Ndugulile Atembelea Hospitali Ya Taifa Ya Muhimbili na Kusema “Ni Dhahiri Kuwa Mgomo wa Madaktari na Sasa Manesi Upo,Ni Dhahiri KuwaMGOMO WA MADAKTARI NCHINI:Mbunge Wa Kigamboni(CCM) Dk Faustine Mgomo Huu una Madhara kwa Wagonjwa Wasio na Hatia.”


Mbunge wa Kigamboni(CCM)Dk Faustine Ndugulile

UTANGULIZI
Leo mchana nimepata nafasi ya kutembelea hospitali ya Muhimbili hali niliyokuta ni tofauti na taarifa zinazotolewa kwenye vyombo vya habari.Kwa kifupi hali ni mbaya sana. Nilipofika maeneo ya mapokezi nilikutana na gari la Halmashauri ya Bagamoyo lililokuwa limezongwa na waandishi wa habari. Nilipoulizia nikaambiwa kuwa mgonjwa aliyekuwa mahututi katika gari hilo hakupokelewa na hospitali hiyo na hivyo kuamuriwa kurejeshwa Bagamoyo. Nilichukua hatua za haraka za kuwasiliana na uongozi wa idara ya dharura (Emergency Department). Namshukuru Prof.Victor Mwafongo kwa kuwasili katika eneo husika na kuchukua maamuzi ya kumpokea mgonjwa yule.

Nilipata nafasi ya kutembelea maeneo mbalimbali ya hospitali. Baadhi ya wodi hazikuwa na madaktari wala manesi. Nilitaarifiwa kuwa manesi nao walikuwa kwenye vikao vyao vya majadiliano. Wagonjwa walikuwa wanahudumiwa na wahudumu wa afya ambao kitaaluma hawapaswi kuhusika na matibabu ya mgonjwa.

Kliniki za wagonjwa wa nje vilikuwa hazina watu kabisa kinyume na hali ya kawaida. Madaktari waandamizi walinitaarifu kuwa operesheni zote zisizo za dharura (elective operations) zimesimama isipokuwa operesheni chache za dharura.

Ni dhahiri kuwa mgomo wa madaktari na sasa manesi upo. Ni dhahiri kuwa mgomo huu una madhara kwa wagonjwa wasio na hatia. Tusichokijua ni idadi ya wagonjwa waliopoteza maisha na kukosa tiba muhimu katika kipindi cha mgomo.

KIINI CHA MGOGORO
Mgogoro huu unatokana na kucheleweshwa kulipwa kwa posho za kila mwezi za madaktari walio kwenye mazoezi ya vitendo (Interns). Suala hili lilipelekea madaktari kugoma. Pamoja na kulipwa fedha walizokuwa wanadai madaktari hao, Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii haikutumia busara kuwahamisha madaktari waliokuwa wanadai haki zao. Vilevile kauli za kejeli na ubabe za viongozi wa Wizara zilizidi kuwachochea madaktari hawa, hali iliyopelekea kubadili sura ya mgomo kutoka ule wa interns hadi kuwa mgomo wa nchi nzima wenye madai lukuki kuhusu hali ya huduma za afya, maslahi na madeni ya madaktari n.k. Cha kutisha zaidi ni kwamba kada yingine kama manesi, mafundi sanifu maabara, mionzi na wafamasia nao wameanza kugoma pia.
Vilevile Wizara haikujipanga vizuri na wala kushirikisha wadau wengine muhimu katika kutafuta suluhu ya sakata hili.

NINI KIFANYIKE

Hekima na busara zitumike katika kushughulikia suala hili. Nguvu na vitisho vitazidi kuchochea mgomo huu.

Serikali ichukue hatua za haraka za kukutana na madaktari walio kwenye mgomo na kuwasikiliza madai yao. Iundwe timu ya Serikali na madaktari kupitia madai yote , kuyachuja na kuyapa vipaumbele. Madai yatakayokubalika na pande zote mbili yawe na muda maalum wa utekelezaji (Timeframe).

Niwaombe madaktari wenzangu waweke utaratibu wa kutoa huduma za dharura kwa wananchi wakati huu ambao wako kwenye majadiliano na Serikali ili kupunguza usumbufu usio wa lazima kwa wananchi. Hatua hii itawajengea heshima kwenye jamii.
Serikali iangalie upya maslahi ya watumishi wa umma ikiwa ni pamoja wale walio kwenye sekta nyeti. Hili liendane sambamba na kuboresha mazingira ya kazi na upatikanaji wa vitendea kazi.

Serikali ichunguze kiini cha mgogoro huu na kuchukua hatua za nidhamu kwa watendaji waliosababisha sakata hili.