NAPE ATUNUKIWA SHAHADA YA PILI YA UONGOZI MZUMBE


Watangazaji wa Kituo cha Televisheni cha Chanel Ten Fredy Mwanjala, Salama Hamadi na Zainab Abdul, wakimpa zawadi ya hongera, Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye ambaye ametunukiwa shahada ya pili ya uongozi leo kwenye mahafali ya kumi ya Chuo Kikuu Mzumbe, kwenye ukumbi wa Diamond Jubilee, Dar es Salaam

Nape (kushoto kwenye kona) akiwa na wahitimi wenzake wakati wakinutunukiwa sahada ya pili ya uongozi kwenye mahafali hayo...

Katibu wa NEC ya CCM Itikadi na Uenezi Nape Nnauye akipongezwa na mama yake, Kezia Alfred, baada ya kutunukiwa shahada ya pili ya uongozi katika mahafali ya kumi ya Chuo Kikuu Mzumbe, leo...

VIFUA CHUMA !


Vijana hawa akipasha kuweka misuri sawa kabla ya kuanza kazi yao

Kijana akionyesha misuri yake wakati akipasha kabla ya kuanza kazi yake hiyo...

Vifua mbele ...

Tumezoea kuwaona vijana hawa wengi wao wakiwa katika mageti ya Kumbi maarufu za starehe kwa lengo la kulinda usalama, lakini siku hizi watu hawa wamekuwa na kazi nyingi kulingana na mteja anavyowapangia.

Tumesikia siku za hivi karibuni Mabaunsa kama hawa wamekuwa wakitumiwa na baadhi ya watu wenye fedha zao kwa ajili ya kuwahamisha wananchi katika maeneo fulani na wengine wamekuwa wakitumiwa kuvunja ama kubomoa Nyumba za watu wanaokuwa wamegoma kuhama mahala fulani baada ya eneo hilo kuuzwa.

Kwa kweli Vijana kama hawa hivi sasa wamekuwa ni Tegemeo kila kona kama ambavyo walikutwa Vijana hawa wakijiandaa kwa ajili ya kubeba Kijikiti kidogo tu kilichokuwa na Kijitabu kidogo juu yake na kuingiza ukumbini wakati wa Hafla ya kukabidhi Tuzo za Super Brands kwa Makampuni yaliyofanya vizuri mwaka 2011, iliyofanyika jana usiku katika Ukubi wa Hoteli ya Kilimanjaro Kempisky. Hongereni Vijana kwa kujiajiri kupitia miili yenu Wenyewe.Chanzo ni http://sufianimafoto.blogspot.com/

Godbless Lema Anaelekea Kwenye Ushindi Mkubwa


Ndugu zangu,

Kunako saa tano asubuhi ya leo zoezi la kupiga kura mtandaoni litafungwa. Ni kwenye Pima- Maji ya http://mjengwablog.com . Ni katika mchakato huu wa kumpata mbunge bora Kijana kwa mwaka 2011.

Habari kubwa siku ya leo?

Watu elfu tatu na zaidi wamepiga kura ndani ya saa 24 zilizopita. Ni rekodi mpya. Inaonyesha hamasa kubwa ya hususan vijana kushiriki siasa. Kijana Godbless Lema anaelekea kwenye ushindi mkubwa wa kura za mtandaoni.

Anatarajiwa kuzoa kura si pungufu ya 3500. Atafanya hivyo huku mpinzani wake wa karibu Zitto Kabwe anatarajiwa kuzoa kura zipatazo 2600. Hivyo basi, Godbless Lema atakuwa mbele ya Zitto Kabwe kwa tofauti ya kura takribani 2000.

Tafsiri yake?

Pima- Maji hii , hata kama kuna wasiotaka kukubali, inabaki kutusaidia kusoma alama za nyakati. Upepo wa kisiasa nchini umedhihirika kubadilika. Ni ukweli , kuwa asilimia zaidi ya sitini ya WaTanzania watakaoshiriki kupiga kura kwenye Uchaguzi Mkuu wa 2015 watakuwa ni vijana. Na wengi walioshiriki kupiga kura hizi za mtandaoni ni vijana.

Hivyo basi, matokeo ya Pima-Maji hii si habari njema kwa Chama Cha Mapinduzi ambacho vijana wengi kwa sasa wanaelekea kukipa mgongo. Kuna ambao, ndani ya Chama Cha Mapinduzi wasingependa ukweli huu uelezwe kwa njia ya Pima-Maji au maandiko kama haya. Lakini, huko ni sawa na mwanadamu kujaribu kukikimbia kivuli chake. Kwa walio makini kisiasa, haya si matokeo ya kubeza wala kumtafuta mchawi, bali kuyafanyia kazi.

Inachokosea CCM

Kutumia vyombo vya dola kuikandamiza Chadema na upinzani kwa ujumla katika wakati ambao wananchi wangetaka kuiona CCM walioiheshimu kwa miaka mingi ikionyesha tofauti na kwenda na wakati uliobadilika. The old communistic style ya utawala wa Chama Kimoja na Chama kushika hatamu imepitwa na wakati.

Wananchi wameshabadilika na CCM ibadilike pia. CCM kwa sasa hawahitaji kuikandamiza Chadema bali kui-engage Chadema kwenye hoja za msingi za kitaifa. CCM bado ina hazina ya vijana mahiri ambao katika kuendesha fair politics wangeng’aa badala ya kufubaa kama ilivyo sasa. Kwa bahati mbaya, taswira ya CCM kwa vijana wengi kwa sasa ni chama ‘ kandamizi’ . Hivyo basi, vijana wengi hawa-sympathy na CCM inayoonekana kucheza rafu za wazi wazi. Kwa maana hiyo, hata vijana nyota wa CCM wanashindwa kung’ara kwenye timu inayocheza rafu na inayozomewa na watazamaji wengi.

Chadema nao hawako salama

Matokeo ya kura hizi yanaonyesha uwepo ndani ya Chadema, viongozi vijana wawili, ambao, kwenye kuelekea uchaguzi wa ndani wa chama hicho mwakani, wana uwezo wa kukigawa chama hicho kutokana na ushawishi wao mkubwa walio nao kwa vijana. Chadema kwa sasa kinaungwa mkono na vijana wengi. Siasa za makundi, ambazo bila shaka zimo pia ndani ya Chadema, zaweza, kama Zitto na Lema wasipotanguliza maslahi ya nchi, kupelekea kukibomoa chama chao, na hivyo basi, kubomoa siasa za upinzani hapa nchini.

Tofauti ya Zitto na Lema

Kitabia, wapiga kura wengi wa sasa hawaangalii tofauti za kiitikadi kivyama au wagombea, bali misimamo ya vyama na misimamo ya wagombea katika masuala ya msingi yanayowagusa.

Zitto Kabwe ni rafiki yangu. Nimemfahamu kwa miaka mingi sasa. Zitto Kabwe ninayemfahamu ni mmoja wa wanasiasa mahiri mwenye sifa kuu mbili; ana uwezo wa kujenga hoja na kubomoa hoja za wapinzani wake, kwa nguvu za hoja. Zitto ni moderate politician, pragmatic and less of dogmatic, Zitto anaamini unaweza kufanya mabadiliko kwa kushirikiana na mfumo na labda hata kuwa ndani ya mfumo. Lema anachagua njia ya kupambana na mfumo moja kwa moja kutokea nje.

Zitto anaamini na angependa harakati za kufikia mabadiliko zifuate mkondo wa kisiasa na kwa taratibu za kisiasa ikiwamo kuyapa nafasi majadiliano. Hivyo basi, kutafuta muafaka au maridhiano ya kisisa kwa njia ya mazungumzo. Lema anaamini mabadiliko hayaji bila kupambana na hata kujitoa muhanga.

Kimsingi huwezi kusema Lem a ni bora kuliko Zitto au kinyume chake. Wanatofautiana. Na kichowatofautisha ndicho kinachowatofautisha wapiga kura pia. Kwa hapa tulipo, njia ya Zitto katika kufanikisha mabadiliko ya kisiasa ina wafuasi wachache miongoni mwa vijana. Na njia ya Lema ina wafuasi wengi miongoni mwa vijana.

Hata hivyo, katika uwanja wa sasa wa kisiasa, na hususan kwa vijana wenye hasira na kuchukizwa na ubinafsi wa baadhi ya viongozi wao huku wao ( Vijana) wakiwa hawana hakika ya ajira wala mikopo ya vyuo vikuu. Kwa vijana wengi, ’Kamanda’

Godbless Lema , kama wanavyopenda kumwita, ni kielelezo cha kiongozi mwenye ujasiri hata wa kupambana na nguvu za dola katika kuwatetea wanyonge wengi ambao vijana wengi wanajihesabu kuwa katika kundi hilo.

Kwa vijana wa kizazi hiki, Godbless Lem a ni kiongozi jasiri. Ni kiongozi shujaa kwenye mapambano yao. Na hatari ya vijana wa sasa, hawaamini katika njia ya Mahtma Ghandi kwenye kuleta mabadiliko. Wako tayari kuifuata njia ya Steve Biko. Njia ya kiharakati ikiwamo mapambano na dola. Busara ni kuwepo na uwiano wa njia ya harakati na mazungumzo. Uwiano wa Zitto na Lema. Hivyo basi, uwezekano wa kutafutwa njia ya tatu itakayotokana na kuunganisha mazuri ya njia ya Zitto na Lema.

Kwanini Lema ni maarufu?

Ni pale dola inapotumia bunduki kuua nzi ndipo inapowageuza nzi kuwa nyuki wanaozaliana kwa wingi. Ndipo inapozalisha mashujaa kwenye nchi yenye mamilioni wanaojiona wako kwenye hali ya kukandamizwa. Ndipo inapojiandalia kaburi lake.

Tuzifatute Hekima za Maaskofu Pengo na Laizer

Kwenye gazeti la Majira la Desemba 13 mwaka huu imeandikwa;

“Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Kaskazini Kati, Dkt.Thomas Laizer, amesema Serikali isifanye kazi ya kudhoofisha nguvu ya vyama vya upinzani hasa wakati wa kupiga kura na kama hali hiyo itaendelea, wananchi watashindwa kuvumilia hivyo kusababisha uvunjifu wa amani na utulivu uliopo nchini.

Alisema Chama cha Demokrasi na Maendeleo (CHADEMA), kina umaarufu mkubwa kuliko vyama vingine vya siasa nchini hivyo umefika wakati wa Serikali kuviheshimu na kuvipa nafasi vyama vya upinzani ili viweze kufanya shughuli zao bila vikwazo hasa katika chaguzi mbalimbali.” ( Majira, Desemba 13, 2011)

Na leo Ijumaa kwenye gazeti la Mwananchi inaripotiwa; “ Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, amesema, ongezeko la posho kwa viongozi wa umma ni ubinafsi na kuonya kama Uchaguzi Mkuu mwaka 2015 utafanyika bila ya kuwako kwa Katiba Mpya, utagubikwa na ghasia.”
Askofu anaongeza kusema kuhusu posho; “Viongozi wa Serikali na umma wakiwamo wabunge, wanapaswa kuacha ubinafsi na badala yake wafanye kazi kwa kuwafikiria zaidi wananchi kuliko maslahi binafsi.

Sisi Wakristu tunaamani kuwa, Kristu licha ya kuwa alitumwa na Mungu Baba kuja kutukomboa wanadamu alifanyika mwili na kuzaliwa katika hali ya umaskini na ufukara ili atukomboe. Viongozi wa Serikali, dini na watumishi wa umma, inatupaswa kuiga mfano huo.” Anasema Kardinali Pengo.
Na kuhusu Katiba hakukosa la kutuasa, anasema Katiba ni chombo muhimu kinachotakiwa kufanya kazi kwa umakini na kuhakikisha inapatikana kabla ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015. Askofu anaonya, kuwa bila Katiba Mpya, taifa linaweza kuingia matatizoni kwa kuwa katiba ndio inayoelekeza wananchi kuchagua viongozi.

“Tumeshasema Katiba iliyopo kwa sasa ni mbovu, tuchukulie suala hili “very serious (kwa uzito), tukamilishe kabla ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, vinginevyo tutaingia matatizoni.”

Askofu anasema pia; “ Jibu la kufikia kwenye siasa bora ni, kulifanyia kazi suala la Katiba, ambayo ndio itakayoamua wananchi wanataka kutawaliwa na watu wa namna gani. Kwa sasa bado tunaishi ndani ya mawazo na mtazamo wa chama kimoja cha siasa katika mfumo wa vyama vingi vya siasa. Ndio sababu, mawazo ya chama ndio yanayochukuliwa kama mwongozo wa Serikali. Lakini tukiweka mkazo katika Katiba, tunapaswa kutambua tunatengeneza katiba ya nchi na si ya chama kimoja.” ( Kardinali Pengo, Mwananchi, Desemba 16, 2011)

Naam, kuna hekima kubwa katika kauli za viongozi hawa wakuu wa kidini. Na wanadamu tunapaswa kuitafuta hekima . Mfalme Suleiman aliambiwa ndotoni aombe kitu chochote kwa Mola wake, naye akajibu; “ Ewe Mola wangu, nipe mimi mtumwa wako moyo wa adili ili niwahukumu watu wako, na kupambanua mema na mabaya, maana ni nani awezaye kuwahukumu hawa watu wako walio wengi?”

Hivyo basi, Mfalme Suleiman alichagua hekima. Maana, ni Mfalme Suleiman huyo anayekaririwa na vitabu vya dini akitamka, kuwa; “ Watu wangu wanaangamia kwa kukosa hekima”. Naam, hekima ndilo jambo lililo bora kabisa kwa mwanadamu kuwa nalo. Mwanadamu aliyepungukiwa hekima ana hasara kubwa maishani.

Hekima ni tunu na kipaji ambacho Mwenyezi Mungu amewajalia waja wake, ili nao waweze kupambanua na kuamua kati ya yaliyo mema na maovu. Duniani hakuna shule ya hekima.

Tuliokulia pwani tunajua , kuwa mtu mzima ukiambiwa ’ mwanaharamu’ n i tusi baya. Mwanaharamu haina maana tu ya mtu aliyezaliwa nje ya ndoa. Mwanaharamu aweza pia kuwa ni mtu mwenye matendo ya hovyo hovyo, mtu asiye na adili. Mtu asiye mwungwana.

Na mtu mzima unayejiona kuwa ni mwuungwana ikatokea ukasimama na mwanaharamu. Kisha watu wazima wenzako wakaambiwa wachague mmoja kati yenu. Ikitokea watu wazima hao wakamchagua mwanaharamu. Basi, kuna mawili; ama watu wazima hao nao ni wanaharamu au wewe uliyesimama na mwanaharamu ni mwanaharamu zaidi. Watu wazima hao watakuwa wamechagua ’ afadhali’ ya mwanaharamu. Na tuendelee kuitafuta hekima.

Maggid Mjengwa,

Iringa.
Mjengwa Blog::Habari,Picha,Matangazo