Ikulu yaguswa kwenye ujangili


 

Ikulu yaguswa kwenye ujangili MIEZI tisa tangu mwandishi wa Uingereza, Martin Fletcher wa gazeti la The Mail on Sunday, kuchapisha makala akidai Serikali ya Tanzania inabariki ujangili wa meno ya tembo, gazeti la New York Times la Marekani, nalo limechapisha habari ikihusisha ndege ya Rais wa China, Xi Jinjing kuhusika kubeba pembe za ndovu alipokuwa Tanzania. Katika toleo la Novemba 5 mwaka huu, mwandishi wa New York Times, Dan Levin alinukuu ripoti ya Shirika la ujasusi la mazingira lenye makao yake mjini London, akisema kwamba China ilinunua maelfu ya kilo za pembe za ndovu na kuzitorosha kwa kutumia ndege ya Rais huyo wakati alipozuru Tanzania Machi 2013. Machi 2013, Rais wa China, Xi Jinping, aliwasili Tanzania katika ziara yake ya kwanza kwenye Bara la Afrika akiwa ni kiongozi wa nchi ambayo ni ya pili kiuchumi duniani. Katika ziara hiyo aliambatana na ujumbe wa maofisa wa serikali na wafanyabiashara ambao walikuwa maalum kwa ajili ya kukuza mahusiano baina ya nchi hizo mbili. Kwa mujibu wa mwandishi huyo, ripoti mpya ya shirika la ujasusi la mazingira inaonesha kuwa ujumbe wa Rais Jinping ulitumia ziara hiyo kama nafasi ya kufanya biashara haramu ya pembe za ndovu kwa kupandisha bei yake mara mbili kufikia dola 70,000 za Marekani kwa kilo, au dola 31,800 kwa kila paundi. Kwamba, wiki mbili kabla ya Rais Jinping kuwasili, wanunuzi wa Kichina walikwenda kwenye maeneo mbalimbali yanayojihusisha na biashara hiyo na kununua maelfu ya pembe hizo ambazo baadaye zilipelekwa China kwa kutumia mabegi ya wanadiplomasia kwenye ndege ya Rais. “Rais wenu alikuwa hapa,” ananukuliwa Suleiman Mochiwa, Mtanzania anayedaiwa kujihusisha na biashara hiyo haramu ya pembe za ndovu, akimaanisha Rais Jinping. “Akiwa hapa, kilo nyingi zimekwenda nje kwenye ndege pasipo ulinzi. Walinunua kutoka kwetu.” Ripoti hiyo inaitaja Tanzania kama chanzo kikuu duniani kwa uharamia wa pembe za ndovu na kwamba, China imekuwa mnunuzi mkubwa wa bidhaa hizo kimagendo. Read more »