MBOWE ACHACHAMAA



freeman-mbowe-chadema
http://chademablog.blogspot.com/

Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe, ameonya kuwa iwapo kiongozi yeyote wa chama hicho ataruhusu mgombea wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wa ngazi yoyote ya uongozi katika uchaguzi, kupita bila kupingwa katika eneo lake, atawajibika.

Alitoa onyo hilo alipokuwa akifungua Mkutano Mkuu wa Bavicha, jijini Dar es Salaam jana.

“Misiruhusu uongozi, kuanzia serikali ya mtaa kupita bila kupingwa. Ikitokea hivyo, na wewe kiongozi (wa Chadema) jiandae kuwajibika,” alisema Mbowe.

Aliutaka uongozi mpya wa Bavicha utakaochaguliwa kuendeleza kazi nzuri iliyoachwa na uongozi wa baraza hilo uliopita.

Kazi hizo ni pamoja na namna ya kuwaandaa vijana, wazee na wanawake, kujiandikisha kwenye daftari la kudumu la wapigakura na kushiriki chaguzi zote, kuanzia ule wa serikali za mitaa, vijiji na vitongoji, udiwani, ubunge na urais mwakani.

Mbowe, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) alisema muda mwafaka ukifika, watakutana na viongozi wenzake wa vyama vinavyounda umoja huo vya CUF na NCCR-Mageuzi kuangalia namna watakavyofanya kazi pamoja katika chaguzi zijazo.

Alisema kifungu cha 6 (3) na (4) cha katiba ya Chadema kinaelezea ukomo wa uongozi, hivyo akasema wana kazi kubwa ya kupanua wigo wa chama.
Kwa kuzingatia hilo, alisema watakuwa na kazi ya kutathmini utendaji wa kila kiongozi katika chama kila baada ya miezi sita kuona namna alivyochangia kukuza na kukiimarisha chama.

“Kiongozi atakayeruhusu katika eneo lake chama kisikue, atawajibika kabla ya miaka mitano,” alisema Mbowe.

Alisema Chadema siyo ya fujo, bali ni chama chenye dhamira ya kweli, hivyo akaonya kuwa iwapo mwanachama wake yeyote anayegombea uongozi kwa kutumia mbinu chafu, ikiwamo rushwa, atang’olewa hata kama atakuwa amekwishakupitishwa katika uchaguzi.

Awali, akimkaribisha Mbowe kufungua mkutano huo, Mwenyekiti wa Bavicha anayemaliza muda wake, John Heche, alisema Chadema imekua na kwamba, kigezo cha hilo ni namna ilivyofanikiwa kufanya kwa mara ya kwanza uchaguzi, kuanzia ngazi za msingi.

Aliushukuru uongozi wa Chadema kwa kuwashughulikia wasaliti ndani ya chama na kusema kamwe vijana hawatavumilia kuona mtu yeyote anakivuruga chama hicho.

Mapema, Katibu Mkuu wa Bavicha anayemaliza muda wake, Deogratius Munishi, alisema wajumbe waliotakiwa kuhudhuria ni 336 na kwamba, hadi kufikia saa 5.40 asubuhi, waliosajiliwa walikuwa 301 sawa na asilimia 89 ya akidi ya wajumbe wote wa mkutano huo.

RAIS KIKWETE HAWEZI KUAHIRISHA BUNGE


Mjumbe wa Bunge Maalum la Katiba, ambaye ni  Mwenyekiti wa Kituo cha Demokrasia Tanzania(TCD)Mhe. John Cheyo amesema kwamba mchakato mzima wa Katiba utamalizwa kwa kura ya maoni ya wananchi, hivyo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.Dkt. Jakaya  Kikwete haiwezi kutamka leo kuliahirisha Bunge Maalum la Katiba kwa kuwa liko Kisheria.
Aidha Mhe. Cheyo alisema kilichoahirishwa ni mchakato wa kura ya maoni ya wananchi na si Bunge hilo kwa kuwa walikubaliana   katika kikao cha mashauriano, baina Rais Kikwete na  Viongozi  Wakuu wa Vyama vya Siasa vyenye wabunge vinavyounda TCD kuwa bunge hilo liendelee.
Kauli hiyo imetolewa leo Bunge Mjini Dodoma na Mhe. Cheyo wakati wa mjadala wa kujadili sura zilizobakia za Rasimu ya Katiba Mpya, ambapo alisema hayo ndiyo makubaliano yaliyofikiwa.
 Aidha Mhe. Cheyo alisisitiza Katiba Mpya inayopendekezwa itakayopatikana itadumu kwa njia ya maridhiano.
“ Bunge hili linaendeshwa kwa mujibu wa sheria , Tangazo la  Serikali (Government Notice) Na 254 hili ndilo uhai wa Bunge hili hadi Oktoba 4, mwaka 2014, na wote tukakubaliana haiwezekani   Mhe. Rais akasema   leo Bunge likasitishwa.
“ Vitu viwili vikukutana  kwa nia ya maridhiano, vitu vingine vinaweza kuwekwa pembeni sawa na sasa na baadae vinaweza vinashughulikiwa kwa wakati huo,” alisema Mhe. Cheyo.
Mhe. Cheyo alisema anamwomba  Rais Kikwete atoe ruhusa ya kuwepo kwa kipindi maalum  cha kitakachorushwa na televisheni (video) ili kila mtu aonekana alichokisema, huku akionesha kusikitishwa na upotoshwaji wa makubaliano hayo, uliofanywa na baadhi ya wanasiasa.
 “ Mojawapo  ambayo tuliyokubaliana  Bunge hili lipate Katiba ambayo inapendekezwa na wananchi pia kwa hali tulinayo haiwezekani  mchakato mzima ukamalizika, mchakato utamalizika kwa kura ya maoni  ya wananchi. Kama tukifika  huko itabidi tuhairishe uchaguzi wa mwaka 2015.   Niliyoyasema  ndiyo makubaliano tuliyokubaliana,” alisisitiza.
Mhe. Cheyo alisema Rais Kikwete alikubali kukaa chini pamoja na TCD na hao wanaojiita Ukawa.
 Alisema  Rais Kikwete alifanya mazungumzo na  viongozi wa Vyama vya Siasa vyenye wabunge vinavyounda TCD  mara  kwa mara ya kwanza, Agosti 31, mwaka 2014 kwa saa nne na mara ya pili, Septemba 8, mwaka 2014 kwa  saa mbili.
Kikao hicho cha mashauriano kilihusisha  kamati ya makatibu wakuu,  kamati ya wenyeviti wa vyama  vya CCM, CHADEMA,CUF na NCCR-  Mageuzi.
(Awadh Ibrahim)