MAMBO YALIVYOJIRI MKOANI SONGEA LEO


Polisi wakiwatawanya na kuwakamata baadhi ya waandamanaji hao katika manispaa ya Songea baada ya wakazi wa manispaa hiyo wengi wao wakiwa madereva wa pikipiki kuandamana hadi ofisi ya kamanda wa polisi mkoa wa Ruvuma kupinga mauaji ya watu yanayoendelea kwa kasi mjini humo ambao hadi sasa jeshi la polisi halijafanikiwa kuwakamata wauaji.

NA MUHIDIN AMRI,SONGEA

JESHI la polisi mkoani Ruvuma limelazimika kutumia mabomu ya machozi na risasi za moto kuwatawanya wananchi waliokuwa wakiandamana kuelekea ofisi ya mkuu wa mkoa wa Ruvuma na kituo kikuu cha polisi Songea mjini hali iliyopelekea shughuli mbalimbali kusimama.

Hali hiyo ilianza kujitokeza majira ya asubuhi ambapo wananchi wa mtaa wa Lizaboni wengi wakiwa ni madereva wa pikpiki walianza kujikusanya na kuanza maandamano kuelekea kituo kikuu cha polisi kilichopo karibu na uwanja wa majimaji mjini hapa.

Wananchi hao walikuwa wakiimba nyimbo za kulaumu jeshi la polisi wakidai kuwa limeshindwa kudhibiti mauaji yanayoendelea kujitokeza mjini hapa kila mara ambapo hadi sasa zaidi ya watu kumi wameshauawa na watu wasiojulikana.

“Tumeamua kuandamana kwani kimsingi mauaji yamezidi kutokea mjini hapa jana ameuwawa mtu,juzi na usiku wa kuamkia leo ameuwawa mwendesha pikipiki na abiria wake”walisikika wakisema.

Baada ya wananchi hao kukaribia kituo cha polisi walianza kurusha mawe na ndipo polisi walijihami kwa kutumia mabomu ya machozi ambapo wananchi hao na waendesha pikipiki walianza kukimbia ovyo na kupeleka maduka kufungwa kwa hofu ya kuibiwa.

Licha ya biashara mbalimbali kusimama pia ofisi za serikali ikiwemo ofisi ya mkuu wa mkoa na ya mkuu wa wilaya Songea zilifungwa kwa kuhofia waandamanaji kuingia kwenye ofisi hizo na kufanya uharibifu.

Kabla ya maandamano ya leo februari 20 mwaka huu wananchi kutoka kata ya Lizabon waliandamana hadi kwa mkuu wa wilaya ya Songea Thomas Ole Sabaya kulalamikia kukithiri kwa mauaji katani humo ambayo yamekuwa yakifanywa na watu wasiojulikana.

Akijibu malalamiko hayo mkuu huyo wa wilaya alisema kuwa serikali itahakikisha ulinzi unaimarishwa na kwamba aliwataka kuimarisha ulinzi shirikishi ili kukabiliana na matukio hayo maovu.

Februari 19 mwaka huu mkazi wa Lizaboni Bakary Ally(20) aliuwawa kwa kukatwakatwa na mapanga na watu wasiojulikana ambapo februari 20 mwaka huu majira ya saa 3.00 usiku mtu mmoja mkazi wa mtaa wa Kipera shekhe Jamari(65) alikutwa ameuwawa kwa kukatwa mapanga kichwani na watu wasiojulikana wakati alipokuwa akielekea nyumbani kwake.

Marehemu Jamari alikuwa ni mmoja kati ya viongozi wa msikiti uliopo katika eneo hilo la Kipera.

Mauaji hayo yameendelea kujitokeza ambapo mwendesha pikipiki ambaye jina lake halikufahamika mara moja ameuwawa na watu wasiojulikana katika mtaa wa Mji Mwema mjini hapa usiku wa februari 22 mwaka huu na kupelekea wananchi mjini hapa kuishi kwa hofu kubwa.

BARNABA, TWANGA PEPETA NA MSONDO NGOMA JUKWAA MOJA J’PILI HII LEADERS CLUB


African Stars Band “Twanga Pepeta” jumapili tarehe 26-02-2012 kuanzia saa tisa jioni inataraji kufanya onyesho pamoja na Mkali wa muziki wa kizazi kipya Barnaba na bendi kongwe ya Muziki wa Dansi ya Msondo Ngoma Music.

Onyesho linataraji kufanyika katika viwanja vya Leaders vilivyopo maeneo ya kinondoni na matayarisho yote muhimu ya onyesho yamekamilika ikiwa ni pamoja na msanii Barnaba kufanya mazoezi maalum na Twanga Pepeta kwa ajili ya kupiga live.

Martin Sospeter

Meneja Twanga Pepeta

MKUU WA MKOA WA RUKWA AIOMBA SERIKALI KUSAIDIA KUHAKIKISHA UJENZI WA BARABARA ZA LAMI ZINAZOJENGWA MKOANI HUMO ZINAKAMILIKA KWA WAKATI


Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mhe. Injinia Stella Manyanya akizungumza Wilayani Mpanda. Kushoto ni Mhe. Makamu wa Rais Dkt. Mohammed Gharib Billal na Mke wake Mama Asha Billal.

 

NA HAMZA TEMBA-OFISI YA MKUU WA MKOA rukwareviw.blogspot.com
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Injinia Stella Manyanya ameiomba Serikali kupitia Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Mohammed Gharib Billal kusaidia kuhakikisha ujenzi wa barabara za lami zinazoendelea kujengwa Mkoani Rukwa zinakamilika kwa wakati.
Mkuu huyo wa Mkoa alitoa ombi hilo jana mara baada ya kusomwa taarifa ya ujenzi wa barabara za lami zinazoendela kujengwa Mkoani humo kwa Mhe. Makamu wa Rais ambapo taarifa hiyo ilielezea changamoto zinazokabili ujenzi huo ambazo zinatishia kukamilika kwa ujenzi huo katika muda uliopangwa.
Taarifa hiyo iliyowasilishwa na Meneja wa Tanroads Mkoa wa Rukwa Ndugu Florian Kabaka jana iliweza kuainisha changamoto mbalimbali zinazoukabili ujenzi huo ikiwemo ucheleweshwaji wa malipo ya fedha kwa ile miradi inayotemea fedha za ndani hususani barabara za Sumbawanga-Kasanga na Sumbawanga-Mpanda.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo changamoto nyingine ni baadhi ya wakandarasi wanaojenga barabara hizo kukimbiwa na wafanyakazi wao kutokana na ukosefu wa fedha za kuwalipa hali inayopelekea kuzorota kwa ujenzi huo.
Mbali na changamoto hizo, nyingine ni kuchelewa kulipwa fidia wananchi waliothibitika kustahili malipo hayo ili kuepusha shughuli za ujenzi katika maeneo wanayotakiwa kuhama.
Pamoja na changamoto hizo nyingine ni wizi wa vifaa vya ujenzi wa barabara hizo zikiwepo nondo, mafuta, simenti, vyuma na hata mabati. Kwa mujibu wa Meneja huyo wa Tanroads ujenzi huo unatakiwa kukamilika mwakani 2013 lakini kama hali itaendelea kuwa hivyo basi huenda ukamilishaji wa miradi hiyo ukachelewa.
Baada ya kusomwa taarifa hiyo ilifika wakati kwa Mkuu wa Mkoa wa Rukwa kumkaribisha na kumtambulisha Mhe. Makamu wa Rais kwa wananchi wa Wilaya ya Nkasi ambapo amenza ziara akitokea Wilayani Mpanda. Kabla ya kufanya hivyo alilazimika kutumia fursa hiyo kutoa ombi lake rasmi kwa Makamu wa Rais kuhusu ujenzi unaondelea na kuhakikisha kuwa changamoto zinzozikabili barabara hizo zinapatiwa ufumbuzi.
“Wananchi wote wa Mkoa wa Rukwa wanaishukuru sana Serikali yao kwa hatua yake kubwa ya kuleta miradi mikubwa ya ujenzi wa barabara za lami Mkoani hapa kitu ambacho ni cha kujivunia kwa wanarukwa wote, Nitumie fursa hii kuiomba Serikali itusaidie kuondokana na changamoto zinazoikabili miradi hii ili iweze kuakamilika kwa wakati” Alisema Injinia Manyanya.
Serikali imesaini mikataba ya ujenzi wa barabara za lami Mkoani Rukwa kwa barabara za Tunduma-Ikana-Laela, laela-Sumbawanga, Sumbawanga-Kasanga na Sumbawanga-Mpanda. Hadi hivi sasa ujenzi wa barabara kwa baadhi ya maeneo hayo unaendelea na maeneo mengine yamesimama kwa muda kutokana na uhaba wa fedha.
Mhe. Makamu wa Rais yupo Mkoani Rukwa kwa ziara ya kikazi ya siku saba ambapo, ameshatembelea Wilaya ya Mpanda, Sasa yupo Wilayani Nkasi na baadae atamalizia ziara yake Wilayani Sumbawanga amabap atatembelea miradi mbalimbali ya maendeleo, kuizindua na kuweka mawe ya msingi. Ziara yake hiyo itakamilika tarehe 24 Februari 2012 ambapo ataenda Mkoa jirani wa Mbeya kwa ziara kama hiyo ya kikazi.