Urais Chadema moto 2015 …


[Katibu Mkuu wa chadema, Dk Willibroad Slaa ] Katibu Mkuu wa chadema, Dk Willibroad Slaa
Dk Slaa, Mbowe, Zitto hapatoshi
Mwandishi wetu
FUKUTO la Urais mwaka 2015 ndani ya vyama vya siasa linazidi kupamba moto, huku majina ya makada wanaowania nafasi hiyo kupitia chama kikuu cha upinzani nchini Chadema, yakianza kuanikwa.

Ikiwa imebaki takribani miaka mitatu kabla ya kufanyika Uchaguzi Mkuu wa Rais mwaka 2015, makada mbalimbali ndani ya vyama, wameanza kupigana vikumbo kila mmoja kujaribu kujipanga ili achaguliwe kupeperusha bendera ya chama chake kwenye uchaguzi huo. Ndani ya chama tawala CCM, taarifa zinadai kuwa baadhi ya wanasiasa wameanza kuunda mitandao huku wengine wakilaumiwa kuanza ‘kucheza rafu’ kwa kumwaga mamilioni ya fedha kwa lengo la kutekeleza mkakati huo.Tayari hatua hiyo imelaumiwa na baadhi ya makada ndani ya chama hicho kikongwe nchini huku wengine wakionya kuwa mbio za Urais mwaka 2015, zinatishia kuisambaratisha CCM.

Wakati heka heka hizo zikiendelea ndani ya CCM, habari kutoka ndani ya Chadema, zimetaja baadhi ya majina ya makada wa chama hicho, wanaopewa nafasi kubwa kugombea urais kwa tiketi ya chama hicho mwaka 2015.

Habari zilizopatikana kutoka ndani ya Chadema, zimewataja watu hao kuwa ni Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe, Katibu Mkuu wa Chadema ambaye pia aligombea urais kupitia chama hicho kwenye uchaguzi uliopita, Dk Willibroad Slaa na Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho, Zitto Kabwe.

Ingawa Zitto tayari ameweka wazi kuwa hatagombea kutokana na umri wake kuwa chini ya ule unaotambuliwa kikatiba kwa nafasi hiyo, bado ana matumaini kwamba kipengele hicho kinaweza kubadilishwa ndani ya katiba mpya.

Kwa mujibu wa katiba ya sasa, mtu anayewania Urais wa Jamhuri ya Muungano lazima awe na umri kuanzia miaka 40 na kuendelea. Mwaka 2015 Zitto atakuwa hajafikisha umri huo na ‘atanusurika’ endapo tu katiba mpya itapunguza umri huo.

Chanzo chetu kimeeleza kuwa picha halisi ya atakayewania nafasi ya urais kupitia chama hicho itadhihirika baada ya kukamilika kwa chaguzi za ngazi zote ndani ya chama hicho baadaye mwaka huu.

Mazingira mengine ambayo yanaweza kuathiri ama kuamua juu ya mgombea urais wa chama hichona kujiunga kwa wanachama wapya husasan kama baadhi ya vigogo watajiengua CCM na kuamua kujiunga na chama hicho.

Hofu ya makada wa CCM kutimkia Chadema inatokana na kundi kubwa la wanasiasa ndani ya chama hicho kutaka nafasi hiyo, hali itakayowafanya wengine kwenda vyama vingine kujaribu bahati zao.

Kutokana na idadi kubwa ya wanaCCM wanaotaka nafasi hiyo, baadhi ya watu wanadaiwa kuunda mitandao yenye malengo ya kuchafuana

CCM katika kikao chake cha Halmashuari Kuu (NEC) kilichoketi mjini Dodoma Novemba mwaka jana, kilikiri kuwa mvutano mkubwa wa makundi uliopo ndani ya chama hicho, chanzo chake ni Urais wa mwaka 2015.

Kwa upande wa Chadema, ingawa bado hakuna vita ya wazi wazi kama ilivyo ndani ya CCM, wanachama wake wameaanza kuzungumzia na kujipanga kwa ajili ya uchaguzi huo.

Dk Slaa ambaye aligombea katika uchaguzi uliopita na kuibuka mshindi wa pili baada ya kupata asilimia 26 ya kura zote zilizopigwa, ndiye anayeonekana kupewa nafasi kubwa. Mwanasiasa huyo anaonekana kuwa bado anafaa kuwania tena nafasi hiyo kutokana na rekodi nzuri kwenye uchaguzi uliopita.

Katika uchaguzi huo, Dk Slaa alionesha kuyaelewa vyema matatizo ya Watanzania na kujaribu kueleza nini kifanyike kuondokana nayo, hali iliyowafanya wananchi wengi kuwa na imani naye.

Mbowe (50) ambaye aliwania kiti cha urais mwaka 2005 na kushika nafasi ya tatu, anatajwa kuwa anaweza kuwania tena nafasi kutokana na rekodi yake safi ya kukiimarisha chama hicho kunzia tangu kikiwa kichanga hadi kukiwezesha kuwa chama kikuu cha upinzani nchini.

Wanachama wengine wa chama hicho wanaotajwa kuwania nafasi hiyo ni pamojan na John Shibuda ambaye mwaka juzi alichukua fomu za kuomba kuwania urais kupitia chama CCM, lakini baadaye alijitoa na kumuunga mkono mgombea wa chama hicho, Rais Kikwete.

Wengine ni Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu, Mbunge wa Ubungo, John Mnyika, Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi maarufu Sugu na Mbunge wa Nyamagana, Ezekiel Wenje na Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema.

Hata hivyo Lema ambaye ametajwa kuwa mbunge bora kwenye moja ya mitandao ya kijamii nchini, aliliambia Mwananchi Jumapili juwa hana nia ya kuwania urais kupitia chama hicho mwaka 2015.

Alisema pamoja na kupata kura nyingi za watu waliomuunga mkono kwenye mtandao huo, alisema hatarajii kugombea nafasi hiyo ya urais ila akasisitiza kuwa ataweka nguvu zaidi kwenye ubunge.”Nashukuru kwa kupata kura hizo, lakini sitarajii kuwania nafasi hiyo… Atakayeteuliwa na chama changu nitamuunga mkono,” alisema.

Urais na migogoro
Imeelezwa kuwa migogoro mingi inayovikumba vyama vya siasa vikiwemo NCCR -Mageuzi na CUF inachangiwa kwa kiasi kikubwa na mbio za Urais mwaka 2015.

Tayari NCCR- Mageuzi na imetangaza kumvua uanachama Mbunge wa Jimbo la Kigoma Kusini David Kafulila na wanachama wengine 11 huku CUF kikimfukuza Mbunge wa Wawi, Hamad Rashid Mohamed na wenzake, huku wanachama wengine wakipewa karipio kali.Hata hivyo, wabunge hao wamekataa kutambua kufukuzwa kwao huku wakifungua kesi Mahakama kuu kupinga maamuzi vyama vyao.

Profesa Wangwe
Kuhusu nani anaweza kuteuliwa kugombea urais kupitia Chadema mwaka 2015, Mkurugenzi wa Taasisi ya Kuondoa Umasikini (Repoa), Profesa Samweli Wangwe alisema vyama vitakavyoteua wagombea ni lazima vichunguze kwa makini na kuona kwamba mgombea huyo lazima awe na uwezo wa kuimarisha uchumi ambao Watanzania wote wanaweza kushiriki katika kuujenga.

Alisema matatizo mengi ya kiuchumi yaliyopo nchini yanatokana na uchumi kusambaratika na wanaoshiriki katika kuujenga kuwa wachache.”Mtu huyo lazima awe na mtazamo wa kiuchumi na ili mabadiliko hayo yawepo ni lazima ujengwe uchumi ambao watu wote pamoja na masikini wata-participate (watashiriki).
Lakini akasema vyama vya upinzani hususan Chadema ambayo ilionekana kufanya vizuri katika uchaguzi uliopita, kitategemea kufanya vibaya kwa CCM ili kiweze kupata ushindi.
“Ili mgombea wa Chadema aweze kuchaguliwa itategemea sana kufanya vibaya kwa serikali ya CCM… Lakini ikifanya vizuri, itakuwa ni wakati mgumu kwao,” alisema Profesa Wangwe.

Alipotakiwa kumtaja mtu ambaye anamuona kuwa anaweza kufanya vizuri kupitia Chadema, alisema ni vigumu kufanya hivyo kwa sababu hali hiyo inategemea sana ajenda ya chama hicho kwa mwaka 2015.

Alikiri kuwa Chadema kiliweza kuungwa mkono katika uchaguzi uliopita, lakini mipango yake kwa mwaka 2015 itategemea ajenda waliyo nayo na kufanya vibaya kwa serikali ya CCM.

Ndani ya CUF
Kwa upande wa CUF Mbunge wa Wawi aliyefukuzwa kutoka chama hicho hivi karibuni Hamad Rashid amekataa kuuhusisha mgogoro huo na harakati zake za kutaka urais wa Zanzibar.

“Sikuyaanzisha mapambano haya kwa kutaka cheo. Mimi nilipewa uwaziri wakati wa Mwalimu Nyerere, lakini sikukubali, nikawaambia kuwa nitabaki tu na u-naibu Waziri wa Fedha” alisema Hamad na kuongeza;

“Mimi nimeshiriki kuanzisha CUF lakini sijawahi kuwa na uongozi mkubwa ndani ya chama, zaidi ya u-naibu Mkurugenzi tu. hata leo tukianzisha chama, wenzangu wakichagua viongozi, mimi niko radhi tu”.

Lakini kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho upande wa Zanzibar Ismail Jussa ametuhumu Hamad kufanya vurugu ndani ya CUF kwa lengo la kumpindua Maalim Seif katika nafasi ya ukatibu Mkuu, kisha kugombea urais.
“Kama anapinga kutotaka cheo, basi Hamad anaanza kuchanganyikiwa. Mara ngapi katika matamshi yake amekuwa akitangaza kuitaka nafasi ya Ukatibu Mkuu. Anajidanganya,” alisema Jussa na kuongeza.Chanzo :Mwananchi