Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad Akutana na Balozi Wa Sudan Nchini Tanzania


Amesema eneo hilo ni muhimu kwa maendeleo ya Zanzibar kwa vile litasaidia kutoa ajira kwa vijana wengi nchini na kuwawezesha kukabiliana na ukali wa maisha.

Maalim Seif ameeleza hayo leo ofisini kwake Migombani mjini Zanzibar alipokuwa na mazungumzo na balozi wa Sudan nchini Tanzania Dk. Yassir Mohamed Ali.

Amefahamisha kuwa Sudan inayo fursa nzuri ya kuwekeza viwanda vya nguo hapa Zanzibar ikizingatiwa kuwa nchi hiyo ni mzalishaji mzuri wa zao la pamba barani Afrika, hali ambayo pia itasaidia kuhimili ushindani wa kibiashara katika soko la Afrika Mashariki.
Makamu wa Kwanza wa Rais pia ameelezea haja kwa nchi hiyo kutoa ushirikiano katika kilimo cha umwagiliaji, ili kuweza kusaidia sera za serikali za kuinua kilimo hicho ambacho ni muhimu katika wakati huu wa mabadiliko ya tabia nchi.
Maalim Seif amesema Zanzibar imekuwa ikinufaika kwa kiasi kikubwa kutokana na uhusiano wa kihistoria uliopo baina yake na Sudan na kutaka uhusiano huo uendelezwe kwa maslahi ya pande hizo mbili.
Amesema kwa muda mrefu Sudan imekuwa ikishirikiana na Zanzibar katika sekta mbali mbali za maendeleo zikiwemo elimu, Afya na kilimo, sambamba na kubadilishana wataalamu katika sekta hizo.
Katika sekta za elimu na afya, Makamu wa Kwanza wa Rais amesema Sudan imekuwa karibu na Zanzibar kwa kutoa fursa za elimu nchini humo sambamba na kuleta wataalamu wa afya ambao huisaidia Zanzibar katika kupambana na maradhi mbali mbali.

Ameiomba Sudan kuangalia uwezekano wa kuisaidia zaidi Zanzibar katika sekta ya elimu ili kuziba pengo la upungufu wa walimu wa sayansi katika skuli mbali mbali nchini.
“Vijana wetu wengi wanahitimu masomo ya sanaa yakiwemo yale ya dini ya kiislamu na lugha ya kiarabu, hali inayopelekea kuwa wengi na kusababisha hata kukosa ajira, na kwamba kwa sasa serikali inahitaji sana walimu wa sayansi mashuleni hasa wale wa somo la hisabati”, alifafanua Makamu wa Kwanza wa Rais.

Ktika hatua nyengine, Makau wa Kwanza wa Rais ameipongeza Sudan kwa kuandaa kura ya maoni na hatimaye uchaguzi uliopelekea kuligawa taifa hilo kwa njia za amani.
Ameiomba Sudan kutafuta ufumbuzi wa kudumu katika jimbo la Darfur ili kuliweka taifa hilo katika hali ya amani ambayo itasaidia maendeleo na ustawi wa bara zima la Afrika.

“Zanzibar itafurahi kuona Sudan inaishi kwa amani kwa kuwa ni nchi kubwa ambapo amani hiyo itaweza kuzinufaisha nchi nyengine kiuchumi ikiwemo Zanzibar”, alisema Maalim Seif.
Kwa upande wake Balozi Yassir amemueleza Maalim Seif kuwa nchi yake iko tayari kuendeleza ushirikiano huo na kutafuta maeneo mengine ya ushirikiano ambayo yatasaidia kukuza maendeleo ya wananchi.

Amesema nchi yake ina uzoefu mzuri katika kilimo cha umwagiliaji na sekta ya elimu, na kuahidi kutoa ushirikiano zaidi katika nyanja hizo, sambamba na kuangalia uwezekano wa kuwekeza katika maeneo mbali mbali.

Hassan Hamad
Ofisi ya Makamu Wa Kwanza Wa Rais Zanzibar

Balozi wa Sudan nchini Tanzania Dk. Yassir Mohamed Ali akizungumza na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad huko OMKR Migombani.(Picha NA Salmin Said-Ofisi ya Makamu Wa Kwanza Wa Rais Zanzibar ---