Maoni Ya Mbunge wa( NCCR- Mageuzi- kigoma Kusini) David Kafulila Juu Ya Marekebisho Ya Sheria Ya Kusimamia Mchakato Wa Katiba Mpya


Mbunge wa( NCCR- Mageuzi- kigoma Kusini) David Kafulila ---Habari Watanzania, Nina maoni tofauti kuhusu hiki kinachoendelea kuhusu marekebisho ya sheria ya kusimamia mchakato wa katiba mpya. Nimejaribu kuomba kuchangia ili niweke maoni yangu wazi lakini imeshindikana, Spika amesema NCCR amepewa mtu mmoja tu Mh. Machali hivyo nikaona ni vema niwajulishe kupitia mtandao maoni yangu. UTANGULIZI Hapa ningependa kukumbusha kuwa kutoka NCCR ni mimi David Kafulila na Felix Mkosamali ambao tulikuwa wajumbe wa kamati ya sheria na Utawala. Mh.Mkosamali ni mjumbe wa kudumu kwenye kamati hii, mimi ni miongoni mwa wajumbe walio ongezwa wakati wa kupitia muswada huu. Pia ikumbukwekuwa ni mimi na Mkosamali ambao tuliungana na CHADEMA kutoka nje katika mkutano wa tano wa Bunge kupinga namna mchakato ulivyoendeshwa. Niliomba kuchangia bungeni lakini imeshindikana kabisa kupata nafasi lakini kwa kuzingatia umuhimu wa jambo hili na nafasi niliyokuwa nayo katika jambo hili naona kuna umuhimu wa kuzungumza kitu kwani hatawale mabalozi wa nchi tano za Ulaya walipokuja bungeni kwenye mkutano wa tano ni mimi niliyekuwa mmoja wa wabunge waliokutana nao kutoa maoni. MAONI Nimeshangaa kuona mvutano wa kisiasa kuhusu mabadiliko yaliyoletwa na serikali kwani ninavyofahamu kuna mambo mengi ya msingi katika sheria hii ambayo yalipaswa kubadilishwa, na nilidhani ndiyo yangeletwakwenye marekebisho ya sheria hii baada ya vikao vya Rais na wadau wengine vikiwemo vyama vya siasa. Mabadiliko yaliyoletwa sio issues za msingi ambazo zingesaidia kuiboresha tume na mchakato mzima wa katiba mpya. Kwa mfano; 1. Hoja ya kumwondoa DC na Kuweka Mkurugenzi (DED)Wabunge wengi wa CCM wanataka DC ndio asimamie, wakati hotuba ya kambi rasmi ya upinzani inapendekeza DED.Ukweli ni kwamba wote DED na DC hawafai kwasababu wote ni sehemu ya serikali na badala yake ilipaswa jukumu hilo litekelezwe na Tumeyenyewe ambayo inapaswa kuwa huru. 2.Hapa ndipo inakuja hoja ya mchakato huu mzima wa kura ya maoni kusimamiwa na Tume huru. Uamuzi wa kuifanya Tume ya sasa ya Uchaguzi kusimamia mchakato huu ni kinyume cha msimamo wetu wa awali kama wapinzani kwasababu moja ya hoja ya mahitaji ya katiba mpya ni tume huru ya uchaguzi, sasainawezekanaje tume mbovu ya uchaguzi isimamie mchakato wa kupata katiba huru?. Hili lilikuwa muhimu sana. Tungekubaliana kuhusu kupata kwanza tume huru ya uchaguzi kisha tume hiyo isimamie mchakato wakatiba mpya tungekuwa na uhakika wa kupata katiba ambayo watanzania wanaitaka. 3.Hoja ya Tume huru ya kusimamia mchakato wa katibaHii pia ni hoja iliyoachwa kwasababu Tume hii ya sasa inateuliwa na Rais na kwa namna ilivyo bado Rais ndio mwenye mamlaka ya kumtoa mjumbe yeyote. Marekebisho yaliyoletwa leo yanapendekeza namna ya kumtoa mjumbe wa tume hii ambaye anayetuhumiwa kukiuka kanuni za maadili, kwamba Rais atateua Kamati ya kufanya maamuzi. Hapa haikupaswa Rais kuteua kamati badala yake ilitakiwa sheria itamkerasmi kamati hiyo itakuwa akina nani ili kamati hiyo iwe huru kuliko iteuliwe na Rais, pengine kosa la mjumbe ni mvutano unaohusu nguvu za serikali kwa tume. 4. Hoja ya Sekretariet huru. Kwa mujibu wa sheria hii Sekratariet itaundwa na waziri mwenye dhamana. Hii inaondoa uhuru wa utendaji wa sekretariet, ilipaswa Sekretariet iteuliwe na Tume na iwajibike kwa tume ili kupunguza mkono wa serikali kwenye mchakato na utendaji wa kupata katiba mpya. 5. Hoja ya ushiriki wa Jumuiya za kiraia, taasisi za dini vya vyama vya siasa Marekebisho yaliyoletwa sehemu A, kifungu cha 7 yanatoa uhuru wa jumuiya hizi kushiriki kwa kualikwa na Rais, lakini sehemu hiyo hiyo ya marekebisho kifungu cha 8 inatamka kuwa Rais hafungwi namapendekezo hayo kuteua watu wengine kuwa wajumbe. Hapa kwa tafsiri rahisi ni kwamba, haki imetolewa kwenye kifungu cha 7 na imepokonywa kwenye kifungu cha 8 kwa kuwaweka wananchi tayari wasishangaeitakapotokea mapendekezo yaliyopelekwa na jumuiya yoyote kukataliwayote. Ingepaswa kuweka wazi kuwa Rais atalazimika kuteua miongoni mwa walipendekezwa na sio nje ya waliopendekezwa. Kwa ujumla pamoja na sheria hii kupitishwa leo lakini ina matundu makubwa sana kuweza kuifanya isimamie mchakato huu muhimu kwa uhakika. Bado ni sheria ambayo inategemea sana dhamira ya Rais mwenyewe kuliko mfumo tulioweka. Napenda ifahamike kuwa, sheria hii iliyopitishwa leo haijafanya mabadiliko ya msingi ambayo sisi sote ( wananchi, wanaharakati na wanasiasa) wenye moyo wa dhati wa kuleta mabadiliko kitaifa tulitazamia. Pamoja katika kujenga Taifa David Kafulila(MB)

Taswira Za Kikao Cha Waziri Mkuu Mizengo Pinda na Madaktari na Wauguzi wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili


Waziri Mkuu, Mizengo Pinda akisalimiana na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari inayoongoza mgomo wa madaktari, Stephene Ulimboka baada ya kuzungumza na madaktari na wauguzi wa hospitali ya taifa ya Muhimbili jijini Dar es salaam, Februari 9,2012Waziri Mkuu, Mizengo Pinda akizungumza na Madaktari na wauguzi wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili jijini Dar es salaam Februari 9,2.2012. Kushoto ni Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu, Peniel Lymo, Wapili kushoto ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Hawa Ghasia na Kulia ni Mkurugenzi Mkuu wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Dkt. Marina Njelekela.

Thursday, February 09, 2012 MAREKEBISHO YA SHERIA YA KATIBA:WEREMA APENDEKEZA MAPENZI YA DHARURA


Ile nia njema iliyoonyeshwa na serikali baada ya kujifunza na  kuleta marekebisho ya sheria ya katiba yako shakani kwani mama malecela anataka turudi tulikotoka.amekomaa komakoma kutaka wakuu wa wilaya wabaki kuwa wasimamizi wakuu wa katiba mpya huku upinzani ukiunga mkono mapendekezo ya serikali kuwaondoa na kuingiza wakurugenzi wa wilaya.inavyoonekanakwetu MALECELA na wenziye wanataka turudi nyuma.mwanasheria wa serikali katika kujaribu kunusuru hali amependekeza mapenzi ya dharura kati ya vyama hasimu bila shaka.spika amezuia kupigwa kura juu ya jambo hilo.nadhani ameona athari zinazoweza kuletwa na kura za ushabikizinazoweza kusahau maumivu ambayo taifa limepata kabla.tusubiri kesho

HOTUBA YA MHE CELINA O. KOMBANI, WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA AKIWASILISHA BUNGENI MUSWADA WA MAREKEBISHO YA SHERIA YA MABADILIKO YA KATIBA YA MWAKA 2011 LEO BUNGENI MJINI DODOMA


Waziri wa Katiba na Sheria Mh Celina Kombani --HOTUBA YA MHE CELINA O. KOMBANI, WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA AKIWASILISHA BUNGENI MUSWADA WA MAREKEBISHO YA SHERIA YA MABADILIKO YA KATIBA YA MWAKA 2011 __________________________ Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Katiba na Sheria, Mheshimiwa Celina O. Kombani, kwa heshima na taadhima, naomba kutoa hoja kwamba Bunge lako tukufu sasa lijadili na hatimaye kupitisha Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba wa mwaka 2012 yaani, “The Constitutional Review (Amendment) Act, 2012”. Mheshimiwa Spika, Muswada ni matokeo ya kazi nzuri iliyofanywa na Waandishi wa Sheria; Kamati; na baadhi ya Wabunge kutoka vyama vyote vya siasa. Ninawashukuru sana. Ninamshukuru sana Mhe. Pindi Hazara Chana, Mbunge Viti Maalum, Mwenyekiti wa Kamati ya Katiba, Sheria na Utawala , Mhe. Angela Jasmine Kairuki, Mbunge wa Viti Maalum, Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo na kupitia kwao Wajumbe wote wa Kamati kwa mchango na kazi kubwa waliyoifanya kuuboresha Muswada huu. Maoni na ushauri wao kwa kiasi kikubwa vimesaidia kuuboresha sana Muswada huu. Hii inathibitishwa na marekebisho katika Muswada kama yanavyoonekana katika Jedwali la Marekebisho ambalo waheshimiwa Wabunge wamegawiwa. Mheshimiwa Spika, Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya mwaka 2011, Na. 8/2011 ilipitishwa na Bunge hili katika Mkutano wake wa Tano. Tunaleta mapendekezo ya kufanya marekebisho hayo muda mfupi tu baada ya Bunge kutunga Sheria hii na baada ya Mhe. Rais kuiridhia tarehe 29 Novemba, 2011 na kuanza kutumika tarehe 1 Desemba, 2011. Mantiki ya marekebisho haya, na kama yatakubaliwa na kupitishwa na Bunge hili, yanalenga kuiboresha Sheria hiyo na kuwezesha kuwepo kwa muafaka wa kitaifa katika kuendesha mchakato wa kuipata Katiba Mpya. Jambo lolote linalotuwezesha kuwa na muafaka wa kitaifa katika jambo muhimu kama mchakato wa kupata Katiba Mpya inayokidhi matarajio, matumaini na mahitaji ya Watanzania wengi ni jambo jema na linalopaswa kupewa nafasi kila inapowezekana. Mheshimiwa Spika, historia ya kuupitisha Muswada huo kuwa Sheria hii hapa Bungeni inaeleweka na sina sababu ya kuirudia. Kama mnavyofahamu, kabla na baada ya kusaini Sheria hiyo, Mheshimiwa Rais aliendelea kupokea maoni ya wadau mbalimbali kuhusu namna ya kuiboresha Sheria hiyo ili kuwezesha kuwepo muafaka wa kitaifa. Maoni hayo yalitolewa na vyama vya siasa, asasi za kiraia na jumuiya za kidini. Kwa kuzingatia baadhi ya maoni yaliyotolewa, Serikali imetoa mapendekezo ya kurekebisha Sheria hiyo kama yalivyoainishwa kwenye Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya mwaka 2011 na Jedwali la Marekebisho. Mheshimiwa Spika, Muswada huu unapendekeza kufanya marekebisho katika vifungu vya 6, 12, 13, 17, 18 na 21 vya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya mwaka 2011. Lengo la mapendekezo katika vifungu hivyo ni kuondoa sharti la viongozi wa vyama vya siasa kwa ngazi yoyote kutoteuliwa kuwa wajumbe wa Tume, kumruhusu Rais kualika vyama vya siasa vyenye usajili wa kudumu, mashirika ya kidini, taasisi, asasi na makundi mengine ya watu wenye malengo yanayofanana kutayarisha orodha ya majina ya wajumbe ili Rais achague miongoni mwao Wajumbe wa Tume; kuainisha utaratibu wa kumuondoa Kamishna wa Tume na kuruhusu Wakurugenzi wa Serikali za Mitaa, Wakurugenzi wa Manispaa na Makatibu wa Mabaraza ya Miji au Wilaya kupokea taarifa za programu zitakazoendeshwa katika maeneo yao, badala ya Wakuu wa Wilaya. Aidha, marekebisho hayo yanalenga pia kuruhusu jumuiya, asasi, taasisi au makundi ya watu yenye malengo yanayofanana kuandaa mikutano kwa ajili ya kutoa fursa kwa ajili ya kukusanya maoni juu ya Rasimu ya Katiba na kisha kuwasilisha maoni hayo kwenye Tume. Mheshimiwa Spika, katika Jedwali la Marekebisho, tunapendekeza kuwa Ibara ya 2 ya Muswada ifanyiwe marekebisho kwa kuiandika upya. Lengo la mapendekezo hayo ni kuondoa kizuizi kwa madiwani kuwa wajumbe wa Tume. Kwa kuwa madiwani hawataingia katika hatua ya Bunge Maalum la Katiba, tunapendekeza kuwa wasizuiwe kuwa wajumbe wa Tume iwapo itaonekana kuwa wapo wenye sifa za kuteuliwa kuwa wajumbe wa Tume. Mheshimiwa Spika, Jedwali la Marekebisho linapendekeza kuongeza masharti katika Ibara hiyo ya 2 ya Muswada kwa kuongeza masharti mapya katika kifungu cha 6 cha Sheria ya Marekebisho ya Katiba. Masharti yanayopendekezwa yanalenga kumwezesha Mheshimiwa Rais kualika vyama vya siasa, mashirika ya kidini, asasi za kiraia, jumuiya, taasisi na makundi mengine yenye malengo yanayofanana kumpatia orodha ya majina, ambayo miongoni mwao Rais atateua wajumbe wa Tume. Hii itasaidia kuweka uwazi na ushirikishi wa wananchi katika hatua ya uteuzi wa wajumbe wa Tume. Aidha, masharti mengine yanayoongezwa katika kifungu hicho yanalenga kuweka bayana kuwa pamoja na kualika vyama vya siasa, mashirika ya kidini, asasi za kiraia, jumuiya na taasisi na kuteua wajumbe kutoka miongoni mwa majina hayo, Rais hatazuiwa kuteua wajumbe wengine ambao ataona wanafaa kuwemo kwenye Tume. Mheshimiwa Spika, aya B ya Jedwali la marekebisho inapendekeza kuingiza masharti mapya katika kifungu 12 ili kuainisha jinsi mjumbe wa Tume atakavyoondolewa kwenye Tume. Inapendekezwa kuwa iwapo suala la kumwondoa mjumbe wa Tume litajitokeza, basi Rais awateue Wajumbe wa Kamati kuchunguza suala hilo. Kamati hiyo itakuwa na Jaji wa Mahakama ya Rufani ambaye atakuwa Mwenyekiti wa Kamati, Kamishna wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Kamishna wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Wakili wa Mahakama Kuu ya Zanzibar atakayeteuliwa na Chama cha Wanasheria cha Zanzibar na Wakili wa Mahakama Kuu atakayeteuliwa na Chama cha Wanasheria Tanganyika. Aidha, inapendekezwa kuwa Kamati hiyo ipewe mamlaka ya kutengeneza taratibu zitakazoingoza katika kufanya uchunguzi. Marekebisho mengine yanapendekezwa katika kifungu cha 13 cha Sheria hiyo katika kifungu kidogo cha (6) kwa azma ya kuifanya Tume kuwa mamlaka ya nidhamu kwa wajumbe wa Sekretarieti. Sheria ya sasa haionyeshi mamlaka ya nidhamu kwa wajumbe hao. Mheshimiwa Spika, tunapendekeza kufanya marekebisho katika kifungu cha 17 cha Sheria ili kuwezesha Tume kufanya kazi na Wakurugenzi wa Mamlaka ya Serikali za Mitaa kwa upande wa Tanzania Bara, na Mkurugenzi wa Manispaa na Makatibu wa Mabaraza ya Miji au Wilaya kwa upande wa Tanzania Zanzibar katika uandaaji wa mikutano na hadhira zenye kufanana na hizo badala ya Wakuu wa Wilaya walioanishwa kwenye Sheria. Marekebisho mengine yanapendekezwa katika kifungu hicho hicho ili kuruhusu mtu binafsi, taasisi au kikundi cha watu wenye malengo yanayofanana kuendesha progamu ya elimu kwa umma kuhusu mabadiliko ya Katiba baada ya kutoa taarifa, kusajiliwa na kuanisha chanzo cha mapato ya kuendeshea programu hiyo kwa Tume. Inapendekezwa pia kuwa asasi, taasisi, jumuiya au vikundi vyenye malengo yanayofanana viruhusiwe kuandaa mikutano kwa lengo la kukusanya maoni ya wanachama wao kuhusu Katiba na kisha kuyawailisha kwenye Tume. Hata hivyo, endapo asasi, taasisi, jumuiya au vikundi hivyo vitataka kufanya mikutano au mikusanyiko ya hadhara, watalazimika kutoa taarifa kwenye mamlaka husika kwa mujibu wa Sheria husika za Tanzania Bara au Tanzania Zanzibar. Marekebisho ya Mwisho yanapendekezwa kufanywa katika kifungu cha 21(3) ili kupunguza adhabu kwa watu watakaokiuka masharti ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba. Adhabu inayopendekezwa ni faini isiyopungua shilingi milioni mbili na isiyozidi shilingi milioni tano au kifungo kwa muda usiopungua mwaka mmoja na uziozidi miaka mitatu badala ya faini isiyopungua milioni tano na isiyozidi milioni kumi na tano au kifungo kwa muda usiopungua miaka mitatu na uziozidi miaka saba inayoanishwa kwenye Sheria ya sasa. Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo haya ninapenda, kupitia kwako, kuwaomba Waheshimiwa Wabunge, kuujadili Muswada huu na kuupitisha katika hatua mbili, yaani, Kusomwa Mara ya Pili na Kusomwa Mara ya Tatu. Nina imani kwamba Bunge lako litaridhia marekebisho yote yanayopendekezwa na litakubali marekebisho haya yawe sehemu ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya mwaka, 2011. Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja. ____________________________

 

 

WAVULANA WAPETA MATOKEO KIDATO CHA NNE


Mwanafunzi wa Shule ya Sekondari Marian Girls, Roselye Tandau (16) akishangilia jijini Dar es Salaaam jana baada ya kutangazwa mshindi wa pili katika mtihani wa Kitaifa wa Kidato cha nne wa mwaka 2011. Picha na Venance Nestory
BARAZA la Mtihani la Taifa(Necta) limetangaza matokeo ya mtihani wa kidato cha nne uliofanyika mwaka jana yanaonyesha kuwa asilimia 53.59 ya wanafunzi 426,314 waliofanya mtihani huo wamefaulu.
Hata hivyo, wakati asilimia hiyo ambayo ni sawa na wanafunzi 180,216 wakifurahia matokeo hayo, wenzao 3,301 wamefutiwa matokeo kutokana na udanganyifu ikiwamo mfanano usio wa kawaida wa majibu. Akitangaza matokeo hayo jijini Dar es Salaam jana, Katibu Mtendaji wa Necta, Dk Joyce Ndalichako alisema wasichana waliofaulu ni 90,885 sawa na asilimia 48.25 na wavulana ni 134,241 sawa na asilimia 57.51.

“Mwaka 2010 watahiniwa waliofaulu walikuwa 223,085 sawa na asilimia 50.74, hivyo ufaulu umeongezeka kwa asilimia 2.63,” alifafanua Dk Ndalichako. Wanafunzi 10 bora Dk Ndalichako aliwataja wanafunzi 10 bora kitaifa kuwa ni Moses Andrew Swai kutoka shule ya Feza Boys, Rosalyn Tandau kutoka Marian Girls, Mboni Mumba kutoka St Francis Girls na Sepiso Mwamelo kutoka St Francis Girls. Wengine na shule zao kwenye mabano ni Uwella Rubuga (Marian Girls), Hellen Mpanduji (St Mary’s Mazinde Juu), Daniel Wallace Maugo (St Joseph Millennium), Benjamin Tilubuzya, (Thomas More Machrina), Simon Mbangalukela (St. Joseph Millennium) na Nimrod Rutatora (Feza Boys).

Wasichana 10 bora
Kwa upande wa wasichana kumi bora, Dk Ndalichako aliwataja na shule walizotoka kwenye mabano kuwa ni Rosalyn (Marian Girls), Mboni (St Francis Girls), Sepiso Mwamelo (St Francis Girls), Uwella Rubuga (Marian Girls) na Hellen Mpanduji (St Mary’s Mazinde Juu). Wengine ni Lisa Chille (St Francis Girls Mbeya), Elizabeth Ng’imba (St Francis Girls Mbeya), Doris Noah (Kandoto Sayansi Girls), Herieth Machunda (St Francis Girls Mbeya) na Daisy Mugenyi (Kifungilo Girls Tanga).

Wavulana 10 bora
Wavulana kumi waliofanya vizuri zaidi katika mtihani humo ni Moses Andrew Swai (Feza Boys), Daniel Maugo (St Joseph Millennium), Benjamini Tilubuzya, (Thomas More Machrina), Simon Mbangalukela (St. Joseph Millenium) na Nimrod Rutatora (Feza Boys). Wengine ni Simon Mnyele (Feza Boys), Paschal Madukwa (Nyegezi Seminary), Henry Stanlay (St Joseph Millenium), Fransisco Kibasa (Mzumbe) na Tumain Charles (Iliboru).
Shule 10 bora
Matokeo hayo yanaonyesha shule kumi bora zenye zaidi ya watahiniwa 40 kuwa ni St. Francis Girls ya Mbeya, Feza Boys, St Joseph Millenium, Marian Girls, Don Bosco Seminary, Kasima Seminary, St. Mary’s Mazinde Juu, Canossa, Mzumbe na Kihaba.

Matokeo hayo yanaonyesha pia shule 10 bora zenye watahiniwa chini ya 40 kuwa ni Thomas More Machrina, Feza Girls, Dungunyi Seminary, Maua Seminary, Rubya Seminary, St Joseph Kilocha Seminary, Sengerema Seminary, Lumumba, Queen of Apostles- Ushirombo na Bihawana Junior Seminary.
Shule 10 za mwisho
Shule kumi za mwisho zenye watahiniwa zaidi ya 40 ni Bwebwera, Pande Daraja, Mufindi, Zirai, Kasokala, Tongoni, Mofu, Mziwa, Maneromango na Kibuta. Na shule kumi za mwisho zenye watahiniwa chini ya 40 ni Ndongosi, St Luke, Igingwa, Kining’inila, Ndaoya, Kilangali, Kikulyungu, Usunga, Mto bubu day na Miguruwe. Waliofutiwa matokeo Dk Ndalichako alifafanua zaidi kuwa watahiniwa 3,301 waliobainika kufanya udanganyifu wamefutiwa matokeo na hawataruhusiwa kufanya mtihani wowote wa Necta kwa kipindi kisichopungua miaka mitatu.

Dk Ndalichako alisema kati yao watahiniwa waliofanya mtihani huo walikuwa 426,314, sawa na asilimia 94.67 ya watahiniwa wote waliosajiliwa. “Mwaka 2010 watahiniwa waliosajiliwa walikuwa 458,114 hivyo, idadi ya watahiniwa imepungua kwa watahiniwa 7,790 sawa na asilimia 1.70,” alisema Dk Ndalichako. Alisema mwaka jana, watahiniwa wa shule waliosajiliwa walikuwa 349,39 na watahiniwa huku wa kujitegemea wakiwa ni 100,934. Akifafanua zaidi juu ya matokeo hayo, Mtendaji Mkuu huyo wa Necta alisema watahiniwa 450,324 walisajiliwa kufanya mtihani huo ambao wasichana ni 201,799, sawa na asilimia 44.81 na wavulana 248,525, sawa na asilimia 55.19. Alisema jumla ya watahiniwa wa shule 180,216 sawa na asilimia 53.59 ya waliofanya mtihani wa kidato cha nne wamefaulu, kati yao wasichana wakiwa 69,913 na wavulana 110,303.

Kwa upande wa watahiniwa wa kujitegemea, waliofaulu ni 44,910 wasichana wakiwa 20,972 na wavulana 23,938.
Waliofutiwa mitihani
Dk Ndalichako alisema Necta imefuta matokeo ya watahiniwa 3,03 waliobainika kufanya udanganyifu kati yao, watahiniwa wa shule ni 3,301 na wawili wakiwa wa maarifa (QT). Akifafanua zaidi juu ya udanganyifu huo alisema , 182 walikamatwa na wasimamizi wakiwa na makaratasi (notes) sita walikamatwa na simu, watatu walikuwa wakifanyiwa mtihani na watu wengine, wanne walisajiliwa kufanya mtihani kwa majina ya watu wengine.

Dk Ndalichako aliongeza kwamba, pia watahiniwa 2,896 karatasi zao za majibu zilikuwa na mfanano usio wa kawaida, 155 karatasi zao za majibu zilikuwa na miandiko zaidi ya mmoja, 14 kubadilishana karatasi katika chumba cha mtihani, 18 kukamatwa na karatasi za majibu zaidi ya moja, 25 wakiwa na mfanano usio wa kawaida wa majibu , kuwa na vikaratasi ama kubadilishana vikaratasi. “Mtu mmoja unakuta mitihani yake ya majibu ina miandiko zaidi ya 10, na jeshi la polisi ndilo lililothibitisha kuwa miandiko ya wanafunzi hawa ilikuwa inatofautiana. Alisema pia kuwa, baraza hilo limefuta matokeo ya watahiniwa nane walioandika matusi ya nguoni kwenye karatasi zao za majibu. “Kitendo cha kuandika matusi kwenye karatasi za majibu kinaonyesha utovu wa nidhamu, hivyo pamoja na kuwafutia matokeo ufuatiliaji zaidi unaendelea ili kuona hatua za kuwachukulia,” alisema Dk Ndalichako.

Pia alitoa onyo kali kwa vituo vilivyohusika na udanganyifu huo, huku akisema kwa vilivyobaika vitaandikiwa barua ya kutaka vijieleze kwa nini visifutiwe matokeo. Dk Ndalichako akielezea zaidi juu ya hali hiyo, alisema baadhi ya watahiniwa waliandika nyimbo za kizazi kipya (Bongo fleva) kwenye karatasi zao za majibu huku wengine wakichora michoro isiyo eleweka na wachezaji wa mpira. “Mwingine aliandika bongo fleva, ngoja niwasomee ‘wasahihishaji msinisamehe…, acha utani na girl wangu, najukuja home nakukuta.. nikifeli mtihani naendelea na fani ya muziki,” Dk Ndalichako alisoma moja ya karatasi za majibu za watahiniwa hao huku akiruka baadhi ya maeneo akisema ameandika matusi yasiyoweza kusomeka.
Ubora wa ufaulu kwa jinsi
Dk Ndalichako alisema ubora wa ufaulu kwa kuangalia madaraja waliyopata watahiniwa wa shule unaonyesha kuwa, jumla ya watahiniwa 33,577 sawa na asilimia 9.98 wamefaulu katika daraja la kwanza mpaka la tatu.

“Wasichana waliofaulu katika daraja la kwanza mpaka la tatu ni 10,313 sawa na asilimia 7.13 na wavulana ni 23,267, sawa na asilimia 12.13,” alisema Dk Ndalichako. Aliongeza kwamba, waliopata daraja la nne ni 146,639 sawa na asilimia 43.60 ambao wavulana ni 87,039 sawa na asilimia 45.40 na wasichana 59,600, sawa na asilimia 41.22. Dk Ndalichoka aliongeza kwamba, waliofeli ni 0156,089 sawa na asilimia 46.41, kati yao wavulana wakiwa 81,418 sawa na asilimia 42.47 na wasichana wakiwa 74,667, sawa na asilimia 51.64. mwisho
Chanzo.Mwananchi

UPDATE:Kikao Kinaendelea Kati Ya Madaktari Bingwa na Waziri Mkuu Mizengo Pinda


Waziri Mkuu Mizengo Pinda ---Madaktari walijumuika ukumbi wa CPL leo asubuhi kusubiri ujio wa PM.ambae meshafika na maongezi yameanza.Dk.Ulimboka yuko mbele na madaktari bingwa wako mbele.tutawajuza zaidi -- Katibu mkuu na mganga wa serikali wameondolewa, waziri na naibu waziri watashughulikiwa na rais, call allowances za madaktari bingwa ni 25000/= na madaktari wa kawaida ni 20000/=,madaktari watapewa nyumba na green card.. Madaktari wamekubali offers za serikali na wametoa mwezi mmoja kuona kama kweli serikali inatekeleza kwa dhati ahadi zake.Kesho wataingia kazini .kikao kinaendelea *Taarifa ya Ofisi yaWaziri Mkuu Juu ya Kikao Cha Waziri Mkuu Mizengo Pinda na Madakatari ipo hapo chini -- WAZIRI MKUU MIZENGO PINDA YUPO DAR ES SALAAM KUTOKA DODOMA KUSHUGHULIKIA MGOMO WA MADAKTARI AMBAO UMEKUWA UKIENDELEA KWA LENGO LA KUUPATIA UFUMBUZI.LEO AMEKUTANA NA UONGOZI WA HOSPITALI YA TAIFA YA MUHIMBILI PAMOJA NA MADAKTARI BINGWA KUTOKA SEKTA YA UMMA NA BINAFSI NA WASTAAFU. KESHO(LEO) SAA 3 ASUBUHI ATAKUTANA NA MADAKTARI BINGWA, MADAKTARI WALIOSAJILIWA (REGISTRALS) NA MADAKTARI WALIOKO KWENYE MAFUNZO KWA VITENDO (INTERNS) NA BAADA YA HAPO SAA 4 ATAKUTANA NA WAFANYAKAZI WA HOSPITALI YA MUHIMBILI, MOI, OCEAN ROAD NA WAWAKILISHI KUTOKA HOSPITALI ZA MKOA WA DAR ES SALAAM, KWENYE UKUMBI WA CPL, MUHIMBILI. MATARAJIO YA SERIKALI NI KWAMBA MAZUNGUMZO HAYO YATAWEZA KUMALIZA MGOGORO HUU NA MADAKTARI WOTE KUREJEA KAZINI NA HIVYO KUREJESHA HUDUMA ZA MATIBABU KATIKA HALI YA KAWAIDA KWA WANANCHI WA TANZANIA. HIVYO SERIKALI INAWAOMBA WOTE WANAOHUSIKA WAFIKE KATIKA MIKUTANO HIYO BILA YA KUKOSA. IMETOLEWA NA OFISI YA WAZIRI MKUU