MAKAMU WA RAIS DK GHARIB BILAL AWATEMBELEA WANANCHI WALIOATHIRIKA NA MAFURIKO DAR ES SALAAM


Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akisalimiana na mmoja kati ya wananchi waliohifadhiwa katika Kambi ya Shule ya Sekondari ya Azania, waliookolewa katika maeneo yaliyojaa maji kutokana na mvua zilizonyesha jijini Dar es Salaam kuanzia majuzi, wakati Makamu alipofika katika Kambi hiyo leo Desemba 23, kwa ajili ya kuwapa pole waathirika hao…
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akizungumza na Bi. Monica Luis, Mkazi wa Jangwani aliyeathirika na mafuriko ya Mvua kubwa iliyonyesha jijini kuanzia majuzi, wakati makamu alipotembelea katika Kambi ya Shule ya Sekondari Azania jijini Dar es Salaam leo Desemba 23, kwa ajili ya kuwapa pole waathirika wa mafuriko hayo…
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akizungumza na baadhi ya wananchi waliohifadhiwa katika Klabu ya timu ya Yanga ya Jijini Dar es Salaam, wakati alipowatembelea kuwapa pole wananchi hao walioathirika na mafuriko ya Mvua kubwa zilizonyesha jijini kuanzia majuzi. Makamu alifanya ziara hiyo ya kutembelea baadhi ya kambi za waathirika leo .Desemba 23…
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akisikiliza maelezo ya jinsi maji yalivyokuwa yamejaa wakati wa mvua kubwa iliyosababisha mafuriko, kutoka kwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mecky Sadick (kulia), wakati alipotembelea kuwapa pole wananchi waliokuwa wamehifhadhiwa katika Klabu ya Yanga, iliyopo Jangwani leo Desemba 23. Picha na Muhidin Sufiani-Ofisi ya Makamu Wa Rais.

Rais Kikwete awakumbuka watoto wanaoishi mazingira hatarishi, Singida


:Mkuu wa Mkoa Singida Dk.Parseko Kone, kwa niaba ya Rais Dk.Jakaya Kikwete, akikabidhi zawadi ikiwemo mchele na mbuzi wawili kwa ajili ya kituo cha Malezi Kititimo kilichopo mjini Singida, kwa ajili ya watoto hao kusherehekea vizuri sikukuu ya Krismasi,Watoto hao wanaishi mazingira hatarishi, wa pili kutoka kulia ni mkuu wa wilaya Singida Paschal Mabiti na kulia kabisa ni kaimu mkurugenzi manispaa Singida, Simon Hoja.

Singida,Desemba 23,2011.
RAIS Jakaya Kikwete ametoa zawadi ya sikukuu ya Krismasi, kwa ajili ya watoto wanaolelewa na kituo cha Malezi Kititimo, kilichopo Mjini Singida.

Zawadi hiyo ya Krismasi kwa kituo hicho, imetolewa jana ijumaa, na Mkuu wa Mkoa wa Singida Dk.Parseko Kone, kwa niaba ya Rais Dk.Jakaya Kikwete.

Akikabidhi zawadi hizo, Rais Dk.Kikwete amewatakia kila la heri watoto hao, katika kusherehekea sikukuu hiyo, na anawaomba wajione sawa na watoto wengine duniani katika Krismasi hiyo.

Msaada huo wa chakula uliotolewa ni mchele kilo 60, mafuta ya kupikia dumu moja kubwa, mbuzi wawili na viungo mbalimbali kwa ajili ya mapishi,vyote vikiwa na thamani ya Sh.550,000.

Mkuu wa mkoa Singida, Dk.Kone, naye aliunga mkono msaada huo kwa kutoa katoni moja ya juisi, boksi moja la biskuti na mifuko ya pipi.

Wakitoa shukrani hiyo, watoto hao walimshukuru Rais Kikwete kwa kuwakumbuka kipindi hiki cha kusherehekea sikukuu ya Krismasi na mwaka mpya.
Na Elisante John.

Salaam za X-Mas na Mwaka Mpya za Mchungaji Peter Msigwa, Mbunge wa Iringa Mjini (Chadema)


Waraka mahususi kwa viongozi wa dini wa Tanzania:
kuweni macho na wanasiasa wenzangu

Utangulizi

Ndugu Wanahabari,
Kwa nafasi yangu kama raia, Mbunge ninayewakilisha wananchi wa Jimbo la Iringa Mjini na Watanzania wote kwa ujumla na mmoja wa viongozi wa dini/dhehebu nchini, naomba kutumia fursa yenu na ya vyombo vyenu vya habari kutoa ujumbe mahususi kwa viongozi wenzangu wa kidini kwa manufaa ya taifa letu.
Ninapowasilisha salaam zangu hizi za X-Mas na Mwaka mpya wa 2012, ningependa kusisitiza yafuatayo kwa viongozi wenzangu wa dini, kuhusiana na nini hasa unapaswa kuwa wajibu wetu kuhusiana na mwenendo wa viongozi wetu wa kisiasa (mimi pia nikiwa mmoja wao);

Nianze kwa, kuwapongeza viongozi wenzangu wote wa dini waliojitokeza hadharani au kupitia vyombo vya habari hivi karibuni kupinga kusudio au mpango wa kuongeza posho za vikao kwa wabunge. Suala la malipo ya posho za vikao (Sitting allowance) kwa wabunge na watumishi wa umma pamoja na mpango wa kuongeza posho hizo kutoka sh 70,000 hadi sh 200,000 (kwa siku ya kikao), kama ulivyotangazwa na Mhe. Spika wa Bunge, Anne Makinda, hivi karibuni, limegusa hisia za Watanzania wengi wakiwemo viongozi wenzangu wa dini ambao naungana nao kuzipinga nikisisitiza msimamo wa siku nyingi wa chama chetu (Chadema).
Pongezi hizi zinazingatia ukweli kuwa katika suala hili la posho,Baadhi ya viongozi wa dini wameweza kuchukua wajibu wao kikamilifu wa kuwa juu ya wanasiasa wenye malengo mabaya tofauti na desturi iliyoanza kujengeka hivi karibuni ya baadhi ya wanasiasa hususan wale wa Chama cha Mapinduzi (CCM) kupenda kuwatumia vibaya baadhi ya viongozi wa dini na nyumba za ibada kama sabuni ya kujisafishia uchafu wao na ngazi ya kufikia malengo ya kuutafuta urais au ubunge na udiwani (uongozi mchafu). Ingawa kanisa ni mahali pa kusafishwa uchafu na kila mtu anakaribishwa, lakini tumkumbuke yule Simon Mchawi katika kitabu cha matendo ya mitume,aliyejaribu kununua kipawa cha Roho mtakatifukwa faida yake binafsi,Ndipo mtumishi wa Mungu Petro alipomwambia apotelee mbali pamoja na pesa yake.
Nawasihi viongozi wa dini wenzangu kwamba kamwe tusikubali kuwa mawakala wa kufanikisha mbio za urais mchafu. Tusikubali kuwa chini ya wanasiasa maana jukumu letu la kuwanusuru wanadamu kiroho kwa kuwaongoza kumcha Mungu, ni jukumu zito na kubwa kuliko uroho wa madaraka unaowakimbiza baadhi ya wanasiasa kwenye nyumba za ibada.
Ni udhalilishaji mkubwa wa huduma ya kiroho pale viongozi wa dini tunapowakaribisha wanasiasa kufanya shughuli kama za uzinduzi wa makanisa au albamu za nyimbo za kidini kana kwamba wao ndio wenye upako, utukufu na mamlaka zaidi ya kubariki kinachozinduliwa kuliko sisi viongozi wa dini wenyewe.
Tabia kama hii ya kuwatanguliza mbele wanasiasa kwenye shughuli za kiroho badala ya kuacha huduma hii ijitegemee yenyewe (maana Mungu ni Mkuu na mwenye uwezo kuliko siasa), kwa namna moja au nyingine imekuwa ndio kichocheo cha kufanya wanasiasa kutafuta pesa kwa gharama yoyote, ilimradi wakiitwa kwenye mialiko hiyo waweze kutoa fungu kubwa wakiamini itawajenga kisiasa hata kama hawana nia ya kweli na Mungu.

Tusikubali kamwe kutumiwa vibaya na wanasiasa wanaojipenyeza kwenye matukio mbalimbali kama ya harambee na uzinduzi wa albamu za nyimbo za kiinjili, kwa lengo la kujitangaza, kujisafisha na kujipendekeza kwa umma uliowakataa au kukosa imani nao.
Tusikubali nyumba takatifu za ibada zigeuzwe viwanja vya kampeni za kisiasa na wala tusiwe chanzo cha kuiingiza nchi yetu katika mgawanyiko na machafuko ya kidini kwasababu tu ya kuwabeba baadhi ya wanasiasa ambao ama kwa sababu ya uchafu wao au umma kukosa imani nao, wameona hawawezi tena kuwa na uhalali wa kujitangaza wala kujijenga tena kwenye majukwaa ya kisiasa bila kwanza kukimbilia makanisani. Binafsi naamini, mwanasiasa msafi anayejiamini na anayemcha Mungu kwelikweli haitaji harambee au tukio lolote la kujinadi kanisani , maana huko si pahali pake.
Najua kuwa Watanzania wengi wanakerwa na tabia ya baadhi ya sisi viongozi wa dini kama maaskofu, wachungaji na mapadri kubabaikia wanasiasa kwa kiasi cha kuonekana wanaidhalilisha huduma hii kuu. Kanisa likitakiwa kuzinduliwa – mwanasiasa, uzinduzi wa nyimbo ya injili – mwanasiasa, ununuzi wa magitaa – mwanasiasa, ununuzi wa maspika – mwanasiasa. Hivi hawa wanasiasa wana upako gani kana kwamba kazi ya Mungu haiwezi kufanyika bila wao?
Tunapokwenda kusherehekea siku kuu hii ya X Mas na Mwaka Mpya, ninawasihi tena viongozi wenzangu wa kidini, kwamba tumkumbuke nabii Baalam ambaye vitabu vitakatifu vinaeleza jinsi alivyoifanyia biashara huduma yake ya kinabii mpaka alisababisha Punda aongee;

Tumkumbuke mtumishi wa nabii Elisha, aliyeitwa Gehazi, ambaye vitabu vitakatifu vinatufundisha kwamba alipenda pesa na zawadi akasahau mwito wake wa kitume mpaka ukoma wa Nahaman ukahamia mwilini mwake;
Tumkumbuke Esau aliyeuza haki ya uzaliwa wake wa kwanza kwa njaa ya muda mfupi (dengu,mlo moja tu);
Na tumkumbuke Yuda Eskarioti ambaye alimuuza mwokozi wetu, Yesu Kiristu, kwa vipande thelathini vya fedha, na kwa hiyo, sisi viongozi wa dini tusikubali kamwe kuwauza Watanzania wenzetu kwa pesa za wanasiasa wachafu.

Nasisitiza tena, kwamba sisi viongozi wa dini tunapaswa kuwa viongozi na sio wafuasi wa wanasiasa, tunapaswa kuwaonyesha njia wanadamu wote wakiwemo wanasiasa na sio wanasiasa watuonyeshe njia sisi, maana kufanya hivyo ni kulishusha thamani neno la Mungu.
Naamini kama taifa kwa ujumla tuna hali za duni za kimaisha zinazotugusa pia sisi viongozi wa kiroho, lakini hii isisababishe tukasahau misingi yetu ya kitume kana kwamba Mungu aliyetuita ametuacha. Naamini sisi viongozi wa dini tukisimama imara bila kuyumba, Tanzania yetu inayougua umaskini, ujinga, maradhi na ufisadi, hatimaye itaponywa. Hizi ndio salamu zangu za mwaka mpya kwa viongozi wa dini ambao naamini kupitia wao Watanzania wote wataongozwa vema.

Nawatakia kheri na fanaka ya X- Mas na Mwaka Mpya.

Mungu ibariki Tanzania,

BABA WA MAPACHA WATATU’ ATOA SHUKRANI KWA WALIOSAIDIA KUNUSURU MAISHA YA WANAE


Watoto Mapacha Rehema, Amani na Neema ambao hivi sasa wamefikisha miezi mitano…
Watoto mapacha katika pozi…
Mmoja wa Wasamaria Wema Dada Norah alipowatembelea Mapacha hao hivi Karibuni .
Watoto mapacha katika pozi.
Watoto Mapacha Rehema, Amani na Neema ambao hivi sasa wamefikisha miezi mitano.
Kijana Edwin Dossantos na mkewe waliojaliwa kupata watoto watatu mapacha mwezi wa 7 mwaka huu ametoa shukrani zake za dhati kwa wasamaria wema wote waliomsaidia kwa hali na mali kutoa michango kwa ajili ya malezi ya watoto hao kutokana na halisi ya kipato chake kuwa cha chini na maisha kuzidi kuwa magumu.

Akizungumza na MO BLOG ilipomtembelea nyumbani kwake eneo la Kimara jijini Dar es Salaam, Dossantos amesema ni msaada wa wasamaria wema ndio umemuwezesha kumudu gharama za matumizi kwa ajili ya watoto hao haswa ukizingatia hakuwa na kazi.

Aidha Dossantos licha ya kuwashukuru wanao onekana katika orodha hii, pia amewashukuru na wale ambao hawakutaka kujulikana waliomsaidia kupitia mawakala wa M-Pesa pasipo kujitaja majina yao, ambao licha ya kuwashukuru amesema hawakumtendea haki kwa kuwa wamemnyima fursa ya kuwashukuru kwa majina yao wala namba zao.
Dossantos ametoa shukrani kwa watu waliosaidia kwa namna mbalimbali kama wanavyoonekana katika orodha ifuatayo.:-
Mr. Frank wa DSM, Mrs. Norah wa Silver Boutique, Mama Sige wa KIBAMBA, Mrs.Pamela wa USA, Mr. Sagday wa DSM, Mrs. Caroline Kazinza wa AZANIA BANK-Tegeta, Mrs. Emakulata wa UK, Miss Nyota Omary wa NORWAY, Mr. Joshua wa DSM, Mrs.Pamela wa DSM, Mrs.Mosha wa ARUSHA, Mrs. Lestituta wa DSM, Mrs. Theresia na Mrs Zahara wa Hisense DSM, Mr. Shabiby wa GAIRO Morogoro, Mrs. Fane wa DSM, Mrs. Ikupa wa AZANIA BANK-Tegeta DSM, Mrs. Vale wa AZANIA BANK-Tegeta DSM, Miss Hoyce Temu wa Channel Ten DSM, Mrs. Mercy Mariale wa DSM, Mr. Rongen Kambugu wa Kigali RWANDA, Advocate Komba wa NSSF-DSM,  Miss Jehn wa DSM, Mr. Freya Mahinya wa Zanzibar, Mr. Chube wa DSM,Mr. Yusuph Mdoe wa DSM, Mr.Emmanuel Messo wa WORLD BANK-DSM, Mr. Deogratius Rweyunga wa ITV-DSM, Mr. Iddi Kibwana wa TTCL-DSM, Mr. Hashim Lundenga wa DSM na Bi. Asia Waziri Moyo wa Zanzibar.
Hata hivyo amesema watoto hao ambao kwa sasa wanaumri wa miezi 5 bado wanahitaji msaada angalau hadi wafikishe umri wa miezi 6 ambapo watakuwa wanaanza kula vyakula vya kawaida.
Katika hatua nyingine Edwin Dossantos ametoa ombi kwa msamaria mwema atakayekuwa na uwezo wa kumpatia nafasi ya kazi yoyote itakayompatia kipato cha kuweza kumudu gharama za malezi ya watoto hao.
Amesema bila ya yeye kuwa na kazi ya kumuingizia kipato anaweza kuja kwa wasamaria kuomba misaada kila mara, hivyo ameshukuru kwa kumpatia kile alichokiita samaki na sasa anaomba nyavu (Kazi) ili avue mwenyewe.
Edwin Dossantos anapatikana kwa simu ya mkononi namba 0719 909085 na 0767 646599.