneo mbalimbali ya nchi, ukiwemo Mkoa wa Tanga tumekuwa  tukishirikishwa, kupitia utaratibu maalum unaopangwa na Ofisi ya Katibu  Mkuu, ambao tunaamini mpaka sasa umetoa fursa kwa wanachama wote, wakiwemo  wazee, wanawake na vijana kukieneza na kukiimarisha chama maeneo mbalimbali  ya nchi. 
 
Na maamuzi yote ya msingi kwa uendeshaji wa Baraza hasa kwa Mkoa wa Tanga  yatafanyika kupitia vikao na hatua zitachukuliwa kwa kufuata katiba,  kanuni, maadili, itifaki na miongozo ya chama. 
 
 *Aron J Mashuve* 
*Mwenyekiti wa BAVICHA* 
*Mkoa Wa Tanga*

Kituo cha Mabasi yaendayo mikoani na nje ya nchi (UBT) kuhama januari 2013


 

MCHAKATO wa kuhamisha Kituo cha Mabasi yaendayo mikoani na nje ya nchi (UBT), kwenda Mbezi Luis unatarajiwa kuanza Januari 15 mwaka ujao.
 

Akizungumzana wandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Mkurugenzi wa Jiji Mussa Zungiza, alisema lengo la kuhamisha kituo hicho ni kwa ajili ya kupisha Mradi wa Mabasi yaendayo Haraka (DART).

 
Alisema kuhamishwa kwa kituo hicho kutakuwa kwa awamu, kutakakokwenda sambamba na kukamilika kwa ujenzi wa kituo hicho cha Mbezi.
 
“Siyo kweli kama ifikapo Januari tunahamisha au tunasimamisha shughuli zote pale Ubungo la hasha, tutakacho fanya pale tutawakabidhi wajenzi wa mradi huo wa DART ambao nao watachagua maeneo maalumu ya kuanzia shughuli zao, huku maeneo mengine yakiendelea kutoa huduma bila ya kuleta athari katika utoaji huduma”alisema Zungiza.
 
Zungiza alisema hadi sasa pale Mbezi kinachofanyika usafishaji wa eneo hilo la stendi hiyo mpya.
 
Alisema katika awamu hiyo ya kwanza watejenga miundombinu ikiwemo uzio, alama za kuelekeza magari, njia za kuingia na kutoka.
 
“Pengine tunatarajia ndani ya miezi mitano tunaamini awamu yakwanza itakuwa imekamilika”alisema.
 

Zungiza alisema uhamishaji kabisa wa kituo hicho cha Ubungo kutategemea kukamilika kwa ujenzi wa kituo hicho kipya cha Mbezi. Chanzo:fullshangweblog

TAARIFA KWA UMMA JUU YA MAAMUZI YA BARAZA LA MADAKTARI KUHUSU MADAKTARI WALIOGOMA


 Kutokana na mgomo wa madaktari uliotokea kati ya tarehe 23 na 29 mwezi juni 2012.Wizara iliwasilisha malalamiko kwenye Baraza la madaktari Tanganyika ili lifanye uchunguzi kuhusu madaktari hao .Idadi ya madaktari wote waliogoma walikuwa 394, kati yao madaktari 376 walikuwa ni madaktari walio katika mafunzo kwa vitendo (Interns) kutoka hospitali za Muhimbili, K.C.M.C. Bugando, Mbeya Rufaa, St.Francis – Ifakara, Dodoma, Temeke, Mwananyamala, Amana, Haydom na Sekou Toure. Aidha, Madaktari waajiriwa(Registrar) 18 walishiriki katika mgomo huo kutoka hospitali ya Rufaa ya Mbeya.

Baraza lilipitia malalamiko yote na limetoa adhabu stahiki kwa kila daktari aliyethibitishwa kushiriki katika mgomo huo.  Adhabu hizo zilikuwa katika makundi yafuatayo; onyo, onyo kali na kusimamishwa udaktari kwa muda wa kati ya mwezi mmoja na miezi sita.Vile vile kuna Madaktari ambao hawakuwa na hatia ya kushiriki katika mgomo na hivyo walifutiwa mashtaka.

MCHANGANUO WA ADHABU

  • Waliofutiwa mashitaka madaktari 49
  • Waliopewa onyo  madaktari 223
  • Waliopewa onyo kali madaktari 66
  • Kusimamishwa kwa muda madaktari 30
  • Mashitaka yaliyoahirishwa kutokana na wahusika kuhitaji ushauri wa kisheria madaktari 4
  • Mashitaka yasiyosikilizwa kutokana na wahusika kutofika walipoitwa na Baraza madaktari 22

Wizara inakamilisha taratibu za kinidhamu kwa mujibu wa Kanuni za Utumishi wa Umma kwa Madaktari wote waajiriwa ambao walipatikana na hatia mbele ya Baraza la Madaktari.   Wizara pia imeridhia kuwapa Madaktari waliokuwa katika mafunzo kwa vitendo fursa nyingine ya kuendelea na mafunzo hayo katika hospitali za Umma walizokuwepo kabla ya kuondolewa. Hata hivyo fursa hii haitawahusu Madaktari wote waliopewa adhabu za kusimamishwa na Baraza la Madaktari, hadi hapo watakapomaliza kutumikia adhabu zao.

HITIMISHO

Kwa taarifa hii madaktari wote waliofutiwa mashtaka na wale waliopewa onyo na onyo kali wanatakiwa kuwasilisha kwa Katibu Mkuu Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii barua kutoka kwa msajili wa Baraza la Madaktari ikithibitisha kurejeshewa usajili  na kuruhusiwa kuendelea na mafunzo kwa vitendo. Vile vile madaktari waajiriwa(Registrar) wanatakiwa pia kuripoti kwa Katibu Mkuu Wizara ya Afya ili kupewa barua zao kulingana na Adhabu walizopewa.  Barua hizi zitatolewa kuanzia tarehe 2 Januari, 2013.Madaktari wote walio katika mafunzo kwa vitendo wanatakiwa kuanza kazi katika vituo vyao vya awali ifikapo tarehe 14 Januari, 2013.Hakuna muda utakaoongezwa kwa kipindi kilichobakia cha mafunzo kwa vitendo. Kwa wale wote waliopewa adhabu wataanza kutumikia adhabu hizo kuanzia tarehe ya adhabu hiyo ilivyotolewa.

 

Nsachris Mwamwaja

Msemaji

WIZARA YA AFYA NA USTAWI  WA JAMII

27/12/2012

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri ya Singida alumbana na diwani wa viti maalum (CCM) kuhusiana na ripoti ya Sikika.


Dk.Henry Mmbando,wa ofisi ya mganga mkuu wa halmashauri ya wilaya ya Singida akitoa ufafanuzi juu ya tuhuma zilizotolewa na shirika la Sikika juu ya uwajibikaji katika kutoa huduma katika halmashauri hiyo.(Picha na Nathaniel Limu).

 

 Mwanakamati wa shirika lisilo la kiserikali la Sikika, diwani (CCM) Salima Kundya akimtuhumu diwani wa mkutano huo diwani Elia Digha (hayupo pichani) kwa kauli yake kuwa kamati ya Sikika haijui kitu chochote kuhusu na utoaji wa huduma ya afya katika halmashauri ya wilaya ya Singida. Salima alikuwa akitoa tuhuma hizo mbele ya mkutano wa mrejesho wa taarifa ya uwajibikaji katika utoaji wa huduma za afya iliyokuwa ikitolewa na shirika la Sikika.

Na Nathaniel Limu.

Halmashauri ya wilaya ya Singida imesema haitakubali kuchonganishwa na wananchi wake na vyombo au taasisi yakiwemo mashirika yasiyo ya kiserikali (NGOs), kwa kutoa taarifa zisizofanyiwa utafiti wa kina.

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo Alli Juma, amesema hayo muda mfupi kabla ya mkutano wa mrejesho wa ripoti/taarifa ya shirika lisilo la kiserikali la Sikika lenye makazi yake jijini Dar-es-salaam, iliyohusu ufuatiliaji wa uwajibikaji katika utoaji wa huduma za afya, haujafungwa rasmi.

Amesema taarifa iliyotolewa na shirika la Sikika, kwa kiasi kikubwa haikufanyiwa utafiti wa kina, kitendo ambacho kinaweza kusababisha halmashauri kutokuelewana vizuri na wananchi wake.

Alli ambaye ni Afisa Utumishi amesema Sikika hawakuwa na mawasiliano wala ushirikiano mzuri na wakuu wa idara katika kupata ukweli wa taarifa mbalimbali walizokuwa wanazikusanya.

“Mimi niwaombeni tu ndugu zangu wa Sikika, fanyeni kazi kwa kufuata sheria, kanuni na taratibu, halafu mkiandika mabaya, upande wa pili andikeni pia mazuri hata kama yapo machahe”,alisema Alli.

Mkutano huo uliokuwa chini ya uenyekiti wa diwani (CCM) Elia Digha, Mwenyekiti huyo alitoa shutuma nzito kwamba wafanyakazi wa Sikika na kamati nzima iliyofuatilia uwajibikaji wa huduma za afya, haijui lolote.

“Mimi nasema timu yote iliyoleta taarifa hii, haijui lolote, naomba siku za usoni tushirikiane vizuri katika kufuatilia uwajibikaji katika sekta zote, kutoa taarifa za jumla jumla kama hii, mtaacha watu waichukie bure serikali”, alisema Digha ambaye ni diwani wa kata ya Msange jimbo la Singida Kaskazini.

Baada ya maneno hayo mazito, diwani wa viti maalum (CCM) Salima Kundya, aliyeshiriki na Sikika kufuatilia uwajibikaji katika sekta ya afya, alimtolea uvivu Mwenyekiti Digha, kuwa lengo lake ni kutaka kuficha ukweli uliopo kwenye taarifa hiyo.

“Kama sisi madiwani wawili wa CCM mliotuchagua tukashirikiane na Sikika na tukabaini yote yaliyopo kwenye taarifa ya Sikika kuwa ni ya ukweli mtupu, halafu wewe unasema hatujui lo lote, basi wewe mwenyekiti Digha na madiwani wote wa CCM walioshiriki kutachagua na ninyi wote hamjui kitu au cho chote kinachofanyika ndani ya halmashauri hii”, alisema Salima huku uso wake ukionyesha kujawa na hasira.

Baada ya maneno hayo ya diwani Salima, bila kulazimishwa, Digha ambaye pia ni msaidizi wa mbunge wa jimbo la Singida kaskazini Lazaro Nyalandu, alisimama na kuomba radhi kwa matamshi yake ambayo yalilenga kuidhalilisha kamati iliyoambatana na Sikika.

Katika mengi yaliyomo kwenye taarifa ya Sikika, kuna hoja iliyotolewa na mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali, inaonyesha kuwa halmashauri hiyo ilikuwa na shilingi bilioni 1,686,561,960 za miradi mbalimbali ya maendeleo.

Lakini taarifa hiyo, ilionyesha kiasi cha shilingi bilioni 1.6 sawa na aslimia 61.4,hazikutumika kwa wakati, kitendo hicho kinamaanisha kuwa baadhi ya miradi ya maendeleo, ilikamilika nusu ama haijakamilika kabisa.chanzo:moeblog