Sitta: Taifa Lina Viongozi Wenye Sura Mbili


Sitta: Taifa Lina Viongozi Wenye Sura Mbili

Tumaini Msowoya, Iringa
WAZIRI wa Ushirikiano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Samwel Sitta amesema taifa linakabiliwa na viongozi wenye sura mbili ambao ni wale wasio waadilifu wanaofikiri kwa kutumia matumbo kwa kujilimbikizia mali na viongozi wachache wanaofikiri kwa ajili ya kuwatumikia wananchi.

Sitta alisema hayo alipokuwa akitoa mada katika katika maadhimisho ya Siku ya Sheria kwa wanafunzi wa vyuo vikuu nchini, alipozungumza na Jumuiya ya Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Tumaini, mjini Iringa (IUCo) jana.

Mada hiyo ilihusu mbinu za kisheria na utoaji wa huduma za kisheria Tanzania, ambapo Sitta alisema matatizo ambayo yanayolikabili taifa yanatokana na sura za viongozi wanaoliongoza.

Akifafanua, alisema wapo baadhi ya viongozi wabinafsi na wasio waadilifu ambao mara zote wamekuwa wakifikiri namna ya kujilimbikizia mali badala ya kuwatumikia watanzania.

“Msishangae, tuna viongozi wenye sura mbili, wapo wanaofikiri kwa kutumia matumbo yao jinsi ambavyo wataneemeka na kujinufaisha wenyewe, hawa ni wale wabinafsi lakini wapo viongozi ambao wanatumia ubongo katika kufikiri jinsi ambavyo watatumia uwezo wao wote katika kuwatumikia wananchi, mimi ni miongoni mwa hawa,” alisema Sitta.

Alisema taifa lina kazi kubwa ya kufikiri jinsi ya kumpata Rais katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, kwa madai kuwa ana kazi kubwa ya kuliondoa taifa mahali ambako limefikia kwa sasa sambamba na kuvunja makundi yote yaliyopo.

Alidai kuwa imefika wakati ambao lazima viongozi waweke bayana mali wanazomiliki ili wananchi wazitambue na kuwapima viongozi hao kulingana na kipato chao.

Aliongeza kuwa viongozi wengi wamesahau falsafa ya ‘Utu na Usawa’ iliyoanzishwa na hayati Mwalimu Julius Nyerere wakati wa uhai wake, jambo ambalo limesababisha kuwepo kwa tabaka kubwa miongoni mwa jamii.

Alisema wakati akiwa Spika wa Bunge la Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, anajivunia jinsi ambavyo Bunge hilo liligeuka la wananchi na kuwajibika pale lilipotakiwa kufanya hivyo.

Kuhusu azimio la Arusha, Sitta alisema kuwa lilikuwa na umuhimu wake kwani lilionyesha namna kiongozi anapaswa kuwajibika, kwa ajili ya kuwatumikia wananchi.

Akizungumzia Jumuiya ya Afrika Mashariki, Sitta aliwataka watanzania kuondoa hofu juu ya kuwepo kwa soko la pamoja la jumuiya hiyo kwa madai kuwa tayari yameandaliwa mazingira mazuri ambayo yatawawezesha wananchi kuwepo katika soko hilo bila wasiwasi.

Alisema wapo katika majadiliano juu ya kuanzishwa kwa shirikisho la kisiasa ambapo tayari baadhi ya wanasheria wameajiriwa kwa ajili ya kushughulikia jambo hilo.

Aidha aliwataka vijana kujiamini na kutoogopa kuomba kazi katika nchi yoyote ndani ya jumuiya hiyo, badala ya kuendelea kunung’unika juu ya kukosekana kwa ajira.

Kwa upande wake, Mkuu wa Kitivo cha Sayansi ya Jamii, Profesa Seth Nyagawa alisema njia pekee ya kuwakomboa watanzania katika umaskini ni kuwanoa ili waweze kuingia kiuhakika katika soko la pamoja la Afrika Mashariki, ikiwemo kuwaandaa kielimu.

Awali, mmoja wa wakufunzi wa Sheria chuoni hapo, Edward Nduguru alisema matatizo mengi yanayowakabili watanzania kwa sasa yanaweza kumalizwa na watanzania wenyewe pale watakaposhirikishwa katika maamuzi huku akiishauri Tume ya Katiba mpya kuhakikisha inakusanya maoni kwa makundi yote.
Chanzo: Mwananchi

Vigogo Uhamiaji wana utajiri wa kutisha


 

TUME YA KUWACHUNGUZA YAANZA KAZI LEO, WAHAMISHIWA MIKOANI KIAINA
Mwandishi WetuKASHFA nyingine imeibuliwa katika Idara ya Uhamiaji.Taarifa mpya yenye kurasa tano, imewataja vigogo hao saba wakidaiwa kuwa na utajiri wa kutisha.Taarifa hiyo ambayo tunayo nakala yake, imedai kuwa vigogo hao wanamiliki mali na mamilioni ya shilingi katika akaunti zao binafsi.

Maofisa saba wametajwa kwa majina na vituo vyao vya kazi ambavyo ni Lindi, Dar es Salaam, Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (Kia) na Moshi.
Tuhuma hizo zimekuja wakati Tume Maalumu iliyoundwa kuchunguza tuhuma za ufisadi na utoaji wa vibali bandia kwa wageni, ikitajwa kuanza kazi juzi. Hata hivyo, habari kutoka wizarani zinaeleza kuwa timu hiyo itaanza rasmi kazi zake leo.
Habari za uhakika kutoka ndani ya Uhamiaji, zimedai kuwa baadhi ya wajumbe wa tume hiyo wamemhoji meneja wa benki moja kubwa ya Moshi ili kupata ukweli wa madai kuwa kigogo mmoja wa Uhamiaji mwenye cheo cha Naibu Kamishna (DCI), anamiliki akaunti ya fedha za kigeni.
Kigogo huyo anahusishwa pia na mtandao wa utoaji vibali bandia kwa raia wa kigeni wanaofanya kazi mkoani Kilimanjaro au kufanya kazi za kujitolea.
Ripoti hiyo imetaja taasisi 13, zikiwamo zisizo za kiserikali (NGO), hospitali na hoteli za kitalii zinazodaiwa wageni wake walipewa vibali bandia.
Mbali na kumhoji meneja huyo, inadaiwa pia walifanya mahojiano na uongozi wa kiwanda kimoja kinachodaiwa kukutwa na vibali bandia vya wageni 84.
Taarifa hizo zilidai kuwa maofisa wengine waandamizi wa Uhamiaji kutoka Makao Makuu, Dar es Salaam walitarajiwa kuwasili Moshi juzi kuungana na wenzao.