Urais CCM kazi pevu


Dar es Salaam. Wakati joto la urais ndani ya CCM likiendelea kupamba moto, watu watakaoingia kundi la tano bora ambalo litapitishwa na Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM (NEC), wamefahamika.
Waziri Mkuu wa zamani Edward Lowassa.PICHA|MAKTABA

Uchambuzi uliofanywa na makada mbalimbali wa chama hicho unaonyesha kuwa makundi hayo ambayo yatatoa wagombea mmoja, ni kundi la wagombea vijana, kundi la kifo, kundi la waziri mkuu aliyepo madarakani, wagombea wanawake na kundi la wagombea kutoka Zanzibar.

Kila kundi katika hayo litatoa mgombea mmoja ambaye jina lake litapelekwa kupitishwa kwenye mkutano wa NEC kupitishwa kabla ya kupigiwa kura kwenye Mkutano Mkuu wa CCM (CC).
Kundi la Vijana
Uchambuzi unaonyesha kwa vyovyote vile CCM lazima iteue jina la mgombea kijana hata kama watakuwa hawamtaki ili kuonyesha kuwa chama hicho kimekomaa na kinawapa moyo vijana kuwania nafasi za uongozi.
Wanasiasa vijana wa CCM ambao tayari wametangaza nia ya kuwania nafasi ya urais ni Naibu Waziri wa Sayansi na Teknolojia, January Makamba na Mbunge wa Nzega, Dk Hamis Kigwangalla.
Wengine ambao wamekuwa wakitajwa katika kundi hilo ni Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, Mbunge wa Songea Mjini, Dk Emmanuel Nchimbi, Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba na Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja.