MAKUBALIANO YA MKUTANO KATI YA KAMATI YA JUMUIYA YA MADAKTARI NA ‘TASK FORCE’ YA MADAKTARI BINGWA WA MNH



1. TUMEKUBALIANA KUWA KAMATI YA KUSHUGHULIKIA MADAI YA MADAKTARI NI
MOJA NA HAKUNA YEYOTE MWENYE MAMLAKA YA KUKUTANA, KUJADILI AU KUKUBALIANA NA SERIKALI JUU YA MADAI HAYO ISIPOKUWA KAMATI YA JUMUIYA YA MADAKTARI AMBAYO INAJUMUISHA MADAKTARI BINGWA PIA KAMA WANAJUMUIYA.
2. TUMEKUBALIANA KUWA NA TAARIFA YA UPOTOSHAJI JUU YA MALENGO YA TIMU
  HIYO YA MADAKTARI BINGWA, KIMSINGI LENGO LAO HASA ILIKUWA NI KUISHINIKIZA SERIKALI KUCHUKUA HATUA HARAKA ILI KUNUSURU HALI YA AFYA NCHINI.
3. PIA TUMEKUBALIANA KUWA KUTOKANA NA HALI YA UZOROTAJI WA HUDUMA YA
  AFYA TUNATOA MWITO KWAMBA KAMATI KWA KUSHIRIKIANA NA CHAMA CHA MADAKTARI KUWA IPO TAYARI HATA LEO KUKAA NA SERIKALI MEZANI ILI KUFIKIA HITIMISHO YA MGOGORO HUU.
4. TUNGEPENDA SERIKALI KUACHA KUTOA VITISHO NA KUKAMATA NA KUWEKA
  RUMANDE BAADHI YA MADAKTARI HAPA NCHINI. KITENDO HICHO HAKITOI SULUHU YA TATIZO HUSIKA.
5. MWISHO SERIKALI ISIJARIBU KUKWEPA KUWASILIANA NA KAMATI SABABU KAMA
  KUNA NJIA YOYOTE YA KUFIKIA SULUHU YA TATIZO HILI NI KUPITIA KAMATI YA JUMUIYA YA MADAKTARI.
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI IMEISHATOLEWA IKIWEMO STAR TV, ITV,  CHANNEL TEN, TUMAINI TV… MAGAZETI KAMA VILE THE CITIZEN, DAILY NEWS, JAMBO LEO, HABARI LEO, MWANANCHI NA KADHALIKA. SOLIDARITY FOREVER

Kauli Ya TPN Kuhusu Migogoro/Migomo iliyopo Hususani Sekta Afya


Rais wa TPN BwPhares Magesa

Rais wa TPN BwPhares Magesa
Kwa muda mrefu sasa jamii yetu imekumbwa na migogoro na migomo ya mara kwa mara katika sekta mbalimbali ikiwemo Afya, Elimu n.k.Na inaonekana kwamba hali hii inataka kuzoeleka na kuonekana ni hali ya kawaida, na kama haitathibitiwa kwa kupatiwa ufumbuzi wa kudumu basi inaweza ikalifikisha Taifa letu mahali pabaya na kupunguza kasi ya ukuaji wa uchumi na hivyo kuathiri mikakati ya kupunguza umasikini.
Kwa sasa dunia nzima iko katika hali tete kutokana na kudorora kwa uchumi na baadhi ya nchi ukuaji wa uchumi umesimama au umeshuka sana hivyo kwa namna moja au nyingine nchi zetu pia zinaathirika na hali hii kwa njia moja au nyingine.
Kwa kuzingatia hali hiyo sisi wanataaluma tunaona kwamba kwa sasa rasilimali tulizonazo ikiwemo watu, ardhi, maliasili n.k tuzitumie vizuri ili zitusaidie kupambana na janga hilo.
Kwa hali hiyo ni dhahiri uwezo wa serikali kugharamia baadhi ya huduma utapungua hivyo basi tunaomba kwa sasa wananchi waelewe hali hivyo na ni jukumu letu sote sasa kushirikiana kupambana na changamoto hizo.
Chanzo kimojawapo cha migomo na migogoro hiyo ni kupungua kwa mawasiliano miongoni mwa wadau husika hivyo kusababisha upande mmoja kutojua au kutohusishwa katika kututua tatizo husika.
Hivyo basi tunashauri wadau wote yaani serikali, viongozi, watendaji wa wizara na taasisi mbalimbali wakae na washirikishane katika sehemu zao za kazi na kupashana habari kwa muda muafaka.
Kuhusu tatizo linaloendelea kwa sasa katika sekta ya afya tunawapa pole nyingi sana watanzania wote waliopoteza maisha na waliaothirika kwa namna moja au nyingine kutokana na athari za mgomo huu.
Baadhi wa waliaothirika yaani wagonjwa na baadhi ya madaktari ni wanachama wetu.
Sisi kama wanataaluma tunaipongeza serikali kwa hatua zilizochokuliwa hadi sasa za kupunguza athari za tatizo hili japokuwa bado sehemu nyingine hali bado haijatengemaa lakini ni matumani yetu kila mtu atatimiza wajibu wake kwa mujibu wa taaluma zao.
Tunaiomba Serikali iharakishe mazungumzo na madaktari na itoe ahadi ya kutekeleza madai ya madaktari kadri uwezo utakavyoruhusu Tunaiomba Serikali ifikire upya uamuzi wake wa awali wa kuwafukuza kazi wale madaktari ambao walikuwa bado hawajaripoti kazini kama agizo la Mh. Waziri Mkuu lilivyoelekeza badala yake tunashauri hatua nyingine za kinidhamu zichukuliwe badala ya kuwafukuza kazi, kwa sasa bado nchi ina upungufu mkubwa wa wataalamu katika sekta hii.
Tunawashauri madaktari wote nchini wakati madai yao yakishughulikiwa warejee katika maeneo yao ya kazi na wafanye kazi kwa bidii na maarifa yao yote, waonyeshe uzalendo kwa nchi yao.
Wale wote walitajwa katika taarifa mbalimbali kwa tuhuma mbalimbali ikiwa ni pamoja na kushindwa kuwajibika kwa kutoa kauli zilizochochea au kukuza mgogoro huu basi waombe radhi mara moja na kama wakishindwa basi hatua za kinidhamu zichukuliwe haraka dhidi yao.
Tunaomba watanzania wote, viongozi, watendaji wa Taasisi za umma na binafsi tuwe waadilifu tuzingatie dhana ya utawala na uongozi bora, tuwe wazalendo wa kweli na tuweke mbele Utaifa na maslahi ya walio wengi.
Phares Magesa 
Rais- TPN

NAPE ATOA TAMKO LA CCM MGOMO WA MADAKTARI,POSHO ZA WABUNGE


TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI.
Kwa muda sasa nchi yetu imepitia kwenye tatizo kubwa la mgomo wa madaktari katika hospitali nyingi hasa za umma ambao kwa kiasi kikubwa mgomo huo umekuwa na madhara makubwa kwa watanzania masikini ambao ni wengi, kiasi cha kugharimu hata maisha yao.
Chama Cha Mapinduzi kinachukua nafasi hii kuwapa pole sana wale wote walioathiriwa kwa namna moja ama nyingine na mgomo huu. Na kwakweli tunasikitishwa sana na hali inayoendelea!
Chama Cha Mapinduzi kinawapongeza na kuwashukuru madakitari walioonyesha ubinadamu na uzalendo kwa kuamua kurudi kazini na ambao hawakugoma kabisa. Tunawashukuru na kuwapongeza kwani hakuna masilahi yanayovuka thamani ya uhai wa binadamu mwenzako!
Tunachukua fursa hii pia kuwashukuru sana na kuwapongeza askari wetu wa jeshi la wananchi wa Tanzania kwa uamuzi wao wa kizalendo wa kuamua kuitikia wito wa serikali kwenda kwenye baadhi ya hospitali kusadia kuwatibu watanzania wenzao. Moyo huu ni wa kizalendo na wa mfano. Tunajivunia uzalendo wa jeshi letu!
Tunachukua nafasi hii kuwaomba madaktari wanaoendelea na mgomo kurudi kazini huku wakiendelea na mazungumzo na serikali. Tunaamini madai yao yanawezekana kushughulikiwa ikiwa pande zote mbili zitaamua kukaa chini kwa dhati na kuzungumza.
Serikali kwa upande mmoja watafute kwa makini chanzo cha mgogoro huu na kutafuta majibu, na madakitari nao kwa upande wa pili, wawe tayari kukaa mezani na kuzungumza. Tunasisitiza thamani ya maisha ya binadamu ni kubwa kuliko masilahi na madai wanayoyaomba!
Serikali ni vizuri ikajenga utamaduni wa kushughulikia matatizo haya ambayo yanaathiri wananchi wengi kwa uharaka na udharura unaostahili badala ya kusubiri hali inapokuwa mbaya zaidi.
POSHO ZA WABUNGE
Kwa upande mwingine Chama Cha Mapinduzi kinapenda kurudia wito kilioutoa juu ya swala la posho za wabunge. CCM iliwaomba na kuwasihi wabunge na mamlaka zinazohusika na mchakato wa swala hili kuliangalia upya na kutumia busara, ikiwezekana kuachana nalo kwasasa.
CCM inaupongeza na kuunga mkono msimamo wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dr. Jakaya Mrisho Kikwete kama ulivyonukuliwa na taarifa ya Ikulu kwa vyombo vya habari, kuwa ni vizuri wabunge wakalitafakari upya swala hili kwa masilahi mapana ya wale waliowapa dhamana ya kuwawakilisha bungeni.
CCM inaendelea kuwasihi waheshimiwa wabunge walitafakari upya swala hili na busara itumike katika kuliamua huku wakifungua masikio kusikiliza sauti za Watanzania kwani huko bungeni wana wawakilisha hawa Watanzania, ni vizuri kusikiliza hiki kilio chao! Si busara kupuuza kilio cha waliokupa dhamana ya kuwawakilisha.
Msimamo wa Rais Kikwete kama sehemu moja ya mamlaka inayohusika na mchakato huo ni uthibitisho wa usikivu wake kwa wananchi anaowaoongoza, yeye katimiza wajibu wake, tunawasihi waheshimiwa wabunge wetu nao walitafakari hili na kuona busara ya kuachana nalo kwasasa.
Imetolewa na;
Nape Moses Nnauye
Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa CCM
Itikadi na Uenezi.

Zitto Zuberi Kabwe : Bunge halina mguso na wananchi ‘out of touch’


Inasikitisha kwamba Bunge laweza kukaa wiki nzima na kujadili masuala mbalimbali bila kutoa muda kujadili suala la mtikisiko katika sekta Afya. Siku ya kwanza ya Bunge nilisimama kutaka taarifa ya serikali kuhusu mgomo wa madaktari na taarifa hiyo ijadiliwe na Bunge. Spika akajulisha Bunge kwamba Serikali imempa taarifa na itawasilishwa. Bunge likaahirishwa siku bila kurejea.